Naibu Katibu Mkuu akikagua kitabu cha kumbukumbu za Wagonjwa katika moja ya kituo cha Afya mkoani Manyara wakati wa Ziara yake ya kukagua shughuli za Afya katika shule na kwenye jamii.
Naibu Katibu Mkuu akizungumza na uongozi pamoja na wananchi mara baada yakukagua kituo hicho cha Afya kilicho pokea kiasi cha Mil.200 kwaajili ya ujenzi huo (Picha zote na OR-TAMISEMI)
Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, anayeshughulikia Afya, Dkt. Dorothy Gwajima akipata chakula na kuhakiki ubora wa chakula hicho,ambapo alionekana kukifurahia na kuupongeza uongozi wa shule kwa chakula kizuri.
Baadhi Wanafunzi wa kidato cha sita, mkoani Manyara wanaojiandaa na mitihani ya kuhitimu kidato cha sita inayotarajiwa kuanza Juni, 29, 2020 kama walivyokutwa wakati wa ziara ya Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI.
……………………………………………………………………….
Na. Atley Kuni –MANYARA
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais -TAMISEMI anayeshughukia Afya, Dkt. Dorothy Gwajima, amewasisitiza Maafisa Afya kote nchini kuhakikisha wanaimarisha ufuatiliaji wa uelimishaji na ukaguzi wa mazingira ya shuleni na kwenye Jamii wakiwa na wataalamu wa Sekta zingine kama Elimu ili kuimarisha afya za watanzania katika kila pahala.
Dkt. Gwajima amesema hayo akiwa na jopo la wataalamu wa Afya na Elimu walipofanya ziara ya kikazi yakutembelea na kukagua Shule za Sekondari zilizopokea wanafunzi wa kidato cha sita wanao tarajiwa kuanza mitihani yao yakuhitimu kuanzia Juni, 29, 2020 ambapo, katika ziara hiyo, Shule na Vituo vya afya vilivyofikiwa ni pamoja na Aldergate Sekondari, Babati Day Sekondari na Kituo cha Afya Mutuka, maeneo mengine ni Singe Sekondari, Bonga Sekondari pamoja na Hayatul Islamiya Sekondari.
Akiwa katika ziara hiyo, Dkt Gwajima aliridhishwa na hali ya usafi wa mazingira na huku akihoji wapi ambapo Maafisa Afya hawa huwa wanakwama katika kuendeleza ajenda ya usimamizi ili hali iwe kama ilivyo hizi siku zote?
Katika ziara hiyo, Dkt Gwajima ameshuhudia mazingira yakiwa safi na vifaa vya maji ya kunawa mikono na sabuni vikiwa kila sehemu huku vyoo na bafu vikiwa vinang’ara bila harufu yoyote kiasi cha kuweza hata kula chakula bila adha yoyote na usigundue kama hizo ni sehemu za kutunza uchafu, ameweza kushuhudia sehemu za kulala wanafunzi, darasani na wanapopata chakula (Bwaloni) kukiwa na mpangilio mzuri na kwa nafasi isiyopungua mita moja toka mwanafunzi mmoja hadi mwingine.
Hata hivyo, Dkt. Gwajima alibaini kuwa katika baadhi ya shule kunaweza kukawa na changamoto ya nafasi iwapo wanafunzi wataongezeka hivyo, ameagiza maafisa afya wafuatilie na kuhakikisha wamiliki wa shule hizo wanaanza maandalizi mapema ya maboresho ya mpangilio wa vitanda kwenye mabweni ili kuendelea kuepuka misongamano ya wanafunzi. Vilevile, ameelekeza kuhakikisha usafi ambao ameuona uwe uendelevu hata baada ya wanafunzi wote kurejea shuleni na kusiwe na visingizio vyote mara watoto wamekuwa wengi mara wengine wadogo kwani katika kipindi hicho ndiyo usafi huo unatakiwa kuwa bora zaidi.
Amewaelekeza Maafisa Afya kote nchini kuhakikisha ajenda ya usafi mashuleni na kwenye maeneo mengine ya jamii kuwa imara na endelevu daima ili kuimarisha zaidi udhibiti wa magonjwa ya mlipuko yatokanayo na uchafu wa mazingira na misongamano inayo epukika.
Amekumbusha kuwa, tabia ya uwepo wa misongamano ya vitanda mabwenini inahatarisha usalama wa watoto iwapo itatokea kuna dharura ya ajali na kutakiwa kujiokoa hivyo wamiliki wa shule waachane nayo mara moja na Maafisa Afya wafuatile kwa karibu na kujiridhisha hali ilivyo.
“Huu ni wakati wa kufanya mapinduzi makubwa katika utekelezaji wa ajenda ya Afya ya Usafi wa Mazingira kwa ujumla wake na kuendelea kudhibiti kila aina ya ugonjwa utokanao hali duni eneo hilo”. Amesema Dkt. Gwajima, na kuongeza, sasa hakuna sababu ya kushindwa kwani katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa Covid 19 chini ya uongozi wenye maono makubwa ya Kamanda wa Vita Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli Tanzania imeithibitishia Dunia kuwa tunaweza hivyo, hakuna kurudi nyuma kamwe bali kwenda mbele kutekeleza Sera na Miongozo ya Afya ya Mazingira.
Amesisitiza Maafisa Afya na Maafisa Elimu kuungana kwa pamoja katika kupunguza uhitaji wa raslimali kwa ajili ya utekelezaji endelevu mfano ni muhimu wawe na ratiba ya pamoja ya kwenda kufanya ufuatiliaji na uelimishaji kuhusu afya ya mazingira katika shule badala kila mmoja anabeba gari lake kwa ratiba yake na anafuatilia suala lile lile ambalo wote wangelifuatilia kwa pamoja kwa raslimali chache zaidi na kupata matokeo makubwa zaidi kwa muda mfupi na usiowachanganya wale wanaofanyiwa ufuatiliaji.
Dkt Gwajima ameagiza Maafisa Afya kote nchini ngazi ya Mkoa na Halmashauri kuwa na Mpangokazi na Ratiba ya Ufuatiliaji na Uelimishaji kuhusu Afya ya Usafi na Mazingira kwenye Shule na Jamii na taarifa iwe inawasilishwa kila mwezi na ioneshe wazi kuwa zoezi lilikuwa shirikishi
“Mganga Mkuu wa Mkoa na Afisa Elimu Mkoa hakikisheni mnapofanya Kaguzi za Afya ya Usafi na Mazingira kwa ushirikiano ili kuendelea kudumisha usafi unao oonekana sasa na kudhibiti magonjwa yote yanayotegemea usafi duni na kuwezesha kuokoa fedha iliyokuwa ikahudumie wahanga wa magonjwa hayo na kuielekeza kwenye shughuli zingine za maendeleo.
Kuhusu suala la msongamano wa vitanda mabwenini huku vingine vikiwa havitumiki amwewataka wasimamie kwani wanafunzi wanatakiwa kulala kwa nafasi na kupata hewa safi huku wakiwa na uhakika wa kujiokoa iwapo itatokea dharura. Hivyo, huku akikemea tabia ya kujaza vitanda na masanduku kwenye korido liishe mara moja na akaagiza atumiwe picha za hali halisi ilivyo mabwenini. Vilevile, simamieni wanafunzi hawa wafunge Vyandarua na kuvitumia siyo vyote viko masandukuni kwani Mbu wa Malaria naye ni adui ambaye bado yupo.
Kwa upande wake mtaalam wa Afya Mazingira kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. Selemani Yondu, alisema ugonjwa wa Corona umetufundisha kunawa mikono ili kujikinga lakini katika uhalisia sio maradhi haya tu bali pia tabia ya kunawa kwa maji tiririka na sabuni inatuepusha na maradhi mengine mengi kipindupindu na homa za matumbo na kuhara.
Naibu Katibu Mkuu akiwa katika Ziara hiyo alipotembelea kituo cha afya Mutuka, hakusita kuwapongeza wananchi wa Kijiji hicho waliojitolea nguvu zao pamoja na maeneo yao katika katika kuhakikisha ujenzi kituo cha kituo cha Afya unafanikiwa mara baada ya kupokea shilingi Mil. 200 kutoka serikalini ikiwa ni jitihada za Serikali kuwaondolea adha ya huduma za afya.
Amempongeza Mganga Mkuu wa Mji wa Babati kwa kuufahamu vema mradi huo jengo kwa jengo na chumba kwa chumba na kuwataka wataalamu wote kuiga mfano huo ili kuepusha gharama za marekebisho ya mara kutokana na mapungufu yanayoepukika.
Naibu Katibu Mkuu alikuwepo mkoani humo kufuatilia kwa karibu masuala mazima ya Afya na Usafi wa Mazingira katika Jamii pamoja na taasisi za umma na zile za watu binafsi kama zinatekeleza ajenda ya afya kwa ufasaha.