Mchimbaji mdogo wa madini, Saniniu Kurian Laizer, akimkabidhi waziri wa madini Dotto Biteko mawe ya Tanzanite yenye thamani ya Shilingi Bilioni 7.7 katika hafla fupi iliyofanyika Mirerani.
Na Pamela Mollel – Mirerani
Mkazi wa Mirerani, wilayani Simanjiro, Saniniu Kurian Laizer, ameibuka bilionea mpya mjini baada ya kufanikiwa kupata madini aina ya Tanzanite ambayo yamenunuliwa na serikali kwa gharama ya shilling Bilioni 7.8.
Rais John Pombe Magufuli kupitia simu aliyompigia Waziri wa Madini, Dotto Biteko, amemsifu mchimbaji huyo mdogo, akisema kuwa amefurahi kuona watanzania wa kawaida sasa wameanza kunufaika na rasilimali zilizopo nchini.
Biteko, pamoja na Naibu wake Stansalus Nyong’o walikuwa wamehudhuria hafla maalum ya kumkabidhi mchimbaji huyo mdogo kitita hicho cha fedha, katika eneo la Mirerani, wilayani Simanjiro, mkoani Manyara, siku ya Jumatano ya tarehe 24 Octoba 2020.
“Zamani tulitishwa kwa maneno ya uongo kwamba wachimbaji wadogo hawawezi kuzalisha kutokana na teknolojia duni, lakini Laizer hapa ameweza kuchimba kina cha mita 1800 na kupata madini haya, kwa hiyo Watanzania wanaweza,” alisema Biteko.
Naibu waziri Stanslaus Nyongo amesema kuwa yote haya yamewezekana kutokana na juhudi binafsi za Rais John Magufuli ambaye pia amefanikiwa kuzuia utoroshwaji wa madini ya Tanzanite kwa kujenga ukuta mrefu wa Mirerani.
Nyong’o aliongeza kuwa sekta ya madini kwa sasa inakuwa kwa kasi kuliko sekta zingine nchini.
Naibu waziri wa fedha Ashatu Kijaji ambaye pia alihudhuria hafla hiyo, ameongeza kuwa tangu miaka ya 80 wakati madini ya Tanzanite yalianza kuchimbwa, hayakuwahi kuwanufaisha wananchi wa kawaida hadi kipindi hiki.
“Hatujui huko nyuma tuliibiwa kiasi gani cha madini, lakini leo tunaona jinsi ambavyo watu kama Laizer wananufaika na hapa tunamkabidhi fedha zake zote kupitia mlipaji mkuu wa serikali,” alisema Kijaji.