Sheikhe Bushira Ally akitoa Khutuba ya Eid-Al-Adhah katika viwanja vya msikiti Kibeta baada ya waumini kutekeleza swala ya hiyo leo julai 31, mwaka huu.
Waumini wa kike walihudhuria na kutekeleza ibaada ya swala ya Eid-Al-Adhah katika viwanja nvya nsikiti kibeta manispaa ya Bukoba leo julai 31,mwaka huu.
Waumini wa dini ya kiislamu walitekeleza ibaada ya swala ya Eid-Al-Adhah wakimsikiliza sheikhe Bushira Ally wakati akitoa Khutuba ya swala ya hiyo leo Jualai 31,mwaka huu.
Picha zote na Allawi Kaboyo.
**********************************
Na Allawi Kaboyo Bukoba.
Waumini wa dini ya kiislamu mkoani Kagera wameungana waislamu wengine nchini pamoja na ulimwengu mzima kufanya ibaada ya swala ya Eid-al-adhah ibaada ambayo hufanyika kila mwaka mara moja kutokana na miandamo ya miezi ikiambatana na suala la uchinjaji.
Akitoa khotuba ya swala ya Eid katika viwanja vya msikiti wa kibeta uliopo manispaa ya Bukoba julai 31, mwaka huu Sheikh Bushira Ally amesema kuwa swala hiyo hufanyika baada ya siku kumi tangu kuandama kwa mwezi wa Dhul-Hijja kwa mujibu wa kalenda ya kiislamu ambapo tarehe 9 katika mwezi huo ni siku ya Arafa ambayo hiyo ni siku bora kuliko siku zote kwa waislamu.
Amesema kuwa siku ya Arafa waislamu wanatakiwa kuitumia kumuomba mungu kwa yale ambayo wanamahitaji nayo na kuomba msamaha kwaajili ya madhambi waliyokwisha kuyafanya, ambapo amesema kuwa katika mwezi huu waislamu duniani hufanya ibaada ya hijja katika nchi ya Saudi Arabia licha ya kuwa ibaada hiyo mwaka huu kwa mataifa ya nje ya nchi hiyo hayakuitekeleza kutokana na janga la Corona.
Ally amesema kuwa waislamu wanatakiwa kujikaribisha kwa mola wao kwa unyenyekevu mkubwa ili kuweza kusamehewa madhambi yao ambapo amewakumbusha mambo muhimu wanayotakiwa kuyafanya katika siku ya leo ikiwemo kuchinja wanyama wenye afya na wa halali ili kuenzi mitume waliotangulia.
“leo tunaswali Eid niwaombe ndugu zangu waislamu tutumie siku hii kumcha mola wetu, tuitumie siku hii kumuomba msamaha mola wetu na atusamehe madhambi yetu, tumeswali lakini vipo vitu ambavyo tunatakiwa kuvifanya baada ya swala kama kuchinja na waislamu tambueni wanyama wanaotakiwa kuchinjwa wanatakiwa wasiwe na sifa nne.” Amesema Sheikh Ally.
Amesema kuwa mnyama anayetakiwa kuchinjwa anatakiwa kwanza asiwe chongo, asiwe mlemavu wa miguu, asiwe amekonda na wala asiwe wa dhuluma ambapo amesema kuwa watu wanatakiwa kuchinja kwa siku hizi tatu mfululizo kuanzia leo na wale wasiokuwa na uwezo wakunua vichinjo wanaweza kuungana na kumnunua mnyama wa kumchinja.
Sambamba na hayo katika khutuba yake amewasihi waislamu kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi oktoba mwaka huu ukitanguliwa na kampeni kutojihusisha na vitendo vya uvunjifu wa Amani na kuitumia misikiti kama vijiwe vya kufanyia siasa badala ya kufanya ibaada ambapo pia amewasihi kutowaunga mkono wanasiasa watakaofanya siasa za uchonganishi zikiashiria uvunjifu wa amani.
Sheikhe Abdulshahidu Abbas ni imaamu mkuu katika msikiti huo ambaye pia ni amiri wa taasisi ya Jamaat Answar Sunna kanda ya ziwa amesema kuwa waislamu katika mataifa mengi wameshindwa kutekeleeza ibaada ya Hijja ikiwa ni nguzo ya tano na muhimu katika nguzo za dini ya kiislamu kutokana na janga la ugonjwa wa Corona.
Ameeleza kuwa uwepo wa gonjwa hili la Covid-19 unaosababishwa na virusi vya Corona umekuwa ni mwiba mkubwa kwa waislamu ambao walipanga kuitekeleza ibaada hiyo mwaka huu ambapo amesema kuwa haijawahi kutokea ibaada hiyo kutotekelezwa kwenye ulimwengu huu.
“Leo Mahujaji walitakiwa kuwa kwenye viwanja vitakatifu vya miji ya Makka na Madina wakiwa kwenye ibaada lakini kwa kadari ya Mwenyezimungu hatukuifanya hili liwe funzo kwa waislamu wale wenye uwezo kufanya ibaada hii pale wanapojaaliwa, tukumbuke walioikosa ibaada hii hawataipata tena hadi mwakani na wengine wanaweza wasifike mwakani na kuwapelekea kushindwa kuitekeleza ibaada hiyo katika maisha yao.” Ameeleza Sheikhe Shahidu.
Hata hivyo baadhi ya waumini waliotekeleza ibaada ya swala ya Eid wamemshukuru mungu kwa kuwawezesha kuifikia ibaada hiyo maana sio kwa ujanja wao bali ni kwa matakwa yake muumba wa mbingu na Ardhi pamoja na vilivyomo.