Washiriki wa Mafunzo ya Mafunzo ya Haki za Binadamu , unyanyasaji na ukatili wa kijinsia hususan kwa wanawake na watoto (wa kwanza kulia) ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe.Rehema Kerefu na (wa pili kulia) ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Gerald Ndika wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo.(wa tatu kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Joaquine De Mello.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakijadiliana kwa pamoja mambo yanayohusu mafunzo hayo.
Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Sehel, na (kushoto) ni Mwenyekiti wa TAWJA Mhe. . Joaquine De Mello na baadhi ya washiriki wakifuatilia kwa karibu mafunzo hayo.
……………………………………………………………………………
Na Tawani Salum – Mahakama
Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Jaji Gerald Ndika amewataka Majaji na Mahakimu kutafsiri sheria zinaohusu masuala ya wanawake na watoto ili ziendane na mazingira ya sasa katika kuendesha mashauri yanayohusu masuala la unyanyasaji na ukatili wa kijinsia.
Akizunguza wakati wa Mafunzo ya Haki za Binadamu na Unyanyasaji hususani kwa wanawake na watoto, yanayofanyika Mjini Bagamoyo Mkoa wa Pwani Jaji Ndika alisema kuwa sheria zilizopo kwa kiwago kikubwa zinajitosheleza kinachotakiwa jinsi ya kuzitafasiri, hivyo Majaji na Mahakimu watoe tafsiri ambayo inaendana na mazingira ya matukio yalivyo.
Jaji Ndika ambaye ni mshiriki katika mafunzo hayo, alisema kuwa moja ya faida zake ni kuwaandaa wawezeshaji katika eneo hilo ili kusaidia Mahakama ya Tanzania, Majaji wa Mahakama ya Rufani,Majaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu,watumishi mbalimbali ambao wanatoa maamuzi juu ya vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa wanawake na watoto kuwa na umahiri.
‘‘Matukio haya yanatokana na mambo mengi ikiwemo mila potofu pamoja na uelewa wao mdogo, wanaona kumpiga mke au mtoto ni jambo la kawaida na ana haki ya kufanya hivyo. Lakini ubora wa mafunzo haya yatasaidia kupata wakufunzi ambao wataenda kuwapa wengine elimu juu ya kuweza kupambana na ukatili na unyanyasaji wa wanawake na watoto,’’ alisisitiza Jaji Ndika. mafunzo hayo, alisema ni ya mara ya tatu kufanyika yakiwa ni endelevu katika kutoa elimu hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Joaquine De Mello akifungua rasmi mafunzo hayo, alisema kuwa yana lengo la kuwawezesha watoa maamuzi kuwa na uweledi zaidi wa kutoa haki na pia kuielimisha jamii juu ya haki zao za msingi na tatizo la unyanyasaji na ukatili wa kijinsia ambalo limekithiri.
Aliongeza kwamba kumekuwa taarifa nyingi zinazotolewa na vyombo vya habari pamoja na wanajamii ambao wamejitokeza wazi kutoa matukio mbalimbali juu ya suala hilo. Pia tafiti mbalimbali ambazo zimefanywa hivyo wamegundua kuwa matukio mengi ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia yanafanywa wahusika wanaotuhumiwa kuwa ni familia au ndugu wa karibu.
Alisema kuna mapungufu katika jamii kama vile utamaduni wa kutokuwa na utayari wa kusimamia na kuyapigia kelele tatizo hilo, ikiwa ni sababu mojawapo ya unyanyasaji na ukatili huo.
‘‘Kupitia mafunzo haya kama watoa maamuzi tunataka wapate jicho la kipekee shauri linapokuja mbele yako mara moja unapata picha kuwa hili ni la kikatili na unalipa nafasi yake na hii itasaidia katika kuandaa taarifa ya matukio haya kwa usahihi, ikiwemo kuna takwimu ambazo tunazihitaji ili kujua nguiu gani ya ziada inahitajika katika kusimamia jambo hili,’’ alisema Jaji De Mello.
Mshiriki mwingine wa mafunzo hayo, ambaye Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine,iliyopo Jijini Dar es Salaam Mhe, Hanifa Mwingira alisema jamii inapaswa kuona kuwa vitendo hivyo ni vibaya na kila mtu anapaswa kusema ‘ukatili sasa basi na mtoto wa mwenzako kuwa ni mtoto wako na hupaswi kumfanyia ukatili,’.
Mwingira alifafanua kuwa mafunzo hayo yametolewa kwa viongozi wa dini ambao watawaelimisha waumini wao, wakiwemo Wenyeviti wa vijiji, kata pamoja na mitaa na Maafisa wa Ustawi wa Jamii, Polisi, Magereza na wadau wengine wa sharia.
Mafunzo hayo yanayoendelea Mjini Bagamoyo Mkoani Pwani yalihudhuriwa na Majaji Wataafu kama vile Mh. Jaji Salum Massati ambaye anashiriki kama mtoa mada,
Jumla ya washiriki 26 wanapatiwa mafunzo juu ya masuala ya unyanyasaji na ukatili kijinsi. Mafunzo hayo yameanza Juni 27, mwaka huu na yatamalizika Julai Mosi, mwaka huu.