Home Mchanganyiko Jamii yahimizwa kumsaidia majukumu ya kazi mama anayenyonyesha kuepusha utapiamlo kwa watoto

Jamii yahimizwa kumsaidia majukumu ya kazi mama anayenyonyesha kuepusha utapiamlo kwa watoto

0

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiongea na wananchi wa wilaya ya Muheza wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji yaliyofanyika kitaifa kwenye viwanja vya jitegemee Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akiingia kwenye viwanja vya jitegemee,kulia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na Lishe(TFNC)Dkt.Germana Lyna na kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe kutoka wizara ya afya Grace Moshi Waziri Ummy Mwalimu akizindua kitita kwa ajili ya vyombo vya habari,kushoto ni Mkuu wa Wilaya Injinia Mwanaasha TumboMwakilishi wa waandishi wa habari kutoka Tanga akipokea kitita cha lishe ya wanawake,watoto na vijana balehe kwa ajili ya,vyombo vya habari kilichozinduliwa kwenye ufunguzi wa maadhimisho hayo.Wakazi wa Muheza waliofika kwenye ufunguzi wa maadhimisho hayo.

****************************************

Na.Catherine Sungura,WAMJW-Muheza

ULISHAJI usio sahihi unaochangiwa na mama kuelemewa na majukumu mengi ya kazi na hivyo kukosa muda wa kutosha wa kumtunza mtoto ni sababu kubwa ya utapiamlo kwa watoto

Hayo yamesema leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji ambayo kitaifa yamefanyika wilayani hapa.

“Ni dhahiri kuwa mchango wa mwanamke katika familia, ajira na uzalishaji kwa ujumla ni mkubwa hivyo ni muhimu kuwatia moyo na kuwasaidia wanawake ili waweze kufanya majukumu ya uzalishaji na utunzaji familia kwa ukamilifu”.

Waziri Ummy amesema kuwa jamii ina wajibu wa kuwawezesha wazazi, hususani wanawake waweze kunyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo baada ya kujifungua.

Aidha, amesema watoto wanapotimiza miezi sita waanzishiwe vyakula vya nyongeza vyenye ubora kilishe huku wakiendelea kunyonyeshwa hadi watakapotimiza umri wa miaka miwili.

Kwa upande wa takwimu za hali ya ulishaji watoto nchini Tanzania zinaonesha kuwa takribani asilimia 97 ya watoto wenye umri chini ya miaka miwili wananyonyeshwa maziwa ya mama.

“Idadi ya watoto wanaoanzishiwa kunyonyeshwa maziwa ya mama kwa wakati sahihi katika kipindi kisichozidi saa moja baada ya kuzaliwa ni asilimia 53 na idadi ya watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila kupewa maji, vinywaji na vyakula vingine katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo baada ya kuzaliwa ni asilimia 58,”
amesema Waziri Ummy.

Amesma Idadi ya watoto wanaoanzishiwa vyakula vya nyongeza kwa wakati sahihi katika umri wa miezi 6 hadi 8 ni asilimia 87 na idadi ya watoto wenye umri wa miezi 6 – 23 wanaolishwa chakula kinachokidhi vigezo vya ubora kilishe ni asilimia 35.

“Vigezo hivyo ni idadi sahihi ya milo anayopewa mtoto kwa siku kulingana na umri wake, na mlo uwe na mchanganyiko wa vyakula kutoka kwenye makundi yasiyopungua manne ya vyakula,” amesisitiza.

Amesema Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani kwa mwaka 2020 yamebebwa na kauli mbiu inayosema “Tuwawezeshe wanawake kunyonyesha watoto kwa afya bora na ulinzi wa mazingira”.

Amesema kauli mbiu hii inalenga kutukumbusha mchango wa unyonyeshaji katika utunzaji wa mazingira ya dunia na ikolojia yake sanjari na kulinda afya ya binamu.

Amesema kauli mbiu hii inahimiza jamii kuboresha kasi ya unyonyeshaji sanjari na kupunguza kiwango cha matumizi ya maziwa na vyakula mbadala vya watoto wachanga na wadogo.

“Aidha tukumbuke kuwa matumizi ya maziwa na vyakula mbadala vya watoto wachanga na wadogo yanakwenda sanjari na matumizi ya vifungashio mbalimbali vikiwemo vya plastiki, nishati ikiwemo kuni na mkaa, maji, chupa za kulishia watoto na ongezeko la hewa ya ukaa inayoathiri mazingira ya dunia,” amesema Waziri Ummy.