************************
Mwandishi wetu
Wafanyabiashara na waajiri nchini wamekumbushwa kuhakikisha wanazingatia suala la usalama na afya kwa wafanyakazi wao wakati wote, kwani ni sekta muhimu ili kuwezesha kufikia uchumi wa kati.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Semina ya siku moja ya kampeni maalumu ya vision zero, ambayo inaratibiwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) iliyofanyika jijini Mbeya , Mkuu wa mkoa wa Mbeya Mhe. Albert Chalamila amesema uchumi wa kati unategemea kwa kiasi kikubwa wafanyakazi wenye afya njema, kwani ni mtaji namba moja katika kuwezesha uchumi huo.
‘’Uwekezaji wa kwanza katika ukuaji wa uchumi katika taifa lolote linalokuwa ni uwekezaji wa watu, ni rasimali watu, ni muhimu sana ili watu waweze kufikia uchumi mwingine tunaouzungumzia, kumbe usalama na afya kwa wafanyakazi, hasa sehemu za kazi ni jambo la msingi sana sisi kama wafanyabiashara,waajiri ,waajiriwa tunapaswa tuyaelewa hayo kwa pamoja sana’’ Alisema Chalamila
Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Mkurugenzi wa usalama na Afya, Alex Ngata amesema lengo la kukutana na wafanyabiashara na waajiri hao mkoani Mbeya ni muendelezo wanaoufanya kutoa uelewa wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi kwa wadau mbalimbali nchini,ni kupitia mafunzo maalumu ya kutoa elimu ya usalama na afya kwa wafanyabiashara na waajiri ya vision zero.
‘’Pamoja na kutoa elimu,tumekuja pia kusikiliza matatizo yao, inawezekana kwa namna moja au nyingine wanakwazika kwa jinsi tunavyotoa huduma hii kwao, kuhakikisha kwamba suala la usalama na afya linazingatia katika maeneo yao ya kazi’’ Aliongeza Ngata
Kwa upande wake Mkurugenzi wa mafunzo, utafiti na takwimu toka OSHA Bwana Joshua matiko alisema, katika utafiti huo walioufanya kwa kipindi cha mwaka 2013 hadi 2018/2019, walipata takwimu 1230 za matukio ya ajali, na katika matukio hayo, walibaini watu waliokuwa nje ya vituo vya kazi ilikuwa ni wastani wa siku 12.1, na kulikuwa na tofauti siku 41 ukijumlisha upata siku 53 ambapo wafanyakazi walikuwa wanakaa nje ya kituo cha kazi kutokana na ajali, hivyo watu waliokuwa wanapata ajali walikuwa wanakaa nje ya kazi kwa muda mrefu
‘’Na katika utafiti huo tulibaini mameneja, ndio waliokuwa wanakaa muda mrefu nje ya kituo cha kazi wanapoumia sehemu za kazi kuliko watu wa kawaida’’ alisema Matiko
Ndugu Matiko alisema katika utafiti huo walibaini wadau wengi hawana utaratibu wa kuweka rekodi za ajali zinazotokea sehemu zao za kazi, sekta ya uzalishaji ndio inayoongoza kwa kusababisha ajali, ikufuatiwa na sekta ya ujenzi na majenzi, na ndio maana wakaamua kuja na program maalamu ya kuelimisha umma juu ya kupunguza ajali na magonjwa sehemu za kazi. Amesema lengo kuu la kuanzishwa kwa Vision zero ni kuhakisha maeneo yakazi yanakuwa na mifumo, yakuwezesha kuzuia ajali na magonjwa sehemu za kazi.
Na kwa upande wao washiriki wa semina hiyo wamesema mafunzo hayo yatasaidia kuwawezesha kuweka mifumo ambayo itasaidia kuwalinda wafanyakazi dhidi ya magonjwa na ajali sehemu kazi kwani jambo hilo litawezekana, amesema kuna mambo mengi ambayo yalikuwa hayaeleweki lakini kupitia semina hiyo, wameweza kufahamu mengi.
Vision zero ni programu maalumu iliyoanzishwa kwa lengo la kupunguza au kuondoa kabisa ajali na magonjwa sehemu za kazi, ambapo waajiriwa wanapaswa kuhakikisha wanakuwa na mifumo madhubuti ya kuhakikisha inawalinda wafanyakazi dhidi ya magonwa na ajali sehemu za kazi.