Mwenyekiti wa JUKWAA la Vijana wa Tanzania, Ramadhan Magambo (katikati)akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani wakati akitoa taarifa ya kumuunga Mkono Rais Dk.John Magufuli katika uchaguzi Mkuu 2020 tukio hilo limefanyika leo jijini Dodoma.
Katibu wa JUKWAA la Vijana wa Tanzania Bw.Frank Chirare,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wakitangaza nia ya kumuunga mkono Rais Dk.John Magufuli katika uchaguzi wa Oktoba 2020 kutokana na utendaji kazi wake leo jijini Dodoma.
Katibu wa JUKWAA la Vijana wa Tanzania Bw.Frank Chirare,akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wakitangaza nia ya kumuunga mkono Rais Dk.John Magufuli katika uchaguzi wa Oktoba 2020 kutokana na utendaji kazi wake leo jijini Dodoma.
……………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna, Dodoma
Mwenyekiti wa JUKWAA la Vijana wa Tanzania, Ramadhan Magambo, amesema kuwa vijana wana kila sababu ya kumuunga mkono Rais John Magufuli katika uchaguzi Mkuu 2020 kutokana na utendaji kazi wake kuwagusa wananchi hasa vijana.
Wito huo ameutoa leo wakati jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa Habari
Aidha amesema kuwa wao kama vijana wana kila sababu ya kumuunga mkono kwani wanaamini katika kipindi hiki amefanya mambo makubwa kwa watanzania hivyo Rais atapitishwa na chama chake(CCM).
“Kwa miaka mingi vijana tumekuwa tukitumika kama daraja, zile zama za vijana kuonekana tuna umuhimu kwa kipindi fulani zimepita, vijana tupo zaidi ya asilimia 60 nchini tunaamini vijana pekee tunatosha kusema tunayemtaka,”ameeleza Magambo.
Magamboamesisitiza kuwa vijana bila kujali itikadi zao wataenda kwa pamoja kumuunga mkono Rais kama watanzania ambao hawafungamani na chama chochote.
“Lengo sisi kama vijana tunataka kumpa zawadi Rais Magufuli katika uchaguzi mkuu, hakuna mtanzania asiyejua mema yaliyofanywa na Rais Magufuli,tutampigia kura za kishindo, na tunataka kuandika historia ya Taifa letu kwamba ndio Rais atakayekuwa amechaguliwa kwa kishindo,”ameweka bayana Magambo.
Kwa upande wake, Katibu wa Jukwaa hilo, Frank Chirare, amesema Rais ameweza kupambana na vitendo vya rushwa ambapo hivi sasa wananchi wanahudumiwa bila kutoa chochote.
Chirare ameongeza kuwa Rais Magufuli amefanya mengi ikiwemo kuongeza mapato ya nchi na hivyo kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati kabla ya mwaka 2025.
“Kwa hiyo kwa hayo tuliyoyapima kwenye utendaji wake, na kiongozi tunayemtaka tumeshamuona kupitia uwajibikaji wake Rais Magufuli, amekaa ndani na kujishughulisha na mambo ya nchi yetu hakuwa mtu wa kusafiri,”amesema Chirare.
“Tutaenda mbele na Rais Magufuli na kuhakikisha anarudi tena Ikulu ili kuiona Tanzania bora zaidi na kufikia uchumi wa juu zaidi,”amesisitiza Chirare.