Mkuu wa Shule ya Sekondari Kawe Ukwamani Safina Egha akizungumzia kukamilika kwa hafla ya ‘Kawe Dar’, Ofisini kwake, shuleni hapo, leo.
Na Bashir Nkoromo, Kawe
Maandalizi ya hafla ya siku ya kuanzishwa kwa Shule ya Sekondari ya Kawe Ukwamani iliyopo Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, ‘Kawe Day’ yamekamilika na itafanyika keshokutwa, Ijumaa, Agosti 7, 2020 katika shule hiyo kwa maonyesho na burudani mbalimbali.
Akizungumza leo, Kawe, jijini Dar es Salaam, Mkuu wa shule hiyo Safina Egha, amesema, ‘Kawe Day’ ni siku maalum ambayo imetengwa kwa ajili ya kuwakutanisha wazazi, wadau wa maendeleo na viongozi wa shule, kwa ajili ya kuona na kujadili mustakabali mzima wa maendeleo ya shule na changamoto zilizopo ili kuifanya shule hiyo kupiga hatua zaidi katika nyanja zote kitaaluma tangu shule hiyo ilipoanza rasmi tarehe Aprili 12, 2006.
” ‘Kawe Day’ ya mwaka huu tunaifanya ikiwa ni kwa mara ya pili, mwaka jana tuliifanya kwa mara ya kwanza mwezi kama huu, lakini tarehe 8, ambayo ndiyo tarehe tuliyoipanga kufanyika kila mwaka, lakini mwaka huu tumelazimika kurudisha siku moja nyuma, kutokana na sababu zilizojitokeza na kuwa nje ya uwezo wetu kuzizuia, lakini tunatarajia kwamba itafana na kukidhi matarajio yetu”, alisema Mkuu wa shule hiyo.
Alisema, katika hafla hiyo pamoja na mambo mengine kutakuwa na maonyesho ya zana za ufundishaji huku wanafunzi wa vidato vyote (Cha kwanza hadi cha nne) wakionyesha walivyofundishwa na kiasi walivyoelewa yale waliyofundishwa na kwamba maonyesho hayo yatakuwa kwa vitendo zaidi.
Egha, alisema, jambo lingine ambalo litapata kipaombele kwenye hafla hiyo itakuwa ni uongozi wa shule kuwaeleza wadau wa maendeleo na wazazi hali ya kitaaluma na changamoto zilizopo kwenye shule hiyo ili kuona kwa pamoja namna zinavyoweza kutatuliwa.
“Mnajua kwenye hafla hii ya ‘Kawe Day’ pamoja na viongozi wetu wanaosimamia elimu katika Wilaya yetu ya Kinondoni, pia tumewaalika wazazi na wadau mbalimbali wa maendeleo, hivyo pamoja na kuwaeleza hatua nzuri tuliyopo kitaaluma lakini pia tutawaeleza changamoto zinazoikabili shule ili kuona jinsi gani wanaweza kutusaidia kuzitatua”, alisema.
Alizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili shule kuwa ni pamoja na vyoo kujaa maji katika mda mfupi, uhaba wa kompyuta na mashine ya kurudufia (photo copy machine), na kufafanua kuwa kuhusu vyoo kujaa maji kwa muda mfupi, hali hiyo inatokana na eneo la ardhi shule ilipo kuwa oevu kwa hivyo maji hujaa kutokana na chemichemi ya maji kutoka ardhini na kwamba ili kuondoa tatizo hilo, inatakiwa kujengwa karo kubwa pembeni mwa vyoo ili kuwezesha maji kujihaulisha kwenda kwenye karo hilo vyoo vinapokaribia kujaa.
“Kuhusu Komyuta, hapa shuleni tuna kompyuta moja tu ambayo haiwezi kukidhi mahitaji makubwa tuliyonayo na mashine ya kurudufia ni kama hatuna, maana tulipewa kwa mkopo kwa mda mrefu sasa na bado hatujalipa, hivyo tutawaomba wadau wa maendeleo watusaidie kulipia”, alisema.
Alisema, katika hafla hiyo mgeni rasmi atakabidhi zawadi mbalimbali kwa wanafunzi waliofanya vizuri zaidi katika mitihani maalum ambayo wanafunzi watakuwa wameshaifanya na kwamba walimu pia ambao watakuwa wameongoza kufaulisha zaidi watoto nao watazawadiwa zawadi mbalimbali.