………………………………………………………………………………………………
Wafanyakazi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira pamoja na wadau mbalimbali wa mazingira nchini wamefanya usafi katika fukwe za Bahari ya Hindi za Salender jijini Dar es Salaam katika kuadhimisha wiki ya utumishi wa umma hapa nchini.
Zoezi la usafi katika eneo hilo limeongozwa na Meneja wa NEMC kanda ya Mashariki, Anorld Mapinduzi pamoja na Meneja Rasilimali Watu na Utawala Bora, Sima Mwakabalile kutoka NEMC.
Anorld Mapinduzi anasema kuwa katika maadhimisho ya siku ya utumishi ni vyema wadau mbalimbali wakaelewa hakuna utumishi bora bila ya mazingira salama.
“Ili mtumishi aweze kutimiza wajibu wake vizuri na awe na amani ya nafsi na iweze kuleta amani katika familia, jamii na mwisho katika taifa na dunia nzima anahitaji rasilimali za mazingira safi na salama.” Amesema Mapinduzi
Bwana Mapinduzi ameongeza kuwa mazingira salama ndio kitovu cha amani katika kila eneo hivyo ni vyema kuyalinda.
“Ili amani iweze kudumu na kujengeka vizuri ni lazima suala zima la mazingira ambalo nazungumzia uhai endelevu wa binadamu lipewe kipaumbele sana.” Amesema Mapinduzi
Kwa upande wa Meneja Rasilimali Watu na Utawala Bora kutona NEMC Sima Mwakabalile ametoa rai kwa kila mmoja kutunza mazingira na kwamba jukumu la kuyalinda mazingira ni la kila mmoja.
“Leo tuko hapa Kinondoni, ningetegemea sana kuona manispaa ya Kinondoni inahakikisha mazingira ya fukwe zetu yanakuwa salama na sisi kama sehemu yake ndio maana tupo hapa leo kuhakikisha kwamba mazingira yetu yanakuwa salama.” Amesema Mwakabalile
Paul Kiyaga miongoni mwa maafisa wanafunzi kutoka NEMC walioshiriki zoezi hilo anasema kuwa ni zoezi zuri na ni vyema likawa endelevu.
“Hili ni zoezi zuri sana na nadhani ifike wakati siyo NEMC tu pekee watakaofanya zoezi kama hili kwa sababu ndio wanasimamia mazingira. Bali hata taasisi nyingine zifanye hivi.”Amesema Kiyaga
Hatahivyo katika maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma mwaka huu 2020 inakwenda na kauli mbiu inayosema *”Jukumu la Utumishi wa Umma katika kujenga na kudumisha amani iliyopo miongoni mwa jamii”.*