Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akilihutubia Taifa kwenye Sherehe ya Uzinduzi wa Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu leo ambapo ujumbe wa mwaka huu Nanenane kwa maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Kiongozi Bora 2020.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizindua Muongozo wa Kitaifa wa Uongezaji wa Virutubisho katika matumizi ya mazao ya Chakula wakati wa Uzinduzi wa Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu leo ambapo ujumbe wa mwaka huu Nanenane kwa maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Kiongozi Bora 2020.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akimkabidhi Muongozo wa Kitaifa wa Uongezaji wa Virutubisho katika matumizi ya mazao ya Chakula Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima mara baada ya kuuzindua Muongozo huo leo katika uzinduzi wa Sherehe ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane kitaifa iliyofanyika katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizindua Jengo la Kituo cha Elimu kwa Wakulima Kanda ya Ziwa Mashariki wakati wa Uzinduzi wa Sikukuu ya Wakulima Nanenane iliyofanyika leo Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu. ambapo ujumbe wa mwaka huu Nanenane kwa maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Kiongozi Bora 2020.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akimsikiliza Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Mlingano Dkt. Catherine Senkoro alipokuwa akimuelezea kuhusu Utafiti wa mazao ya aina mbalimbali ya Kilimo alipotembelea Banda la Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI katika Viwanja vya Maonesho ya Nanenane vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Baadhi ya watumishi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Mlingano alipotembelea Banda la Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI katika Viwanja vya Maonesho ya Nanenane vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiangalia baadhi ya Mazao ya aina mbalimbali ikiwemo Vitunguu maji, Nyanya na Viazi Mviringo alipotembelea mabanda maonesho katika Viwanja vya Maonesho ya Nanenane vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiangalia baadhi ya Bidhaa za aina mbalimbali ya Kilimo ikiwemo alipotembelea mabanda maonesho katika Viwanja vya Maonesho ya Nanenane vya Nyakabindi Mkoani Simiyu leo kulia Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiangalia mazalio ya Samaki alipotembelea Banda ya JKT katika Viwanja vya Maonesho ya Nanenane vya Nyakabindi Mkoani Simiyu leo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiangali Ng’ombe wa Maziwa kwenye mabanda ya maonesho katika Viwanja vya Maonesho ya Nanenane vya Nyakabindi Mkoani Simiyu leo. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
………………………………………………………………………………………..
HOTUBA YA MHESHIMIWA SAMIA SULUHU HASSAN, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA UZINDUZI WA MAONESHO YA KILIMO NA SHEREHE ZA WAKULIMA NANE NANE
TAREHE 01 AGOSTI, 2020 KATIKA
VIWANJA VYA NYAKABINDI – MKOANI SIMIYU
Mheshimiwa Japhet N. Hasunga, Waziri wa Kilimo;
Mheshimiwa Luhaga Mpina, Waziri wa Mifugo na Uvuvi;
Waheshimiwa Mawaziri wote mliopo;
Mheshimiwa Anthony Mtaka, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu;
Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa;
Waheshimiwa Manaibu Waziri;
Ndugu Gerald M. Kusaya, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo;
Ndugu Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu mliopo;
Makatibu Tawala wa Mikoa;
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;
Waheshimiwa Wabunge;
Wadau wa Maendeleo;
Wakurugenzi wa Mamalaka za Serikali za Mitaa;
Viongozi wa Vyama vya Siasa;
Viongozi wa Dini;
Wakulima, Wafugaji, Wavuvi na Wanaushirika;
Ndugu Wanahabari;
Wageni Waalikwa;
Ndugu Wananchi
Mabibi na Mabwana;
Asalaam Aleikum Bwana Asifiwe; Mwadila wa Baba na Wamayo/Iminza/ Ise Simiyu Ise!
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutufikisha Simiyu salama salimini na kuweza kujumuika nanyi leo. Kama mnavyofahamu, juzi tumemaliza siku saba za maombolezo ya mpendwa wetu, Mzee wetu, Kiongozi wetu na Rais wetu Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mheshimiwa Benjamin William Mkapa ambaye alitutoka usiku wa kuamkia Ijumaa ya tarehe 23 Julai 2020. Naomba tusimame kwa dakika moja ili tumuombee Kiongozi wetu. Mungu Ailaze Roho ya Marehemu Mahali Pema Peponi. Amina.
Nichukue fursa hii kumshukuru Mkuu wa Mkoa Simiyu – Mkoa Mwenyeji, Mheshimiwa Mtaka akishirikiana na Wakuu wa Mikoa jirani ya Mara na Shinyanga pamoja na Kamati ya Maandalizi, kwa maandalizi mazuri ya Maonesho ya 28 ya Kilimo na Sherehe za Wakulima Nane Nane zinazofanyika ngazi ya Kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi hapa Simiyu.
Kwa wananchi wa Simiyu nawashukuru sana kwa mapokezi mazuri na ukarimu wenu ambao mmekuwa mkinionesha mara kwa mara ninapotembelea Mkoani kwenu. Hii ni mara yangu ya pili kushiriki maonesho haya na nimeshafanya ziara pia Mkoani hapa. Hakika ukarimu wenu kwangu hauelezeki. Mungu awabariki sana. Hongereni pia kwa kuweza kumudu kwa ufanisi mkubwa uenyeji wa maadhimisho haya kwa miaka mitatu mfululizo.
Kabla ya kuendelea mbele na hotuba yangu niruhusuni niwape salamu kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Rais anawasalimu sana na anawatakia mafanikio katika maadhimisho haya ya Sherehe za Wakulima Nane Nane 2020. Aidha, Mheshimiwa Rais anawapongeza na kuwashukuru sana wakulima, wavuvi na wafugaji wote kwa kazi nzuri mnayofanya ya kuzalisha mazao yanayotuhakikishia uhakika na usalama wa chakula, kipato na kukuza ajira.
Nitoe shukrani za pekee kwa Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara za Kisekta, Wakuu wa Mikoa ya Kanda hii ya Ziwa Mashariki kwa kazi kubwa ya maandalizi ya maonesho haya. Aidha, nichukue fursa hii kuwapongeza wadau wote wa Maonesho haya kwa kujitokeza kwa wingi na ubunifu wa kipekee katika Maonesho haya.
Natambua changamoto za ugonjwa wa Korona ilivyoathiri maandalizi ya maadhimisho kwa mwaka huu. Lakini hakika mmejitahidi sana ikizingatiwa muda mchache wa maandalizi tangu pale Taifa letu tulipojiridhisha kupungua kwa maambukizi ya COVID-19.
Kwa namna ya pekee napenda kutambua uwepo wa wananchi wote kutoka mikoa mbalimbali mliojitokeza kwa wingi wenu kutembelea mabanda ya Wakala, Taasisi za Umma na Sekta Binafsi wakiwemo Wajasiriamali waliojitolea kuunga mkono na kutambua juhudi hizi za Serikali. Waswahili husema shughuli ni watu na kwa kadamnasi hii ya watu ninayoiona mbele yangu basi sina shaka kusema kuwa shughuli yetu imefana.
Ndugu Wananchi, sote tunafahamu umuhimu wa maadhimisho haya ambayo hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuwatambua Wadau Wakuu wa Sekta ya Kilimo ambao ni Wakulima, Wafugaji, Wavuvi, Wanaushirika, Wasindikaji wa mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na maliasili kwa mchango wao mkubwa wanaoutoa katika kuendeleza uchumi wa nchi yetu.
Maonesho haya hutoa fursa kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wanaushirika kuona na kujifunza matumizi ya teknolojia bora za kilimo, ufugaji na uvuvi kwa ajili ya kuongeza tija na uzalishaji kwa uhakika wa chakula, kukidhi mahitaji ya viwanda na masoko ya ndani na nje ya nchi.
Ninayo taarifa kuwa pamoja na kuadhimishwa Kitaifa katika Kanda ya Ziwa Mashariki hapa Mkoani Simiyu, Maonesho haya yanafanyika pia Kikanda kwenye Kanda nyingine Saba (7) za maonesho ambazo ni Kanda ya Mashariki (Morogoro), Kanda ya Kaskazini (Arusha), Kanda ya Magharibi (Tabora), Kanda ya Kusini (Lindi), Kanda ya Kati (Dodoma), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya) na Kanda ya Ziwa Magharibi (Mwanza). Lengo la kuwa na mtawanyiko huo wa maonesho ni kuhakikisha kuwa wadau wengi wa sekta za kilimo wanapata fursa ya kujifunza teknolojia kulingana na ikolojia ya Kanda husika.
Ndugu Wananchi, nimepata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali na kujionea shughuli mbalimbali zinazohusiana na ujasiriamali, uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, ushirika, usindikaji wa mazao na utafiti wa kilimo na mifugo. Nimefurahishwa na kazi nzuri inayofanywa na Wizara za Kisekta na wadau mbali mbali (Taasisi za utafiti, mabenki na sekta binafsi). Natambua umuhimu wa ushiriki wenu kwenye maadhimisho haya kwa kuwa nyie ndio chachu ya kukuza kilimo chetu kwa kushirikiana na Serikali katika kutekeleza maeneo ya kipaumbele ya kuongeza uzalishaji na tija kwenye kilimo. Maeneo hayo ni
- Uimarishaji wa upatikanaji wa pembejeo za kilimo;
- Udhibiti wa visumbufu;
iii. Matumizi ya zana bora za kilimo na huduma za ugani;
- Ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji;
- Ujenzi wa miundombinu ya kuhifadhi mazao ya kilimo;
- Utafutaji wa masoko; na
vii. Kufanya utafiti wa kilimo na kuzalisha teknolojia.
Aidha, nimefarijika kuona muamko wa wananchi katika Kanda hii, pamoja na mabadiliko ya ubunifu ya maonesho ya mwaka huu ikiwemo uwepo wa vituo maalum vya kutoa habari na elimu kwa wazalishaji; maeneo/vyumba maalum vilivyotengwa kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vitendo kuhusu kilimo biashara, ufugaji, fursa za masoko, majadiliano baina ya wadau wa Sekta ya Umma na Binafsi.
Huu ni ubunifu mzuri na endeleeni kuukuza na kuundeleza. Ni imani yangu kuwa wananchi watajifunza na kupata elimu na teknolojia mbalimbali katika maonesho haya ya Nane Nane.
Nawapongeza sana washiriki wote.
Ndugu Wananchi, sote tunatambua kuwa Sekta ya kilimo imeendelea kuwa ni mhimili muhimu katika maendeleo ya uchumi wa taifa letu. Katika kipindi cha miaka mitano, Pato la Taifa linalotokana na kilimo, kwa kutumia bei za Mwaka 2015 limeongezeka kwa asilimia 17 kutoka Shilingi trilioni 25.2 Mwaka 2015 hadi Shilingi trilioni 29.5 Mwaka 2019.
Vilevile, sekta hiyo imeendelea kutoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 58 Mwaka 2018 na kuchangia asilimia 28.2 ya Pato la Taifa na hata kuchangia upatikanaji wa malighafi za viwanda kwa wastani wa asilimia 65. Aidha, kati ya mwaka 2015 hadi 2019 sekta ya kilimo imeendelea kukua kwa wastani wa asilimia 5.2. Ukuaji huu wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi unahitaji usimamizi madhubuti katika Nyanja za kiutaalam, kisera na kiutendaji.
Maadhimisho ya Nane Nane ya mwaka huu yanaadhimishwa na kaulimbiu inayosema, “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi Bora 2020.” Kaulimbiu hii inaendana na wakati huu tulionao tunapojipanga kuelekea katika Uchaguzi Mkuu, wa Rais, Wabunge na Madiwani mwezi Oktoba 2020. Kaulimbiu hii inatoa hamasa kwa wananchi kuchagua viongozi bora 2020 watakaokuwa chachu ya kuleta mapinduzi katika Sekta za Uzalishaji na kuinua uchumi na ustawi wa wakulima, wafugaji na wavuvi.
Ni dhahiri kuwa maendeleo katika sekta mbalimbali hayawezi kupatikana iwapo hatuna viongozi bora wenye kuweza kuweka na kusimamia sera na mipango madhubuti itakayohakikisha kuwa wakulima wanawekewa mazingira rafiki na wezeshi ya kufanya kilimo ikiwemo uhakika wa masoko kwa bidhaa zao.
Ni vyema kila mmoja wetu kwa nafasi yake kuhakikisha kuwa tunachagua viongozi ambao wataweka maslahi mapana ya taifa mbele na sio matumbo yao.
Ndugu Wananchi, nyote ni mashahidi wa kazi na hatua mbalimbali tulizochukua katika awamu ya tano ikiwa ni pamoja na kusimama bega kwa bega na wakulima katika mnyororo mzima wa uzalishaji na uongezaji thamani wa bidhaa za kilimo.
Kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya 2015-2020 tumetekeleza ahadi tulizozitoa kwa wakulima kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) na kuwezesha kilimo kuchangia katika uchumi na maendeleo ya Taifa letu, hususan katika maeneo ya:
- a)Usalama wa chakula na lishe,
- b)Ajira,
- c)Upatikanaji wa malighafi za viwanda
- d)Kuchangia katika kupunguza umaskini na kuongeza kipato cha wakulima.
Si lengo langu kudurusu hotuba za Waziri wa Kilimo na Mawaziri wenzie wa Ufugaji na Biashara walizozitoa wakati wa bajeti ya mwaka 2020/2021; ila niruhusuni nigusie kwa uchache baadhi ya maeneo yaliyopata mafanikio makubwa katika awamu ya tano ambayo ni:
- Usalama wa chakula na lishe; hivyo kupelekea nchi kujitosheleza kwa chakula kwa wastani wa asilimia 121 na kuwa na wastani wa ziada ya takribani tani milioni mbili;
- Ongezeko la uzalishaji wa mazao makuu ya biashara yakiwemo pamba, kahawa, chai, pareto, tumbaku, korosho, mkonge na miwa kutoka tani 796,502 mwaka 2015/2016 hadi tani 1,148,126 mwaka 2018/2019 sawa na ongezeko la asilimia 44.1. Aidha, kutokana na zao la korosho wakulima katika mkoa wa Lindi, Mtwara na Ruvuma hadi sasa wameshalipwa na Serikali zaidi ya shilingi bilioni 800.
- Upatikanaji wa pembejeo za kilimo; Tumeimarisha mfumo wa upatikanaji wa mbolea kwa kuanzishwa mfumo wa ununuzi wa pamoja (Bulk Procurement System-BPS) ambao umewezesha kuongeza upatikanaji wa mbolea kutoka tani 302,482 mwaka 2015/16 hadi tani 604,978 mwaka 2019/20. Vilevile tumefanya maboresho ya mifumo ya biashara ikiwemo ya usajili, uzalishaji na uagizaji wa pembejeo za uzalishaji wa mazao.
- Upatikanaji wa Mbegu bora umeongezeka kutoka tani 36,614.28 mwaka 2015/2016 hadi tani 76,725.52 mwaka 2019/2020 sawa na ongezeko la asilimia 110. Aidha, uzalishaji wa ndani wa mbegu bora umeongezeka kutoka tani 20,604.97 mwaka 2015/2016 hadi tani 69,173.17 mwaka 2019/2020. Uzalishaji huo umepunguza uagizaji wa mbegu kutoka nje ya nchi kutoka tani 2,216,009.31 mwaka 2015/2016 hadi tani 7,552.35 mwaka 2019/2020 sawa na punguzo la asilimia 53.
- Maboresho ya kisera ya kodi na tozo; Tumefuta ushuru, tozo na ada chechefu 105 kati ya mwaka 2015/2016 hadi 2019/2020 ambazo zimesaidia kumuondolea mkulima kero, adha, na kupunguza gharama za uzalishaji na kuchochea uzalishaji na uwekezaji katika Sekta ya kilimo.
- Upatikanaji wa Masoko; Tumeimairisha masoko ya mazao ya kilimo kupitia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani. Serikali imeimarisha mfumo wa stakabadhi za ghala kwa kuhakikisha mazao yanauzwa kwa mfumo huo kupitia vyama vya ushirika ili kuwapatia wakulima masoko ya uhakika na bei zenye tija.
- Kuanzishwa kwa Bima ya Mazao na Kanzidata za wakulima; mfumo wa usajili wa wakulima na uanzishwaji wa Bima ya Mazao umeanzishwa kwa lengo la kumsaidia mkulima kujikinga na athari za majanga ya asili na mabadiliko ya tabianchi. Hadi kufikia Julai, 2020 jumla ya wakulima 1,325,799 wamesajiliwa kupitia mfumo maalum wa kusajili wakulima (Farmers Registration System-FRS). Nitoe wito kwa wakulima na wasimamizi kuendelea na zoezi hili muhimu lenye lengo la kuwatambua wakulima wote nchini ili kuwa na takwimu sahihi kwa ajili ya maamuzi sahihi kwa sekta ya kilimo.
- Upatikanaji wa viuatilifu; umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza upotevu wa mazao wakati wa kuvuna na baada ya kuvuna; Wizara, kupitia TPRI imesajili viuatilifu vipya 66.
- Ongezeko la matumizi ya zana bora za kilimo; matrekta makubwa na matrekta ya mkono yanayomilikiwa na wakulima yameongezeka kutoka 14,200 na 6,348 mwaka 2015 hadi 19,604 na 8,883 mwaka 2019 hii imesaidia kuzalisha zaidi na kurahisisha kilimo.
- Ongezeko la viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo; viwanda 145 vya usindikaji wa mazao ya mifugo vimejengwa vikijumuisha viwanda 33 vya nyama, viwanda 99 vya maziwa na viwanda 13 vya kusindika ngozi. Katika kipindi cha miaka minne jumla ya viwanda vipya 199 vya kuchakata mazao vimeanzishwa vikiwemo vya kubangua korosho, viwanda vya chai, viwanda vikubwa na viwanda vidogo vya kuchakata mkonge, kusindika matunda na mboga mboga.
- Maboresho katika sekta ya Mifugo na Uvuvi; Yamehakikisha kusimamia mpango wa matumizi bora wa ardhi kwa kuhakikisha ufugaji na uvuvi endelevu na unaohimili mabadiliko ya Tabianchi. Maboresho haya yameongeza uzalishaji wenye tija. Kwa upande wa Sekta ya Mifugo ilichangia asilimia 7.4 katika mwaka 2019/2020, katika pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 7.2 mwaka 2018/2019. Pia, Sekta ya Mifugo imekua kwa asilimia 5 kwa mwaka 2019/2020 ikilinganishwa na asilimia 4.9 mwaka 2018/2019. Kwa upande wa Sekta ya Uvuvi ilichangia asilimia 1.71 katika pato la Taifa na imetoa ajira kwa Watanzania milioni 4.5. Vilevile, imechagia takriban asilimia 30 ya protini katika lishe inayotokana na wanyama.
- Utoaji wa mikopo; Serikali imeanzisha Dawati la Sekta binafsi linaloratibu wadau wa sekta ya mifugo na uvuvi wanaohitaji huduma za mikopo, dhamana na bima. Kutokana na uwepo wa dawati hilo, katika mwaka 2019/2020 TADB iliidhinisha jumla ya Shilingi bilioni 26.1 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wazalishaji wa mifugo na wasindikaji wa nyama, wazalishaji na wasindikaji wa maziwa na wavuvi na wakuzaji viumbe maji. Aidha, benki ya TPB imefungua dirisha maalum la mikopo kwa wavuvi, na Shirika la Bima la Taifa (NIC) limeanzisha huduma ya bima ya mifugo itakayochochea ongezeko la mikopo.
Mbali na hatua tajwa hapo juu, vilevile tumefanya maboresho kwenye utafiti, huduma za ugani na mafunzo; uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti Upotevu wa Mazao baada ya Mavuno, ongezeko la uzalishaji wa mazao ya bustani; kuimarika kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko; kuimarika kwa ushirika; kuimarika kwa kilimo cha umwagiliaji; ongezeko la ushiriki wa vijana katika kilimo; matumizi bora ya ardhi; kuhuisha mifumo na sera za kilimo.
Ndugu Wananchi, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi bado inakabiliwa na changamoto zifuatazo:-
- Upungufu wa masoko ya uhakika kwa mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kuyumba kwa bei za mazao.
- Mabadiliko ya tabianchi yamechangia kuwepo kwa mlipuko wa magonjwa ya mimea na mifugo na hivyo kuchangia uzalishaji kuwa mdogo.
- Upungufu wa wataalamu katika Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
- Upungufu wa vitendea kazi kwa Maafisa Ugani hasa katika ngazi za chini kama vile usafiri, kompyuta.
- Baadhi ya viongozi wa Vyama vya Ushirika kutokuwa waadilifu na hivyo kupelekea ufanisi mdogo katika Sekta ya Ushirika.
- Matumizi duni ya pembejeo na zana kwenye Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Ndugu Wananchi, katika kutatua changamoto hizi Serikali kwa kushirikiana na Sekta binafsi imejipanga kutekeleza mambo yafuatayo:-
- Kuendelea kuimarisha mifumo ya masoko kwa kuhakikisha inajenga miundombinu wezeshi na kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya upatikanaji wa masoko ya uhakika ya mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ndani na nje ya nchi.
- Kuwajengea uwezo wananchi kuhusiana na namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kuhimiza matumizi ya zana za kilimo hifadhi ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
- Kuendelea kuajiri na kuwapatia vitendea kazi wataalamu kulingana na bajeti ya kila mwaka na kuwatambua watoa huduma binafsi za ugani.
- Kuhamasisha uanzishaji wa vituo vya kutoa huduma za zana za Kilimo (Agri-Mechanization hub) pamoja na uwezeshaji wa utengenezaji wa boti za uvuvi za kisasa kwa gharama nafuu. Kupitia utaratibu huu wakulima, wafugaji na wavuvi watapata huduma kwa ukaribu zaidi na hivyo kuongeza matumizi ya zana za Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
- Kuhamasisha wananchi kuchagua viongozi waadilifu na pia Serikali inaendelea kuwachukulia hatua viongozi wala rushwa, wabadhirifu na wasiozingatia maadili ya kazi. Hivyo kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu nawahimiza kuchagua viongozi waadilifu na waliotayari kuwatumikia wananchi bila kuzingatia maslahi yao binafsi.
Ndugu Wananchi, napenda kutoa maelekezo ya kuzingatiwa wakati tunatekeleza shughuli za kilimo, mifugo na uvuvi kwa ajili ya kuwa na kilimo endelevu kinacholinda mazingira yetu kama ifuatavyo: –
- Matokeo ya Tafiti
Watafiti wetu wanafanya kazi nzuri sana na kupata mbegu bora zinazokinzana na magonjwa pamoja na mbegu zinazohimili mabadiliko ya tabianchi. Hata hivyo, matokeo ya tafiti hizo zilizo nyingi haziwafikii walengwa. Nitoe rai kwa watafiti wote nchini kutoa matokeo ya tafiti zenu kwa Maafisa Ugani na wadau wengine ili wakulima wetu wanufaike na matokeo hayo.
- Kilimo cha umwagiliaji
Kilimo cha umwagiliaji ni muhimu sana na kinakabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi. Kilimo hiki huwezesha eneo husika kulimwa mara mbili au zaidi kwa mwaka. Hivi sasa eneo la umwagiliaji linalotumika linakadiriwa kuwa Hekta 475,052 tu, hii ni kutokana na gharama kubwa inayohitajika katika ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji. Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi itahakikisha kuwa miundombinu ya umwagiliaji inajengwa na kusimamiwa vizuri. Aidha, naiagiza Wizara ya Kilimo ambayo ndiyo inayoisimamia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kutumia fursa hii kutoa elimu ya utunzaji na uendeshaji endelevu wa miundombinu ya umwagiliaji. (Nisisitize kuwa tuwaze Unyunyiziaji badala ya umwagiliaji).
- Mifugo
Kadri mifugo inavyoongezeka inahitaji eneo kubwa la malisho na maji ya kutosha. Kwa bahati mbaya sana, ardhi haiongezeki. Hali hii, kwa namna moja ama nyingine inaibua migogoro kati ya wakulima na wafugaji kutokana na ardhi kutokidhi mahitaji ya pande zote mbili, wakulima na wafugaji. Kupitia maonesho haya, Serikali inawaelekeza wataalam wa mifugo kutumia vizuri nafasi hii, kutoa elimu bora ya utunzaji wa mifugo pamoja na malisho kulingana na hali halisi ya maeneo tuliyonayo. Ni vyema mkatoa elimu ya jinsi wafugaji wetu wanavyoweza kufanya ufugaji endelevu kwa kuvuna mifugo yao na kujiongezea kipato.
- Uvuvi
Vitendo vya baadhi ya wavuvi wanaovua samaki bila kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, vilipelekea kupungua kwa samaki katika Maziwa yetu, wote ni mashahidi jinsi tulivyokuwa na upungufu wa mavuno ya samaki kutoka Ziwa Viktoria. Serikali imeboresha Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009 ambayo imeelekeza zana za kutumia na aina ya uvuvi ili kujenga uvuvi endelevu. Wizara ya Uvuvi muendelee kusimamia na kudhibiti Uvuvi haramu kulingana na Sheria na taratibu zilizopo.
- Upandaji wa miti
Bado wananchi wanafanya vitendo viovu vya ukataji miti kiholela hususan kwenye maeneo ya hifadhi. Wizara yenye dhamana ya misitu na hifadhi isimamie na kuwakuchukulia hatua wote wanaoendelea na kilimo kwenye hifadhi za misitu. Agizo la kupanda miti 1.5m kwa kila Wilaya ni agizo halali lililoelekezwa na Ilani yetu ya CCM ya mwaka 2015 katika Ibara 193 (a), hivyo nikumbushe kila Mkoa, Wilaya na Halmashauri zetu kutekeleza agizo la kupanda miti na kuhakikisha inamea.
- Kutunza vyanzo vya maji kwa kutofanya shughuli za kibinadamu katika maeneo yanayozunguka vyanzo vya maji.
Ndugu Wananchi, Serikali imeandaa utaratibu kwenye viwanja hivi vya Nyakabindi wa kuwakutanisha wafanyabiashara, wamiliki wa viwanda na wakulima ili kujadili changamoto na mafanikio katika shughuli zao. Natoa wito kwa wananchi wote mnaoshiriki kwenye maonesho kushiriki kwenye majadiliano hayo.
Aidha, kila Wizara na Taasisi za Umma na Binafsi ziwe mstari wa mbele kutafuta na kuwakutanisha wadau wa sekta husika na kujadili ufumbuzi wa changamoto zilizopo katika sekta husika. Suala la masoko, mifumo ya upatikanaji mitaji, maeneo ya uwekezaji, miundombinu ya usafirishaji, uchukuzi na uhifadhi viwe mojawapo ya maeneo ya kipaumbele katika majadiliano yenu. Suala hili lifanyike katika viwanja vya maonesho kote nchini na wananchi jitokezeni kwa wingi kutumia fursa hii. Vitengo na Idara za mawasiliano zihusike katika kuhabarisha umma maonesho na elimu inayotolewa katika viwanja hivi ili wadau wengi waweze kufikiwa.
Ndugu Wananchi, kabla sijahitimisha hotuba yangu napenda kuzungumzia kidogo kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika tarehe 28 Oktoba, 2020. Nawasihi wananchi mjitokeze kwa wingi kwenye mikutano ya kampeni kuwasikiliza wagombea na sera zao ili ziwasaidie kufanya maamuzi sahihi siku ya kupiga kura.
Nayasema haya kwa kuzingatia kuwa Maonesho ya Kilimo Nane Nane mwaka huu kaulimbiu yake imelenga kuwakumbusha wakulima, wafugaji na wavuvi kote nchini kuchagua Viongozi Bora. Serikali yenu imeweka mazingira wezeshi kwa wagombea wote kufanya shughuli za siasa kwa amani na utulivu.
Niwaombe viongozi wote wa vyama vya siasa kufanya kampeni zenu kwa kuzingatia taratibu zinazotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Serikali haitosita kuchukua hatua kali za kisheria kwa wote watakaoendesha kampeni zinazolenga kujenga chuki na kuvuruga amani iliyopo. Napenda kuwasihi wananchi wote kufika kwenye viwanja vya maonesho ya Nane Nane kote nchini kwa lengo la kujifunza kanuni bora za uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Baada ya kusema haya, nitamke rasmi kuwa Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane mwaka 2020 yamefunguliwa rasmi.
Mungu Ibariki Tanzania;
Mungu Wabariki Wakulima,
Wafugaji na Wavuvi