SAILVIA MCHURUZA,BUKOBA.
Mtendaji wa mtaa wa Kyakailabwa katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera amefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Bukoba akikabiliwa na mashtaka mawili ya kumtorosha mtoto mwenye umri wa miaka 14 chini ya uangalizi wa wazazi na kumfanyia shambulio la aibu.
Akisomewa mashtaka hayo namba 149 ya mwaka 2020 na wakili wa serikali Joseph Mwakasege, mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Ruth Migan, amesema mshtakiwa huyo Patrick Rwegasira mwenye umri wa miaka 44 baada ya kumtorosha mtoto huyo aliishi naye nyumbani kwake na alimpapasa matiti akilenga kumfanyia vitendo vya aibu.
Mwakasege amesema kuwa mshtakiwa huyo alimchukua mtoto huyo kutoka kwa wazazi wake Juni 02 hadi 04 alipokamatwa na kupelekwa polisi.
Akijitete mshtakiwa huyo amedai mtoto huyo hajamtorosha bali alikutana naye mtaani baada ya kufukuzwa na wazazi na kuamua kumpa hifadhi kama mtendaji.
Mshtakiwa amerejeshwa rumande kutokana na kukosa wadhamini na kesi yake itatajwa tena Julai 06 mwaka huu