BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza limewataka viongozi wapya wa baraza hilo kujenga uchumi imara na maendeleo ya waislamu, waondoe migogoro na kuimarisha upendo ili kuleta utulivu mkoani humu na kote nchini.
Rai hiyo ilitolewa jana na Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikh Hasani Kabeke baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa viongozi wa BAKWATA mkoani humu watakaoiongoza kwa miaka mitano akisema kuwa viongozi hao wakafanye maendeleo ya kiuchumi na kiroho pamoja na kutimiza ahadi zao za maendeleo waliyoahidi ili jamii iyaone kwa macho na wahakakikishe wanajenga uchumi imara utakoleta maendeleo kwa waislamu na mtu mmoja mmoja jambo litakalosaidia kuondoa migogoro na kuimarisha upendo ili kuleta utulivu.
“Tunafanya kazi ya dini kila na mmoja akaitendee haki nafasi aliyonayo kwani alijipima kabla ya kuiomba kuwa anaiweza, lakini pia malumbano ya muda mrefu ya makatibu wa wilaya yakome maana tunakwenda kwenye maendeleo,migogoro imeondoka,”alisema Sheikhe Kabeke.
Alisema kupatikana kwa viongozi wapya kulete utulivu kwa ajili ya maendeleo ya waislamu badala ya kufarakana kwani BAKWATA imetukanwa mno kuwa si waadilifu na kuonya baraza hilo si la siasa, hivyo viongozi kwa ujumla wao waondoe tofauti zao yakiwemo makundi na migogoro ili wasonge mbele katika kujenga uchumi wa waislamu.
“Awali tumedhibiti ubadhirifu wa mali za waislamu na misikiti.Rai yangu walioshinda na waliokosa tushikamane maana huu ni uchaguzi wa dini mtu hawezi kuwa kiongozi kwa mapenzi yake bali ya Mwenyezi Mungu,twendeni tukazitafute mali za BAKWATA na waislamu zilipo,tukishindwa tutaondolewa kwa sababu ndio wenye dhamana ya kufanya na kuyasimamia hayo na wala siyo Sheikhe wa Mkoa,”alisema
Akitangaza matokeo Msimamizi wa uchaguzi huo Sheikhe Abdulkareem Jonjo, alisema uongozi ni dhima na dhamana inayotoka kwa Mwenyezi Mungu na akawataka ambao kura hazikutosha wavute subira nafasi bado ipo, wavunje makundi na kuwapa ushirikiano walioshinda ili kuijenga BAKWATA kwa maslahi ya waislamu.
Alisema BAKWATA ni moja ya taasisi chache zenye demokrasia ya kukabidhiana vijiti vya uongozi kwa mujibu wa katiba na kwamba uchaguzi huo umefanyika kwa uwazi na ufanisi mkubwa na naamini waliochaguliwa wamepatikana kwa haki kwani lengo lilikuwa kuondoa makandokando na malalamiko ya wizi wa kura.
Aidha Sheikhe Jonjo akitangaza matokeo alisema wajumbe waliopiga kura walikuwa 44 na hakuna kura iliyohabirika na kumtangaza Moshi Juma Shaaban kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Mwanza kwa kura 29 akichukua nafasi ya Amran Batenga ambaye hakugombea ambapo Shaaban aliwashinda Idrisa Aeshi aliyepata kura 8 na Daud Mkama, kura 7,huku Mohamed Kassanga ambaye hakuwa na mpinzani akitangazwa kuwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya BAKWATA Taifa kwa kura 33 kati ya 44 ambapo za hapana zilikuwa 11.
Wajumbe 17 waliwania nafasi tisa za Baraza la Masheikhe ambapo walichaguliwa Idrisa Kemi kura 27, Rajab Saad 27, Shaaban Hugo 29, Mikidadi Masoud 30 na Ahmed Jaha walipata kura 30 kila mmoja, Fadhil Salum 31, Ismail Suleiman 33, Othman Masasi 39 na Hamis Ramadhan 40 huku watu 15 wakijitokeza kuomba ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa ambapo walichaguliwa 10 ambao ni Ahmed Misanga kura 36, Abdul Abeid 36, Hamidu Seleman 37 , Rajabu Rajabu 38, Hussein Magela na Marzuku Magongo wote walipata 41, Hija Said 44, Wessa Juma 43, Bakari Utali 43 na Mohamed Said 44.
Kwa upande wake mwenyekiti mpya Shaaban kwa niaba ya viongoza wapya aliwashukuru wajumbe kwa kuwachagua akisema uongozi ni dhima na hakuna aliyelazimishwa kugombea hivyo wanaianza Mwanza mpya na kazi yao itakuwa ya kutoa aya endapo watakwenda kinyume waelezwe ukweli ambao utawaponya badala ya kuwasema pembeni.