Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemai Jafo akiongea na Viongozi wapya walioteuliwa kushika nyadhifa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa leo kwenye Ofisi ya Rais- TAMISEMI iliyoko Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemai Jafo(kushoto) akimkabidhi vitendea kazi Mkuu wa Mkoa Mpya wa Dar es salaam, Mhe. Aboubakar Kunenge baada ya kuongea na Viongozi wapya walioteuliwa kushika nyadhifa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa leo kwenye Ofisi ya Rais- TAMISEMI iliyoko Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemai Jafo(kushoto) akimkabidhi vitendea kazi Katibu Tawala wa Wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro, Bi.Johari Khamis baada ya kuongea na Viongozi wapya walioteuliwa kushika nyadhifa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa leo kwenye Ofisi ya Rais- TAMISEMI iliyoko Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemai Jafo akiwa katika picha ya Pamoja na baadhi ya viongozi wapya walioteuliwa kushika nyadhifa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa leo kwenye Ofisi ya Rais- TAMISEMI iliyoko Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma
……………………………………………………….
Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemai Jafo amewataka viongozi wanaopatiwa dhamana katika nchi kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa kufanyakazi kwa bidi ili kuacha alama kwa jamii.
Akiongea na Viongozi wapya walioteuliwa kushika nyadhifa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa leo kwenye Ofisi ya Rais- TAMISEMI iliyoko Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma Mhe Jafo amesema kuwa viongozi wanatakiwa kufanyakazi kwa bidi, weledi na uaminifu hasa katika suala zima la kutatua kero za wananchi kwenye maeneo yao.
Mhe. Jafo anafanua kuwa viongozi walioteliwa na kupatiwa dhamana wanapaswa kufanya, kusema na kutenda yale ambayo yatamuacha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania salama, hivyo kushindwa kutimiza majukumu yao ni kumuangusha Rais ambaye lengo lake ni kuwasaidia wananchi maskini.
“Ieleweke kuwa asilimia 21 ya Bajeti ya Serikali ipo OR-TAMISEMI, asilimia 72.6 ya watumishi wote nchini wanatoka Ofisi ya Rais TAMISEMI na miradi yote inayogusa wananchi OR-TAMISEMI, hivyo tukishindwa kutimiza vyema majukumu yetu, kelele za wananchi zinakuwa kubwa kuliko jambo linguine lolote, hivyo katimizeni majukumu yenu kwa ufanisi mkubwa” amesisitiza Mhe. Jafo.
Amewaagiza viongozi hao kusimamia vyema fedha za Serikali zinazotolewa kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo ili iweze kukamilika kwa wakati na kuhakikisha inaanza kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kuhusu Utendaji kazi Mhe. Jafo amewataka kuacha kufanyakazi kwa maigizo kwa kutaka sifa na umaarufu bali wafanye kazi kwa kuwahudumia wananchi na kutatua kero zao kwa wakati ili kupunguza malalamiko na kuleta maendeleo katika maeneo yao.
Ameendelea kuwataka viongozi hao kudumisha ushirikiano, kuacha malumbano na kufanya kazi kwa umoja ili kuhakikisha wanawasaidia wananchi katika kutatua kero na changamoto walizonazo lengo likiwa ni kuleta maendeleo kwa jamii na Taifa kwa ujumla
“Haipendezi kukuta, Mkuu wa Mkoa anagombana na Mkuu wa Wilaya, au Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya kazi haziendi kwasababu ya ugomvi wenu, kusema ukweli sitarajii viongozi nyinyi ambao Rais amewateua ili msaidie majukumu mkafanya hivyo, haya ni mambo ambayo hayaleti maendeleo katika jamii. “amesema Mhe. Jafo
Aidha amewataka kuhakikisha wanafanyakazi kwa kuzingatia mipaka ya kazi, kwa kuheshimiana na wasifanye kazi kwa kushindana kwa kuwa wote wanajenga nyumba moja ya kuwatumikia wananchi.
Wakati huohuo Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamhanga amewataka viongozi hao kuhakikisha wanasimamia ukusanyaji wa mapato kwenye maeneo yao ili kutimiza malengo yalipangwa na Serikali.
Amewataka kufanyakazi kwa bidi, weledi na uaminifu kwa kutimiza majukumu yao kikamilifu ili kuunga mkono juhudu za Serikali za kuwaletea mabadiliko wananchi hasa katika suala zima la utoaji huduma bora kwa jamii.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-salaam Mhe. Aboubakar Kunenge amesema kuwa watashirikiana katika utendaji kazi ili kutimiza malengo ya Serikali ya kuwahudumia wanachi, hivyo watekeleza maagizo yatakayotolewa na Serikali na watatimiza majukumu Kikamilifu.