Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji (mwenye shati la maua) akimsikiliza Meneja Ufundi IRUWASA, Mhandisi Fabian Maganga akielezea ramani ya mtandao wa maji mradi wa Ismani-Kilolo wakati wa ziara yake kwenye mradi
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji (wa pili kushoto) akimsikiliza Meneja Ufundi wa IRUWASA, Mhandisi Fabian Maganga (kulia) akielezea ujenzi wa chujio la kusafisha maji kwenye eneo la Ndiuka kwa ajili ya wananchi wa Iringa Mjini na maeneo mengine ikiwemo Ismani.
………………………………………………………..
NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ametoa Wiki Sita kwa Mamlaka ya Maji Iringa (IRUWASA) na Wakala ya Maji Vijijini (RUWASA) kuhakikisha wananchi wa eneo la Ismani Tarafani Wilayani Iringa wanapata huduma ya maji kupitia mfumo wa maji wa IRUWASA uliofika eneo la kijiji cha Kising’a.
Mhandisi Sanga ametoa maelekezo hayo Julai 16, 2020 wakati wa ziara yake Mkoani Iringa ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji inayotekelezwa mkoani humo kwa lengo la kujionea hatua iliyofikiwa sambamba na kuzungumza na watekelezaji wa miradi husika.
Akiwa katika eneo hilo la Ismani katika ziara yake kwenye mradi wa maji wa Ismani-Kilolo, Mhandisi Sanga hakukubaliana na taarifa ya wataalam wanaotekeleza mradi huo iliyobainisha kwamba wananchi wataanza kunufaika na huduma ya maji ifikapo Juni, 2021 baada ya mradi kukamilika ikiwemo kukamilika kwa ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji.
“Sikubaliani na mapendekezo yenu kwamba wananchi waanze kupata maji hapo mwakani baada ya mradi mzima kukamilika, nimejionea hali ya maji hapa Ismani Tarafani sio nzuri, hatuwezi kuendelea kusubiri hadi tenki la maji likamilike ndipo wananchi waanze kupata huduma wakati tunao uwezo kwa kutumia utaalamu wetu kuhakikisha wanapata huduma kabla ya hilo tenki kukamilika,” alisema Mhandisi Sanga.
Mhandisi Sanga alibainisha kwamba maelekezo ya Wizara ya Maji ni kwamba miradi yote inayopeleka huduma ya maji kwa wananchi ikamilike haraka kwani Serikali haipo tayari kuona wananchi wakitaabika kwa kukosa huduma ya maji hasa ikizingatiwa kwamba fedha ya utekelezaji wa miradi hiyo ilikwishatengwa.
“Maelekezo yangu ambayo ni maelekezo ya Waziri wa Maji ni kwamba miradi yote inayopelekea huduma kwa wananchi ijengwe kwa haraka. Hatuna sababu ya kuwacheleweshea huduma wananchi; Serikali ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli haiwezi kuvumilia kuona wananchi wakiteseka kwa kukosa huduma ya maji,” alisisitiza Mhandisi Sanga.
Mhandisi Sanga alielekeza ifikapo tarehe 20 Julai 2020 wataalam wa RUWASA na IRUWASA wawe wameanza utekelezaji wa maelekezo ya kuhakikisha wananchi wa Ismani Tarafani wanapata huduma haraka kwani fedha zipo tayari na kwamba kiasi cha Shilingi Milioni 200 kitapelekwa Mkoani humo kwa ajili ya mradi husika kabla ya tarehe hiyo.
“Gharama za kufikisha maji hapa Ismani Tarafani ni kiasi cha Shilingi Milioni 600, ninawahakikishia kwamba ifikapo tarehe 20 Julai mtakuwa tayari mmepokea kiasi cha Shilingi Milioni 200 na ninawapa siku mbili hizi kuhakikisha mnajipanga kwa kuanza kutekeleza ikiwa ni pamoja na kutafuta vijana wa kuchimba mtaro wa kulaza mabomba,” alielekeza Mhandisi Sanga.
Aidha, alisisitiza kwamba shughuli ya uchimbaji mitaro ifanywe na wananchi wa maeneo hayo ikiwa ni njia mojawapo ya kuwaongezea kipato na kwamba taratibu za ununuzi wa mabomba zianze mara moja.
Kwa upande wake Meneja Ufundi wa IRUWASA, Mhandisi Fabian Maganga alipokea maelekezo ya Naibu Katibu Mkuu na aliahidi Isiman Tarafani kufikishiwa huduma haraka kama ilivyoagizwa.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi mzima wa Ismani–Kilolo alisema shughuli ya ujenzi wake zilianza rasmi Aprili 15, 2020 na kwamba tayari Wizara ya Maji imekwishatoa kiasi cha Shilingi Milioni 450.
Mhandisi Maganga alisema mradi unajengwa kwa mfumo wa ‘force account’ yaani kwa kutumia uwezo wa ndani na mafundi wa ndani ambao alisema ni kutoka IRUWASA kwa kushirikiana na RUWASA.
Alibainisha kuwa kukamilika kwa mradi mzima kutagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 9.27 na kutawezesha zaidi ya wananchi 58,821 kutoka vijiji 29 yaani vijiji 5 vya Kilolo na vijiji 24 vya Ismani kunufaika na hivyo kuondokana na changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama.
Alisema mradi utatumia chanzo cha maji cha Mto Ruaha Mdogo chenye maji ya kutosha na maji ya chanzo cha kijito cha Mgela yatakuwa yanatumika kwa dharura endapo itabidi kufanya hivyo.
“Kwa usanifu tuliofanya, uzalishaji wa maji kutoka vyanzo hivyo utakidhi mahitaji ya mradi hadi Mwaka 2038 na hapatakuwa na sababu ya kuchimba visima,” alibainisha Mhandisi Maganga.
Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Anthony Sanga yupo kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji kwenye Mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya kwa lengo la kujionea hali halisi ya utekelezwaji wake kwenye mikoa hiyo.