Home Mchanganyiko WEO NA VEO LANGAI KORTINI KWA RUSHWA

WEO NA VEO LANGAI KORTINI KWA RUSHWA

0

……………………………………………………………………………

OFISA mtendaji wa Kata ya Langai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Anna Mlomi na Ofisa mtendaji wa Kijiji cha Langai Masiar Sambana wamefikishwa mahakamani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kusomewa mashtaka ya kudai na kupokea rushwa ya sh100,000.

Mwendesha mashtaka wa polisi, Magira Marwa akisoma hati ya mashtaka mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya hiyo Onesmo Nicodemo, alisema washtakiwa hao walifanya makosa hayo kwenye kijiji cha Langai.

Marwa alisema katika kesi hiyo namba 50 ya mwaka 2020 washtakiwa hao walitenda makosa hayo kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2017.

“Washtakiwa hao walitenda makosa hayo baada ya kuelekezwa na halmashauri ya wilaya hiyo kushughulikia uharibifu wa mazingira kwa kukata miti ovyo uliofanywa na watu bila kibali wakati wanasafisha shamba,” alisema.

Alisema baada ya kuwakamata watuhumiwa hao na kuwafikisha kwenye ofisi ya kijiji waliwapiga faini kutokana na uharibifu huo na ililipwa kihalali na kuingizwa halmashauri.

Alisema wakati watu hao wakiwa mahabusu ya kijiji hicho waliwaomba rushwa ya sh100,000 ili wawatoe mahabusu na wasifikishwe polisi kwa ajili ya hatua zaidi.

Hata hivyo, washtakiwa hao walikana mashtaka hayo mahakamani hapo walipoulizwa kama ni kweli walitenda kosa hilo na walipatiwa dhamana.

Hakimu Nicodemo aliahirisha kesi hiyo hadi Julai mosi mwaka huu itakapotajwa tena mahakamani hapo kwani uchunguzi wa shauri hilo umeshakamilika.

Hata hivyo, mkuu wa Takukuru mkoani Manyara, Holle Makungu alitoa rai kwa watumishi wa umma wa mkoa huo na Tanzania kwa ujumla kutimiza wajibu wao ipasavyo ili kujiepusha na mkono wa sheria.

Makungu alisema inawapasa wafanye rejea kwenye maandiko ya vitabu vitakatifu ikiwemo biblia na Quran ili wasijihusishe na matendo ya rushwa.

Alisema watumishi wanaohusika na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali waliagizwa kutotoza kuliko walivyoamriwa na wote kutosheka na mishahara yao.

Alisema kwa wale wanaokaidi yaliyoandikwa katika vitabu vitakatifu wafahamu kuwa mamlaka ziliwekwa na Mungu hivyo wataendelea kupambana na mkono wa sheria.