Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Umwangilia Bw.Daudi Kaali akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya sekta hiyo ndani ya mika mitano.
Baadhi ya watumishi pamoja na waandishi wa habari wakifatilia hotuba ya Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Umwangilia Bw.Daudi Kaali wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya sekta hiyo ndani ya mika mitano.
Mhandisi Daniel Manase kutoka kitengo cha ukaguzi na uthibiti ubora wa miradi ya umwagiliaji wa NIRC, akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya sekta hiyo ndani ya mika mitano jinsi mafanikio hayo yalivyochangia uzalishaji wa zao la Mpunga.
Kaimu Mkurugenzi wa usanifu na utafiti wa Tume hiyo, Mhandisi Gregory Chigwiye,akizungumzia mikakati ya tume kwa miaka mitano ijayo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dodoma.
………………………………………………………………………………………………
Na.Alex Sonna, Dodoma
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji(NIRC) kwa kipindi cha miaka mitano imefanikiwa kujenga na kukarabati Jumla ya skimu za umwagiliaji 179 ili kuongeza tija kwenye uzalishaji.
Hayo yameelezwa leo jijini na Mkurugenzi mkuu wa Tume hiyo Daudi Kaali wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya sekta ya uwagiliaji kwa miaka mitano.
Kaali amesema kuwa kutokana na ukarabati na ujenzi huo kumeongeza eneo linalomwagiliwa kutoka hekta 461,000 mwaka 2015 hadi hekta 694,715 mwaka 2020 sawa na ongezeko la asilimia 50.7.
Aidha Kaali ameeleza kuwa mradi wa kuendeleza wakulima wadogo(SSIDP) ambao ulitekelezwa katika awamu tatu kwenye Mikoa na Wilaya mbalimbali nchini kumechangia mafanikio hayo.
“Awamu ya kwanza utekelezaji wa mradi huu uligharimu Sh.Bilioni 15.37 na ulihusisha ujenzi na ukarabati wa skimu 48 za umwagiliaji zenye ukubwa wa hekta 13,722,”ameweka wazi Kaali
Kaali ameendelea kusema kuwa awamu ya pili ilihusisha skimu 61 zenye ukubwa wa hekta 22,312 uliogharimu Sh.Bilioni 20.1.
“Awamu ya tatu ya utekelezaji ilihusisha skimu 16 na kati ya hizo 9 zimekamilika na awamu hii inategemea kugharimu Sh.Bilioni 6.3 ambapo hekta 1090 zinategemewa kuongezeka,”ameeleza Kaali
Naye Mhandisi Daniel Manase kutoka kitengo cha ukaguzi na uthibiti ubora wa miradi ya umwagiliaji wa NIRC, amesema kuwa mafanikio hayo yamechangia uzalishaji wa zao la mpunga kuongezeka kutoka wastani wa tani 1.8- 2.0 kwa hekta hadi tani 4.0-5.0.
Manase ameeleza kuwa kwa zao la mahindi uzalishaji umeongezeka kutoka tani 1.5 hadi tani 3.7-5.0 kwa hekta, vitunguu pia uzalishaji umeongezeka kutoka tani 13 hadi 26 kwa hekta na nyanya kutoka tani 5 hadi 18 kwa hekta na hivyo sekta ya umwagiliaji kuchangia asilimia 24 ya mahitaji yote ya chakula nchini.
Kaimu Mkurugenzi wa usanifu na utafiti wa Tume hiyo, Gregory Chigwie, ameweka bayana kuwa Tume imejipanga kutekeleza miradi ya kimkakati kwa kujenga miundombinu mbalimbali ya umwagiliaji kwenye baadhi ya mabonde ya mito nchini.
Chigwie amesema kuwa wanatarajia kukusanya Sh.Milioni 300.4 kwa kipindi hicho kupitia vyanzo mbalimbali katika Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji.