…………………………………………………………………….
Na.Mwandishi Wetu- MAELEZO
Waziri wa Viwanda wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Balozi Amina Salum Ali amefunga rasmi Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA), yaliyokuwa yanafanyika katika viwanja vya Mwl.Julius Nyerere barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika Maonesho hayo, Balozi Ali amesema kuwa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania, (Tantrade) inatakiwa kuangalia namna ya kushusha huduma kwa wananchi walioko katika maeneo mablimbali ya uzalishaji malighafi na bidhaa ili waweze kujua changamoto za wafanyabiashara hao wa chini.
“Siri kubwa ya maendeleo katika Sekta ya biashara ni kushusha huduma kwa wafanyabiashara wa chini kule ambako uzalishaji wa vitu vingi upo yaani malighafi na bidhaa ndogo ndogo huko ndiko kuna changamoto ambazo zikitatuliwa zitaleta maendeleo makubwa kwa wafanyabiashara wa kati na wakubwa hatimaye kukuza viwanda vitakavyoleta uhusiano mkubwa wa biashara”, Alisema Balozi Amina Ali.
Balozi Amina Ali alisema kuwa Tantrade ina jukumu kubwala kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kuwa wakati na wakati kuwa wafanyabiashara wakubwa na hiyo itaondoa changamoto na kukuza biashara katika maeneo mbalimbali nchini ambako bidhaa zinazalishwa na kukosa soko mara kwa mara.
Alivitaka vyombo vinavyohusika na biashara kwa Tanzania bara na Zanzibar kuwasikiliza wazalishaji wa malighafi hizo ambazo zinatagemewa viwandani kutoa bidhaa kwa wafanyabiashara wakubwa ni hii itasaidia kujua wakulima, wazalishaji wa bidhaa ndogondogo wanataka nini ili kuendana na soko la kimataifa.
Aidha alivitaka vyombo hivyo kushusha huduma za biashara ikiwemo utafutaji masoko na aliwapongeza TMX ambao wanafanya minada kwa wananchi kwa kutumia mtandao na wananchi ambao ni wazalishaji kupata bei iliyoko sokoni katika soko la kimataifa.
“Kushusha huduma hizo kwa wananchi hususani wale wanaozalisha malighafi kutoka shambani ni moja ya kuwapatia nguvu na kujua wapi wanaweza pata soko kwa faida Zaidi, nawapongeza sana TMX ambao wanafanya biashara ya mnada ya kuwakutanisha wafanyabiashara wakubwa nawananchi ana kwa ana na sehemu zingine kwa njia ya mtandao kwa hiyo wananchi vyombo vyetu endeleeni kuwajali wananchi kwa kuwatafutia masoko”, Alisisitiza Balozi Amina Ali.
Alibainisha kuwa viwanda vinafanya vizuri kwa sasa kwani kila sehemu kuna kiwanda ambako mazao au malighafi rasmi inazalishwa alitolea mfano kiwanda cha maparachichi, viwanda vya mkonge, viwanda vya alizeti na viwanda vya nyama hiyo inatoa fursa kubwa sana kwa wafanyabisahara wadogo wa mazao na bidhaa za viwandani
Balozi ali aliwapongeza Tantrade kuja na wazo la kulete banda la mazoa ya kimkakati ili kuwezesha wananchi kujua namna ya kulima mazao hayo na kujipatia kipato kikubwa, alitaja bodi hizo kuwa ni Bodi ya Mkonge, Bodi ya Korosho, Bodi ya Pamba, Bodi ya Kahawa, Bodi ya Pareto na Bodi ya Sukari ambazo zilikuwepo katika maonesho ya 44 ya biashara ili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kulima na kuuza mazao hayo.
Mwisho