Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dk. Venance Mwasse (kulia) na Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Wachimbaji Madini wa Katente, Michael Madata wakikabidhiana mikataba ya uendeshaji kituo cha mfano Katente baada ya kuusaini mkataba huo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dk. Venance Mwasse na Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Uchimbaji Madini Katente Michael Madata wakisaini makubaliano ya uendeshaji kituo cha mfano mbele ya wawakilishi kutoka Wizara ya Madini, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Bukombe, Ushirika Katente.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dk. Venance Mwasse na Mwenyekiti wa Kijiji cha Lwamgasa, Mussa Somgoma wakionesha makataba wa makubaliano ya uendeshaji kituo cha mfano mbele ya wawakilishi kutoka Wizara ya Madini, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Bukombe, Ushirika Katente.
………………………………………………………………………………………….
NA MWANDISHI WETU
KATIKA kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo wa madini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limesaini na kukabidhi mkataba wa makubaliano ya uendeshajiwa vituo vya mfano vya mafunzo katika eneo la Katente (Bukombe) na Lwamgasa (Geita).
Hatua hiyo ni mwendelezo wa jitihada za Shirika hilo kuwaendeleza wachimbaji wadogo nchini kwa kuwapatia mafunzo kwa vitendo ili kuboresha shughuli za uchimbaji madini nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kusaini mikataba ya makubaliano ya uendeshaji kati ya STAMICO, Chama cha ushirika cha wachimbaji madini cha Katente na Serikali ya kijiji cha Lwamgasa, Kaimu Mkurugezi Mtendaji wa STAMICO, Dk. Venance Mwasse alisema vituo hivyo ni chachu katika kuinua sekta ya madini nchini.
Alisema shirika hilo lilianzisha vituo hivyo ambavyo vinatumika kama viwanda vya mfano vya uchenjuaji dhahabu katika eneo la Katente (Bukombe) na Lwamgasa (Geita).
Alisema lengo la kuanzishwa kwa viwanda hivyo ni kuwapatia wachimbaji wadogo mafunzo kwa vitendo katika masuala ya uchimbaji wa madini ikiwa ni pamoja na utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini kupitia vikundi vyao vya ushirika.
“Vituo hivi vinatarajiwa kuleta manufaa yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuwapatia wachimbaji wadogo mafunzo ya namna bora ya kuendesha shughuli zao ili wafanye shughuli hizo kwa ufanisi na hatimaye kuongeza kipato chao mmoja mmoja na mapato ya Serikali kwa ujumla,” alisema.
Alisema mafunzo hayo yatakuwa chachu kwa wachimbaji wadogo kukua kibiashara na kuchangia pato la taifa.
“Kwa sababu mchango wa wachimbaji wadogo katika pato la taifa ni mdogo ilihali shughuli nyingi za uchimbaji zinafanywa na wachimbaji wadogo lakini wachimbaji wakubwa ndio ambao wanachangia zaidi katika ukuaji wa pato la taifa.
“Kwa hiyo mafunzo haya yatawasaidia kuongeza mapato yao na kutoa mchango stahiki kwa kulipa kodi zitokanazo na uchimbaji wa madini,” alisema.
Alisema hatua hizo zinaendana na malengo dhabiti ya Serikali ya Awamu katika kuhakikisha kuwa wachimbaji wadogo wanaondokana na uchimbaji usio na tija na kwenda kwenye uchimbaji utakaoongeza kiasi cha uzalishaji na baadaye kuongeza kipato kwa wachimbaji wadogo na taifa kwa ujumla.
Aidha, Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Wachimbaji Madini wa Katente, Michael Madata na Mwenyekiti wa Kijiji cha Lwamgasa, Mussa Somgoma kwa niaba ya wachimbaji wadogo walioko kwenye maeneo haya mawili waliishuruku Wizara ya Madini na STAMICO kwa kutekeleza kwa vitendo uanzishwaji wa vituo hivyo.
Walisema vituo hivyo vya mafunzo vimewaongezea uelewa kwenye uchimbaji wa madini tofauti na awali.
“Tukio hili la kusaini makubaliano ya uendashaji wa vituo vyote hivi viwili vya Katente na Lwamgasa kwa ajili ya kuanza uendeshaji wa vituo hivi, ni dira mpya kwetu wachimbaji wadogo na watanzania kwa ujumla,” alisema Madata.