NA DENIS MLOWE,MUFINDI
WAFANYAKAZI wa Benki ya NMB tawi la Mafinga wametoa msaada wa sabuni na vitakasa mikono zaidi 100 kwa shule za msingi za Wambi na Nyamalala zilizoko kwenye halmashauri ya Mji Mafinga ili waweze kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona.
Wafanyakazi hao ambao waliombwa msaada huo na mkurugenzi wa mji wa Mafinga, Saada Mwaruka na kuamua kuchangishana kama wafanyakazi na kuamua kutoa msaada huo kwa lengo la kuendelea kuwa karibu zaidi na jamii.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Saada Mwaruka, Meneja wa Benki ya NMB tawi la Mafinga, Mary Mpasha alisema kuwa baada ya kupata maombi ya kuombwa msaada waliamua kuchangishana na kufanikiwa kupata vifaa hivyo kwa ajili ya wanafunzi.
Alisema ku wakati wote wafanyakazi wanaamini katika kugusa na kubadili maisha ya wanajamii, ushiriki wa Wafanyakazi katika programu za kuisaidia jamii iliwagusa wafanyakazi hao na kuamua kutoa sehemu ya mishahara yao kwa ajili ya kutoa msaada kwa shule hizo.
“elimu ni haki ya msingi na kipengele muhimu cha malengo endelevu ya milenia, tunatambua mchango muhimu wa shule ya msingi hivyo baada ya serikali kuruhusu masomo kuendelea umuhimu mkubwa ni kuwafanya wanafunzi wasome katika mazingira salama Hali iliyotulazimu kuchangishana sehemu ya mishahara na kuwaletea msaada. huu.” Alisema
Aidha Mpasha aliwataka wanafunzi hao kuwa mabalozi wazuri wa benki ya NMB na kutoa wito kwao kuwashawishi wazazi na walezi kuwafungulia akaunti za watoto na masomo kwani zitawasaidia kwa kiasi kikubwa kwenye masomo yao.
Akizungumzia msaada huo mkurugenzi wa Mafinga Mji, Saada Mwaruka aliwapongeza wafanyakazi wa NMB kwa kuwakumbuka wanafunzi na walimu wa shule hizo kwani utawasaidia kwa kiasi kikubwa kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona na kuepuka magonjwa mingine yanayosababishwa na uchafu yakiwemo kuhara.
“Tunaishukuru wafanyakazi wa NMB Mafinga kwa kwa msaada huu wa sabuni za kunawa na vitakasa mikono kwani zitatusaidia sana katika kipindi hiki hasa itasaidia pia wanafunzi kuepuka magonjwa mengine ya kuhara, kipindupindu kusisitiza wanafunzi kutambua matumizi ya kunawa mikono mara kwa mara,” alisema
Mwaruka alisema kuwa mbali na kupewa msaadakutoka kwa wafanyakazi lakini Benki ya NMB pia amekuwa ikiwaunga mkono mara kwa mara na ni msaada mkubwa kwenye jamii ya mkoa wa Iringa na kutoa wito kwa wadau wengine kuendelea kushirikiana katika kusaidia makundi mbalimbali.