Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin William Mkapa, nyumbani kwa marehemu , Masaki jijini Dar es salaam, Julai 24, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpa pole Mama Anna Mkapa, Mjane wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin William Mkapa, nyumbani kwa marehemu, Masaki jijini Dar es salaam, Julai 24, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, nyumbani kwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, marehemu Benjamin William Mkapa ambako walikwenda kutoa pole kwa familia, Julai 24, 2020. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Abubakar Kunenge na wa tatu kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Godfrey Chongolo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
**********************************
*Yawasihi wanafamilia na Watanzania waendelee kuwa watulivu
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa kilichotokea jijini Dar es Salaam na ametoa pole kwa familia kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Serikali.
“Ndugu wanafamilia, kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali tumepokea taarifa za msiba wa mzee wetu, kiongozi wetu Rais wa Awamu ya Tatu kwa masikitiko makubwa. Nawasihi muendelee kuwa watulivu na wavumilivu katika kipindi hiki kigumu kama alivyosema Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Magufuli.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Julai 24, 2020) nyumbani kwa marehemu Masaki, jijini Dar es Salaam. Amewasihi wanafamilia na Watanzania kwa ujumla waendelee kumuombea marehemu kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu yote ni mapenzi yake.
Amesema kamati ya mazishi ya Serikali inaendelea na maandalizi pamoja na kuwasiliana na viongozi kutoka katika nchi marafiki ambao marehemu alifanya nao kazi ili kutoa fursa ya wao kushiriki. “Tutatoa taarifa ya ratiba ya kuaga mwili itakayofanyika Uwanja wa Taifa.”
Kufuatia kifo hicho kilichotokea usiku wa kuamkia leo, Rais Dkt. Magufuli ametangaza siku saba za maombolezo ya Kitaifa kuanzia leo Ijumaa, Julai 24, 2020 na katika kipindi chote cha maombolezo bendera zote zitapepea nusu mlingoti.
Akitangaza kifo hicho kwa Watanzania kupitia vyombo vya habari usiku wa kuamkia leo Rais Dkt. Magufuli kwa masikitiko makubwa alisema Rais wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamini William Mkapa amefariki dunia hospitalini jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akipatiwa matibabu.
Rais Dkt. Magufuli amewataka Watanzania wote wawe watulivu na wastahimilivu baada ya kupokea taarifa za kuondokewa na mpendwa wao Mhe. Benjamin William Mkapa. “Kwa masikitiko makubwa tumepata msiba mkubwa, Mzee wetu Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu amefariki dunia.”
Aliongeza kuwa “ Amefariki dunia katika hospitali jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa, niwaombe Watanzania tulipokee hili, tumepata msiba mkubwa na tuendelee kumuombea Mzee wetu Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa, ambaye ametangulia mbele za haki.”