********************************
Manispaa ya Kinondoni imepokea Vifaa vya kujikinga na maambukizi ya Virus vya Corona kutoka Shirika la kulinda Watoto (Save the Children) kwa lengo la kuwakinga wanafunzi na Virusi hivyo.
Akipokea Vifaa hivyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispa, Ndugu. Aron Kagurumjuli, Mganga Mkuu Dokta Samwel Laiza amelishukuru shirika hilo na kusema kuwa vitawasaidia wanafunzi kujikinga na Virusi vya Corona katika kipindi hiki ambacho jamii bado inaendelea kuchukua tahadhari.
“Tunawashukuru Ndugu zetu hawa sababu wameona kuna umuhimu mkubwa wa kuwakinga watoto kwani corona bado ipo japo imepungua sana, lakini kama jamii bado inatakiwa kuchukua tahadhari kama wataalamu wa Afya wanavyoshauri”
amesema Dkt Laiza.
Ameongeza kuwa Kinondoni ina mkakati wa kufanya zoezi la unawaji wa mikono kuwa endelevu hata baada ya kuisha kwa mlipuko wa ugonjwa huo kwani tafiti zinaonesha kunawa mikono kunapunguza maambukizi ya magonjwa ya kuambukizwa kwa asilimia 60.
Awali akikabidhi vifaa hivyo, Meneja wa uchechemuzi na kampeni wa shirika la Save the Children Bi Nuria Mshare amesema kama shirika wana wajibu wa kuhakikisha watoto wanakuwa salama , hivyo wameguswa kuwasaidia ili wawesalama.
Amesema kuwa vifaa hivyo vitawasaidia wanafunzi kuwa salama pindi wnaapokuwa shuleni kwakunawa mikono kwa maji tiririka pamoja na vitakasa mikono kabla na baadaa ya kuingia madarasani wakati wote watakapokuwa kwenye masomo yao.
Ameongeza kuwa shirika hilo litaendelea kuwa begakwabega na Manispaa ya Kinondoni ikiwa ni katika kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya virusi vya corona kwa wanafunzi yanafanikiwa pamoja na na Wanafunzi kuendelea na masomo yao bila kuwa na usumbufu wowote.
Naye mwalimu mkuu wa Shule ya Secondari ya Kigogo Mwl Ester Idabu amesema awali walikuwa na changamoto ya vifaa vya kunawia ambapo walikua wanatumia ndoo za kawaida hali iliyowalazimu kujaza maji kila baada ya muda na kwamba baada ya kupata Matanki hayo yatapunguza usumbufu huo.
Afisa elimu Msingi anaeshughulika na masuala ya Afya za Wanafunzi Bi Martha Kusaga amesema vifaa hivyo vitagawiwa kwa shule kumi ambazo ni Kisauke ( Msingi na sekondari) , Sekondari za Kigogo, Mikocheni, Kawe na Bunju , Shule za Msingi Changanyikeni, Salasala, Mbezi Ndumbwi pamoja na Makongo juu.
Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na Matanki ya maji 20, Sabuni za kunawia mikono 500, Taulo za kike 1000 na Nguo za ndani 500.