Picha ya Kaimu Mkuu wa chuo,Profesa Epaphra Manamba akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake wakati akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa zilizozushwa mitandaoni kuhusu wanafunzi wa chuo hicho kuandamana.
Rais wa serikali ya wanafunzi wa chuo Cha uhasibu Arusha IAA ,Michael Munishi akitoa ufafanuzi juu ya kuwepo kwa taarifa hizo za uzushi kuhusu kuandamana kwa wanafunzi chuoni hapo.
…………………………………………..
Happy Lazaro, Arusha
Chuo cha Uhasibu cha Arusha,IAA kimetoa ufafanuzi juu ya taarifa zilizo sambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba wanafunzi wa chuo hicho wameandamana julai 22 mwaka huu, wakidai fedha za mikopo kutoka bodi ya Mikopo na kudai kwamba taarifa hizo hazina ukweli wowote ni za kupuuzwa.
Akiongea na vyombo vya habari chuoni hapo ,Kaimu Mkuu wa chuo hicho,Prof.Epaphra Manamba alidai kwamba wanafunzi 801 kati ya 4,700 wa chuo hicho ambao ni wanufaika wa bodi ya mkopo ya elimu ya juu walifanya kikao na mdhamini wao majira ya jioni kwa lengo la kupata ufafanuzi juu ya mkopo uliotumwa kwao kabla ya serikali kufunga vyuo kutokana na janga la( Covid 19 )mwezi Machi 2020 na pesa iliyotumwa baada ya vyuo kufunguliwa .
Aidha alisema kuwa ,kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na mkuu wa wilaya ya Arusha ,Kenan Kihongosi ambapo yaliyojiri kwenye kikao hicho ni kuwa wanafunzi walipokea pesa ya miezi miwili toka bodi ya mikopo na fedha hiyo ilitumika kwa siku tisa tu kabla ya serikali haijafunga vyuo kwa ajili ya janga la korona Machi 18,mwaka huu.
Hata hivyo baada ya kufunguliwa chuo June 1,mwaka huu bodi ya mikopo kwa kutumia ratiba ya chuo iliongeza pesa ya siku ishirini wakihesabu zile hamsini na Moja ambazo wanafunzi walipewa awali.
“Sasa mategemeo ya wanafunzi yalikuwa ni kupokea pesa ya siku sitini(60) na sio ishirini(20) kwa sababu chuo walikuwa wakiendelea na masomo kwa njia ya mtandao kipindi chote ambacho vyuo vilikuwa vimefungwa”alisema Profesa.
Aliongeza kuwa,ufafanuzi wa bodi ya mikopo kuhusu hela inayotolewa kwa wanafunzi ni kwa ajili ya chakula na malazi ambapo haitolewi wakiwa nyumbani na sio kwa matumizi mengine.
Profesa Manamba aliongeza kuwa,baada ya majadiliano ya pamoja Kati ya bodi ya mikopo,chuo,wanachuo na ofisi ya Mkuu wa wilaya walikubaliana chuo kuwaandikia barua bodi ya mikopo ya elimu ya juu kuwaeleza jinsi ambavyo chuo kiliendelea na masomo kwa njia ya mtandao hivyo,kuwaomba iwaangalie na kuwafikiria wanachuo .
Ambapo waliomba pia kuongeza siku sita baada ya ratiba ya mitihani kubadilika kutoka agosti 7 mwaka huu na kuwa agosti 13 mwaka huu.
Aidha makubaliano mengine yalikuwa ,kutokana na wanafunzi wengine kutumia kiasi cha pesa kutoka bodi ya mikopo ya elimu ya juu kuongeza katika ada wanaodaiwa,chuo kimeruhusu wanafunzi wanufaika wa bodi ya mkopo kufanya mitihani hata Kama hawajakamilisha Ada wakati wakiendelea kutafuta hela.
“Jamani tunaomba Sana watu na kuwaasa kuepuka kutoa taarifa ambazo zinazua taharuki na kupotosha jamii badala yake watu wajikite katika taarifa zinazoelimisha na sio kuzusha vitu ambavyo hawana uhakika navyo.”alisema Profesa Manamba.
Kwa upande wake Rais wa serikali ya wanafunzi,Michael Munishi( IAA)alisema kuwa, wanafunzi hao hawana mgogoro wowote na chuo na kwamba taarifa kwamba walifanya maandamano hazina ukweli wowote na zimelenga kuwachonganisha wanafunzi na chuo chao.