**************************************
Na Mwandishi wetu Mihambwe
Waendesha Pikipiki almaarufu kama Bodaboda pamoja na Wananchi wamelipongeza Jeshi la Polisi kwa kudumisha urafiki, mshikamano na ushirikiano.
Hayo yamejiri kwenye mkutano ulioitishwa na Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu uliofanyika katika kiwanja cha shule ya Msingi Kitama ambapo aliwakutanisha Polisi pamoja na Bodaboda ambapo kila pande imefurahia mshikamano huo na kuomba uzidi Kudumu na hali ya kuonana maadui iishe.
“Nashukuru ujio wa Polisi uliotupa mwelekeo wa namna ya kushirikiana na kutukumbusha umuhimu wa kutii sheria bila shurti. Hili tukio la leo ni la kwanza kutokea, tunawahaidi ushirikiano.” Alisema Kassim Mnyangula kiongozi wa Bodaboda Kata ya Kitama.
Nae Haroun Rada amewashukuru Polisi kujenga mahusiano mapya na kutoa elimu kwa jamii ya kutii sheria ambapo ameomba iwe hivyo kwenye makundi yote.
“Kipindi cha nyuma tulikuwa kama maadui na Polisi, ila leo tumeanza upya nao. Tunamshukuru sana Afisa Tarafa Mihambwe kwa kuleta tukio hili la kutuunganisha kati ya Polisi, Bodaboda na Wananchi. Ni tukio la kihistoria.” Alisema Bashiru Ahmad mkazi wa Kijiji cha Mwenge kilichopo kata ya Kitama.
Mkuu wa kituo cha Polisi Mathias Kipeta aliwasisitiza Wananchi kuwa na ushirikiano na urafiki na Jeshi la Polisi kwa kutii sheria bila shurti. Pia wadumishe amani na usalama nyakati zote hususani kipindi cha uchaguzi Mkuu wa kuwachagua Madiwani, Wabunge na Rais.
Akizungumza mara baada ya mkutano huo Gavana Shilatu alisisitiza kila mmoja ana jukumu la kuhakikisha ni mlinzi wa amani na usalama, anatii sheria bila shurti ili kudumisha umoja na mshikamano.
Mkutano huo ulihudhuliwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi wilaya, Askari Mkuu upelelezi wilaya, Kamanda wa Polisi wilaya kikosi cha usalama barabarani, Afisa Tarafa Mihambwe, Polisi Kata Kitama, Serikali Halmashauri za vijiji, Bodaboda pamoja na Wananchi.
Wakati huo huo, mara baada ya mkutano huo kumalizika ilichezwa mechi kali ya kirafiki kati ya timu ya Bodaboda na Polisi ambapo Polisi walishinda bao 3 kwa 2 dhidi ya Bodaboda.