**********************************
Na.WAMJW, Dar es Salaam
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kuwapo kwa ugonjwa wa Corona nchini, imeleta fursa ya kuboresha huduma za afya katika vituo mbalimbali vya afya hapa nchini.
Michango mbalimbali iliyotolewa zikiwamo vifaa na vifaa tiba zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha huduma za afya na kuokoa maisha kwa wagonjwa mahututi.
Waziri wa afya Ummy Mwalimu ameyasema hayo wakati akizindua upanuzi wa wodi kwenye hospitali ya Ibrahimu Haji iliyo chini ya Jumuiya ya Khoja Shia Ithna Asheri Jamaat itakayotumika kwa ajili ya kinamama na pia kufungua rasmi huduma za magonjwa ya kawaida ambapo hapo awali walikua wakihudumia wagonjwa wa Corona.
Amesema michango iliyotolewa tangu kuibuka kwa ugonjwa wa Corona, itasaidia kuleta mabadiliko chanya kwa mamia ya Watanazania ambao wamekuwa wakipoteza maisha katika ngazi zote za kutolea huduma za afya za mikoa na wilaya.
“Mchango wenu mlioutoa kwa ajili ya upanuzi wa hospitali hii ni wa thamani kubwa na sisi kama Serikali tutaendelea kuuthamini,” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri huyo amesema anaizundua hospitali, huku wagonjwa wa Corona wakiwa wamepungua nchini, huku akiwasisitiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ili kuhakikisha ugonjwa huo unakwisha.
“Tunaishikuru Jumuiya ya Khoja Shia Ithna Asheri Jamaat kwa ajili ya kujitoa kwao wakati wa kipindi cha ugonjwa wa Corona. Taasisi hii ilituletea msaada wa chakula, hivyo kwa niaba ya Serikali tunawashukuru na tunathamini mchango wenu,” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri wa Afya amesema michango hiyo ni muhimu kwani kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kila watu 1,000 vinatakiwa vitanda vitano. Jijini Dar es Salaam kuna karibu watu milioni 6. Hivyo vinatakiwa kuwa na vitanda vya wagonjwa 30,000,000.
“Sasa vituo vya afya vya Serikali na vya binafsi katika Jiji la Dar es Salaam, havifikishi vitanda 10,000, kwa lugha nyingine vitanda tulivyonavyo hatoshi,” amesema Waziri Ummy Mwalimu.