Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo (kushoto) akimpa maelekezo Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda (kulia) juu ya namna ya kufanya baadhi ya marekebisho katika jengo la Ofisi za Baraza la Ardhi la Wilaya hiyo.
**********************************
Wananchi wa Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa, wametolewa hofu na Mkuu wa Mkoa huo Mh. Joachim Wangabo juu ya kufuata huduma za baraza la ardhi katika Wilaya ya Sumbwanga na kuwahakikishia kuwa, baraza la Ardhi la Wilaya ya Nkasi linategemewa kuanza kazi tarehe 1.7.2020 ili kuwapunguzia gharama wananchi wengi ambao walikuwa wakisafiri hadi kilometa 200 kufika Sumbawanga mjini.
Mh. Wangabo ameyasema hayo baada ya kutembelea jengo lililotengwa kwaajili ya ofisi za baraza hilo ambazo zipo karibu na Ofisi za Mkuu wa Wilaya hiyo pamoja na Jengo la mahakama ya mwanzo ya Wilaya na hivyo kuridhishwa na mazingira ya ofisi hizo.
“Katika Wilaya hii ya nkasi mtu anatoka Wampembe mpaka kufika Sumbwanga ni kama km 200, kutoka kule Kabwe halikadhalika hivyo hivyo ni kama km 200, na akifika kule ni lazima ale, alale, nauli na mambo mengine mengi, nap engine mgogoro wenyewe ni mdogo, anahangaika mpaka anakata tamaa, kwa hali hiyo hili baraza la ardhi la Wilaya ya Nkasi, litakuwa ni mkombozi mkubwa sana katika kusuluhisha migogoro mbalimbali na kumnusuru huyu mwananchi ambaye anakwenda mwendo mrefu sana kwenda kutafuta haki,” Alisema.
“Hili jengo lenyewe nina hakika ndani ya wiki moja litakuwa katika ubora, na tunaweza tukaanza kuanzia tarehe 1. Mwezi wa Saba, nataka hili baraza lianze na kwakuwa wizara imeshatukubalia yule Mwenyekiti wa baraza la Ardhi la Sumbawanga, tumeambiwa kuwa atakuwa anakuja angalau mara moja kwa mwezi na wakati huo wizara inajipanga ili iweze kuteua baraza la ardhi na nyumba kwaajili ya Wilaya ya Nkasi, kwasababu hiyo hatuna shaka migogoro hii inaweza kupatiwa ufumbuzi, kwasababu huduma itakuwa inatolewa hapa karibu,” Alieleza.
Jengo hilo lina Ofisi Nane pamoja na Ukumbi Mkubwa ambao unafaa kwaajili ya kusikiliza mashauri mbalilmbali ya migogoro ya ardhi, hali iliyopelekea Mh. Wangabo kuwasifu mkuu wa Wilaya ya Nkasi pamoja na Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya hiyo juu ya kulitoa jengo hilo kwaajili ya shughuli za baraza la ardhi.
Ili kukamilika kwa jengo hilo kunahitajika Shilingi milioni 2 kwaajili ya marekebisho madogo madogo pamoja na samani kadhaa zinazohitajika ili kuanza kwa ofisi hiyo na fedha hizo zitatolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi na kusimamiwa na mkuu wa Wilaya hiyo.