…………………………………………………………………………….
Na.Imani Mbaga,Dar es salaam
Waswahili husema “kumekucha na makucha yake”, bila shaka aliyetunga msemo huu alikuwa katika dunia ya tatu ambako Waswahili tupo, ambako kila uchao, vituko haviishi kukamilisha maisha ya siku.
Nimeamka na “zengwe” kichwani mwangu, kumfanya akwazikaye na maelezo yangu, asomapo tu,akimaliza atajua mswahili aliyesema “kukicha tu yapo makucha yake” alikusudia nini.
Nimeisoma barua rasmi ya uongozi wa klabu ya Yanga, ikiwa na maudhui ya kukemea mgongano wa kimawazo uliopo miongoni mwa wanachama, mashabiki, wapenda soka na wote wanaoitakia mema klabu kuhusu utendaji wa baadhi ya wachezaji akiwemo #Yikpe, mchezaji aliyetokea kuwa maarufu kwa sababu ya aina ya kiwango anachokionyesha.
Kwakweli #Yikpe hajawahi “kukonga” nyoyo za mashabiki wa klabu aliyojounga nayo toka siku aliposajiliwa.
Kwa kifupi hana uwezo ndiyo lugha tunayoweza kuitumia katika kumuelezea mchezaji huyu ambaye wajihi wake amejengeka vyema, kimo chake kinashawishi kabisa akitajwa kama mshambiaji hodari, lakini utendaji wake asingeweza hata kukaa benchi kwenye timu ya soka ya UMISETA kanda ya kusini.
Naungana na waraka wa klabu kuwaomba mashabiki na wapenzi wa klabu kutomzomea #Yikpe.
Lakini sababu ya kutomzomea si kwakuwa ni mchezaji wa Yanga bali kwakuwa hakujileta na kujisajili mwenyewe.
Sisikii watu wanaomtafuta aliyemsajili wala kumchukulia hatua kwa sababu ya kuihujumu klabu na kuiletea klabu hasara, bali tunaishia kumzomea #Yikpe wakati aliyemsajili ameendelea kujificha kwenye kivuli cha mpapai, hatumuoni?
Usajili wa #Yikpe umefunua udhaifu katika mifumo pacha ya muhimu sana katika uendeshaji wa klabu ya soka.
Kwanza ni mfumo wa uendeshaji wa klabu. Kwa mfumo wetu, wanachama wanachagua uongozi kwa kumpigia kura mwenyekiti na kamati ya utendaji, kisha kukabidhi jukumu la kuendesha klabu na kuleta mafanikio.
Mfumo huu humfanya mwenyekiti ateue kamati, na mojawapo ya kamati ni ile inayoshughulikia usajili.
Kamati hizi ndo mwanzo wa uharibifu na uhujumu wa klabu, kwakuwa uteuzi hauzingatii weledi, uzoefu, matakwa ya nyakati bali hapa tunaangalia zaidi kambi za uongozi nyakati za uchaguzi na kuwapa nafasi tuliopiga nao kampeni.
Mfumo huu ndiyo unaotuletea akina #Yikpe wengi katika klabu zetu, kwa sababu usajili wa kamati hauongozwi na misingi ya weledi wa soka, wala uhitaji wa klabu husika bali wizi, kujinufaisha na mashindano kama si kukomoana.
Kumzomea #Yikpe, #Molinga na wengineo haitakuwa msaada wa kuondoa uozo huu kwenye sajili za klabu zetu.
Swali muhimu la kujiuliza ni je? #Yikpe alisajiliwa kwa shilingi ngapi na ni nani aliyezitoa hizo fedha? Je? Aliyetoa fedha haumii kwa fedha yake kwenda bure?
Nilichogundua, aliyemsajili alimleta ili apate “cha juu” na wala si magoli, wakati mashabiki wanategemea magoli, hivyo ni lazima utokee ugomvi.
Tunaelekea kipindi cha usajili, kama tutaendelea na utamaduni huu, basi tutarajie akina #Yikpe wengine wengi na “zomea zomea” zisizokoma kamwe.
Wachezaji wasio na ubora siku zote ni kivuli cha mpapai katu huwezi kujikinga na “jua” la matokeo mabovu, na waliowasajili wanajificha nyuma yao, tukitaka kuwang’amua ni rahisi