………………………………………………………………………
Na.Majid Abdulkarim, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, amewataka viongozi wapya waliyoapishwa leo kuimarisha ushirikiano mzuri na watendaji waliopo katika maeneo yao ya kazi ili kuongeza ufanisi mzuri katika utendaji kazi wa kuleta maendeleo ya kujenga nchi.
Wito huo ameutoa leo Ikulu ya Jijini Dodoma wakati wa kuwaapisha viongozi wapya waliyoteuliwa hivi karibuni.
Aidha Rais Magufuli, amesema kuwa ufanisi mzuri wa watendaji hao katika nafasi zao ndio itakuwa chachu ya kuendelea kuinua uchumi wa kati kutoka hapo ulipo na kukua zaidi.
“Nendeini mkachape kazi ya kuwatumikia watanzania kwa kumtanguliza Mungu ili kuweza kufanikiwa katika kutekeleza majukumu yenu”, amesisitiza Rais Magufuli.
Lakini katika hatua nyingine Rais, Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM) amesema kuwa mpaka sasa katika nafasi ya ubunge jumla ya waliyojitokeza kutia nia ya kuomba kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu mwezi Oktoba,Mwaka huu ni 10,367.
“Mnaosimamia uchaguzi Mkuu ninatamani kuona kura za wagombea wote zinahesabiwa hadharani mbele ya wajumbe ili kila mmoja ajue alichopata nah ii ndio Demokrasia tunayoitaka”, ametoa rai Rais Magufuli.
Naye Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu amewataka wateule hao kuleta mabadiliko ya maendeleo katika utendaji wao kwa kuanzia pale walipoishia waliyokuwepo awali.
“Paukwa Pakawa, lengo ni kuendeleza kuleta maendeleo na hivyo ndo dhumuni kubwa la mabadiliko hivyo karibuni katika mchakamchaka wa kuleta maendeleo”, amesema Mhe. Samia.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge amewakumbusha viongozi hao wateule kuwa ajenda kubwa katika kumsaidia Rais ni kutimiza ndoto kubwa ya kuwaletea maendeleo watanzania.