Na Masanja Mabula. PEMBA
MAHAKAMA ya Mkoa Wete imemtoza faini ya shilingi 500,000 na fidia ya shilingi 200, 000 Seif Othman Khamis (23) mkaazi wa Ndagoni Wilaya Chake Chake kwa kosa la kufanya shambulio la aibu kwa mtoto mwenye umri wa miaka 16 mkaazi wa Mtambwe.
Imeelezwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali Ali Amour Makame mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Abdalla Yahya Shamhuna kwamba kijana huyo alitenda kosa hilo tarehe 10/11/2018 majira ya saa 10:00 jioni huko Kinazini Mtambwe alimchezea binti huyo, sehemu za maungo ya siri jambo ambalo ni kosa kisheria.
Aidha kosa alilotenda ni kinyume na kifungu cha 114 (1) sheria nambari 6 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar,
Endapo atashindwa kulipa faini na fidia hiyo, atalazimika kutumikia kifungo cha miaka miwili katika chuo cha mafunzo.
Wakati huo huo Mahakama hiyo ya Mkoa Wete mbele ya hakimu huyo imemuachia huru mtuhumiwa Juma Rashid Daudi miaka 20 mkaazi wa Majenzi Micheweni anaedaiwa kumtorosha, na kumbaka msichana mwenye umri wa miaka 17.
Hayo yalijiri baada ya mashahidi wa upande wa mlalamikaji kushindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi.
Awali ilielezwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka wa Serikali Ali Amour Makame kuwa, , Oktoba 29/2019 majira ya 1:00 usiku eneo la Ndaambani wilaya ya Micheweni, bila ya halali na bila ya ridhaa ya wazazi wake alimtorosha msichana jina linahifadhiwa, kutoka nyumbani kwao na kumpeleka eneo ambapo ni kosa kinyume na kifungu cha 113[a] Sheria nambari 6 ya 2018 cha sheria ya Zanzibar.