********************************
Na John Walter-Babati
Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa, imewaonya viongozi wa chama cha Mapinduzi (CCM) ambao wanaondoa majina ya wapiga kura halali wa kura za maoni na kubandika majina ambayo wanaamini watawapigia kura wagombea ambao wanawataka.
Wito huo umetolewa leo Julai 16,2020 na Mkuu wa Takukuru Manyara Holle Makungu baada ya kupata taarifa kwamba baadhi ya viongozi wa chama hicho tawala ngazi ya kata wamekuwa na mtindo huo jambo ambalo ni kinyume na taratibu.
Hata hivyo kufuatia hatua hiyo, Makungu amewasambaza Makachero wa Takukuru kufanya uhakiki wa majina halali kwenye maeneo yanayolalamikiwa.
Makungu amewaambia viongozi wa Chama cha Mapinduzi wanaofanya mabadiliko hayo, wafahamu kuwa hawako juu ya sheria na kwamba kitendo hicho cha kubadilisha majina ya wapiga kura ni kosa la kughushi ambalo likithibitishwa adhabu yake kwa mujibu wa Kifungu cha 337 Penal Code ni miaka saba jela.
Aidha amesema kuwa makosa ya rushwa katika kipindi cha Uchaguzi yameanishwa katika vifungu vya 21, 22 na 23 vya sheria ya Gharama za uchaguzi namba 6/2010 ambavyo ni pamoja na hongo ya fedha kwa wapiga kura ili kuwashawishi kupiga au kutopiga kura , ahadi za ajira kwa wapiga kura kwamba nitakuajiri kwenye ofisi Fulani, kutoa zawadi, mikopo isiyo na riba au riba iliyo kinyume cha sheria.
Pamoja na hayo amesema makosa hayo pia yanamhusu mpiga kura anayekubali kupokea fedha,zawadi, mikopo, ahadi ya ajira au kitu chochote cha thamani ili ampigie kura au asipige kura kwa mgombea.
Ameongeza kuwa ni kosa pia kutoa vyakula, vinywaji kwa nia ya kushawishi wapiga kura, sheria ambayo inaanza kufanya kazi kuanzia wakati wa mchakato wa wagombea ndani ya vyama vyote vya siasa hadi wakati wa uchaguzi mkuu hapo Oktoba 2020.
Ametoa onyo kwa Viongozi hao wa kata warejeshe majina ya wapiga kura za maoni ambao ni halali mara moja na kuwataka makatibu wa wilaya wa chama cha Mapinduzi kutoa ushirikiano kwa makachero wao wanaoshugulikia uchunguzi huo kubaini wachache wanaotaka kurejesha demokrasia nyuma.