Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro akiongea na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Dorothy Gwajima, alipomtembelea ofisini kwake wakati wa Ziara yakukagua Miradi ya Afya.
Naibu Katibu Mkuu pamoja na Mganga Mkuu wa Halmashuri ya Mlimba, wakifurahia kwa pamoja ubunifu wa Vyuma vya Kufungia Vyandarua katika Chuma cha Mama na mtoto katika kituo cha Afya Mlimba
Naibu Katibu Mkuu akizungumza na watumishi wa kituo cha Afya Mlali wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za Afya mkoani humo
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Dorothy Gwajima, alipofika ofisini kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo wakati wa ziara yake, hapa wakifurahia jambo sambamba na Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Kusiry Ukio.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya Afya Dkt. Dorothy Gwajima, akiongea na kutoa maelekezo kadhaa kwa watumishi wa wakituo cha Afya Sabasaba kilichopo Manispaa ya Morogoro
Baadhi wa Watendaji wa Kamati za Afya za Hamashauri ya Manispaa ya Morogoro, wakimsikiliza kwa kina Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Dorothy Gwajima hayupo pichani wakati wa maelekezo ya pamoja katika Ukumbi wa Hospitali ya Mkoa
…………………………………………………………………
Na Atley Kuni-MOROGORO
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afya Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Dorothy Gwajima, kwa kushirikiana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kusiry Ukio, wameendesha zoezi la kutathimini sifa na uwezo wa kazi miongoni mwa wajumbe wa Timu za Afya za Halmashauri za Mkoa huo kwa lengo la kubaini jinsi gani kila mjumbe wa timu hizo anaweza kuonesha umahiri katika kusimamia majukumu yake ya ajira na uongozi katika kuleta mabadiliko chanya ya haraka na kukabiliana na changamoto zilizopo kwa wakati.
Katika tathmini hiyo imebainika wapo baadhi ya wajumbe wa timu za afya Halmashauri (CHMT) ambao wanazo sifa za kielimu na uzoefu lakini hawatekelezi ipasavyo majukumu yao ya ajira, uongozi wala yale waliyoelekezwa na wizara kwa nyakati tofauti. Aidha, baadhi ya wajumbe wamezungukwa na changamoto za kawaida huku wakiwa hawana mwelekeo wowote stahiki wa kukabiliana nazo licha ya kupata mafunzo mbalimbali, ambapo huchangiwa na kutotumia muda wa kutosha katika kutafsiri na kushirikiana na wajumbe wa timu hizo.
“Haiwezekani wajumbe wa timu za afya Halmashauri mpo halafu tunakuta hakuna usimamizi, ufuatiliaji wala utekelezaji wa tuliyokubaliana na baadhi yenu hamna kabisa mpango kazi mnasimamia nini kwa kila jukumu wala hakuna tafakari wala tafsiri ya nini kinatarajiwa katika kila jukumu yaani mnafanya kwa mazoea bila mfumo wala utaratibu” amesema Dkt. Gwajima
Dkt Gwajima amesema, umefika wakati wa Wizara kuimarisha tathmini kwa kila mjumbe jinsi gani amesimama kwenye majukumu yake na kutumia ubunifu zaidi tofauti na utekelezaji wa kawaida “kila mjumbe atatuhakikishia jinsi gani ameleta mabadiliko kwa kipindi gani” amesisitiza Naibu Katibu Mkuu.
Dkt Gwajima na timu ya wataalamu aliombatana nao alitumia muda wa masaa 2 dk. 51 kufanya mahojiano ya ana kwa ana ya tathmini ya ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya kila mjumbe wa CHMT toka Halmashauri ya Mvomero na Manispaa ya Morogoro huku wakichambua na kutafsiri kwa undani juu ya matarajio ya kila jukumu. Ambapo katika zoezi hilo waliibuliwa wajumbe kadhaa walionekana kuwa na maono, uwezo, nia na utashi lakini bado hawajapewa fursa inayostahili.
Kwa upande mwingine katika namna isiyotarajiwa baadhi ya wajumbe walikiri kuwa ni kweli ipo changamoto ya utendaji wa mazoea pamoja na baadhi kuwa kwenye nafasi hizo za uongozi miaka mingi llakini bado hawafahamu nini hasa wanatakiwa kufanya bila hata sababu za msingi.
Akizungumza mara baada ya zoezi Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Kusiry Ukio, alisema hakuwahi kutarajia kuna siku atakutana na semina kama hiyo ya kiongozi kuketi na watumishi wanaomsaidia kazi na kuanza kuchambua jukumu moja moja kubaini wanakwama wapi?
Huku akiahidi na kusema umefika wakati wa mabadiliko bila shurti kila mmoja kuonesha uwezo na sio uwingi wa vyeti vya shule. “mara nyingi nimekuwa nikiwaeleza kuhusu utendaji wa mabadiliko, sasa sitegemei kuona mambo yale yale na kama kuna asiyeweza kwenda na kasi hii basi milango ipo wazi kwani katika Mkoa huu wa Morogoro wapo watu wengi tu ambao wanashauku ya kuja kutumika” amesema Dkt, Kusiry.
Mwisho akawataka waganga Wakuu wa Mikoa yote nchini kuhakikisha wanachukua hatua stahiki kwa watumishi ambao wataonekana kutaka kukwamisha ajenda ya mabadiliko kwenye sekta ya afya na kuweka watu watakaoweza kwenda na kasi ya sasa.
Akiwa mkoani hapo Naibu Katibu Mkuu, ametembelea Halmashauri za Wilaya za Malinyi, Mlimba, Mvomero, Gairo na Morogoro Manispaa, ambapo amefanya ukaguzi wa Majengo yanayojengwa na yanayoendelea kujengwa pia amefanya tathimini ya hali ya uendeshaji wa huduma za Afya katika Hospitali na Vituo vya kutolea huduma za afya ambapo, amegundua kuwa wakati timu ya afya ya mkoa imekuwa ikifanya vizuri katika kuelimisha na kufuatilia wapo baadhi ya wajumbe CHMT ambao wamekuwa wakipokea lakini hawatekelezi ipasavyo.