……………………………………………………………………………
Wizara ya Kilimo imesema mafanikio makubwa yamepatikana nchini katika kuzalisha wataalam wa Kilimo kupitia vyuo vyake na kufanya sekta ya Kilimo kuchangia asilimia 28.2 ya pato la Taifa.
Kauli imetolewa leo (29.06.2020) mjini Morogoro na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati alipofungua kikao kazi cha siku mbili cha Wakuu wa Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo (MATIs) chini ya wizara hiyo.
Kusaya alisema anatambua kuwa Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo vya kati ni kiwanda cha kuzalisha wataalam wenye sifa zinazohitajika katika soko la ajira au ajira binafsi katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo.
“Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo vimetoa mchango mkubwa katika kuhakikisha nchi inakuwa na wataalam wa kutosha wenye weledi wa kusimamia sekta ya Kilimo ambapo jumla ya wataalam 16,570 walihitimu mafunzo yao kwenye vyuo vya mafunzo ya Kilimo nchini kati ya mwaka 2009 hadi 2018” alisema Kusaya
Katibu Mkuu Kusaya aliongeza kusema sekta ya kilimo imeendelea kutoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 58, imechangia asilimia 28.2 ya Pato la Taifa ambapo sekta ndogo ya mazao imechangia asilimia 16.2.
Ili kuendelea kuwa na vyuo bora na vyenye tija Katibu Mkuu Kusaya ameagiza wakuu wa vyuo vyote Kumi na Nne (14) chini ya Wizara ya Kilimo kuweka msisitizo katika kufanya mapinduzi ya kilimo kwa kufundisha wanafunzi kwa vitendo zaidi ili kujenga umahili.
“ Sisi ndio vyuo vya kilimo lazima tuoneshe kuwa tunafanya kilimo cha kisasa. Itakuwa jambo la ajabu kukuta chuo hakina shamba darasa bora la kufundishia wanafunzi” alisisitiza Kusaya.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo amevipongeza vyuo vya kilimo nchini kwa kazi nzuri wanayoifanya kufundisha wanafunzi na wakulima mbinu bora na za kisasa za kukuza sekta ya kilimo.
“Nawapongeza sana na ningependa kuona mnaongeza kasi katika juhudi hizo na pia kuwajengea uwezo wanafunzi katika maarifa na ujuzi wa kilimo biashara kwa vitendo ili kufikia lengo la kuongeza uzalishaji na kuiwezesha Tanzania kupata malighafi kwa urahisi zaidi kwa ajili ya viwanda vinavyozunguka maeneo yenu” alipongeza Katibu Mkuu huyo.
Kikao kazi hicho cha siku mbili kimelenga kuweka mipango imara ya kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanakidhi viwango vinavyohitajika kwenye soko la ajira na kujiajiri. Hivyo wakuu wa vyuo hivyo watajadili changamoto na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Mwisho
Imetolewa na :
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo
MOROGORO
29.06.2020