Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akizungumza na mamia ya waendesha bodaboda na magario waliofurika Kituo cha Mafuta (Sheli), Kibaigwa Mkoani Dodoma, leo, waliopanga foleni kwa ajili ya kununua mafuta. Simbachawene amemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi kushirikiana na EWURA kuwakamata Wafanyabisha wa Kampuni mbalimbali waliohodhi mafuta na kuleta taharuki kubwa nchini.
………………………………………………………………………….
Aagiza RPC na OCD kufanya ukaguzi vituo vya mafuta nchini, kuwakamata wanaoficha mafuta.
Na Felix Mwagara, MOHA Kibaigwa
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi kushirikiana na EWURA kuwakamata Wafanyabisha wa Kampuni mbalimbali waliohodhi mafuta na kuleta taharuki kubwa nchini.
Amesema Mkoa wa Dodoma na Singida Kuna ukosefu mafuta kutokana na Makampuni hayo kutokusafirisha mafuta wakiwa na lengo la kusubiri mpaka Jumatano Bei ikiongezeka ili wapate faida.
Akizungumza na mamia ya waendesha Magari na bodaboda walifurika tangu asubuhi katika kituo cha mafuta Cha Kibaigwa, Mkoani Dodoma, leo, Simbachawene amesema nchi haiwezi kuchezewa na matajiri ambao wanaitakia vibaya nchi, lazima wakamatwe na wafunguliwe mashataka
“Haiwezekani nchi ya Rais Magufuli ichezewe hivi hivi, angalia hii foleni, wananchi hawa wanateseka kwasababu ya wafanyabiashara wa mafuta kuhodhi mafuta wakisubiria yapande Bei ndio wauze, lazima wakamatwe haraka iwezekanavyo,’ alisema Simbachawene
Pia aliagiza Makamanda wa Polisi Mkoa (RPC) na Wilaya (OCD) washirikiane na EWURA kufanya ukaguzi wa vituo vya mafuta na kukamata wamiliki wa vituo vyote ambavyo wameficha mafuta hayo.
“Serikali haiwezi ikachezewa hivi hivi, haiwezekani, lazima wanaohoshi mafuta hayo washughulikiwwe haraka iwezekanavyo, Serikali ipo imara na tunafanya kazi muda wote,’ alisema Simbachawene.
Kwa upande wake mwendesha bodaboda Hamisi Shokela ambaye ni mkazi wa Mpwapwa, amesema ametoka Mpwapwa tangu asubuhi amekuja kutafuta mafuta Kibaigwa ni mbali, na mpaka jioni bado hajayqpatq mafuta kutokana na foleni kuwa kubwa.
“Vituo vingi vimefungwa, kituo hiki pekee hapa Kibaigwa ndicho kipo wazi, na foleni Kama unavyoiona ni kubwa Sana, nipo hapa tangu asubuhi na muda huu ni saa 11 jioni, Mhe Waziri naomba utusaidie na pia tunashukuru kwa kuja hapa,” alisema Shokela.
Pia Gaspar Rwambo mkazi wa Kibaigwa amesema ukosefu wa mafuta hayo umemfanya kwa siku ya leo kutokufanya kazi, na atashindwa kuihudumia familia take.
“Namuomba Mheshimiwa Rais Magufuli aingilie Kati, tunapata shida, leo foleni kubwa kiasi hiki, hatujui kesho itakuaje, tangu juzi tunateseka mafuta, hayupo kabisa, na hii ndio sheli pekee inayotoa mafuta Kibaigwa nzima, zingine zimefungwa kutokana na kutokua na mafuta,” alisema Rwambo.
Waziri Simbachawene alifika katika kituo hicho na kusimama akiwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma ndipo akaiona foleni hiyo kubwa ya Magari na bodaboda wakisubiria mafuta.