Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Arusha Ladslaus Bamanyisa akimuonesha sehemu ya eneo la mradi wa Safari City-Arusha Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara ya kukagua miradi inayoendeshwa na NHC kwenye mkoa wa Arusha jana. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Arusha Gabriel Daqqaro.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na watumishi wa Shirika la Nyumba la Taifa pamoja na Watendaji wa sekta ya ardhi mkoa wa Arusha (hawapo pichani) wakati wa ziara ya kukagua miradi inayoendeshwa na NHC kwenye mkoa wa Arusha jana. Wa pili kulia ni Mkuu wa wilaya ya Arusha Gabriel Daqqaro na kushoto ni Meneja wa NHC Arusha Ladislaus Bamanyisa
Mkuu wa wilaya ya Arusha Gabriel Daqqaro akifafanua jambo mbele ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara ya kukagua miradi inayoendeshwa na NHC kwenye mkoa wa Arusha jana.
Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Arusha Ladislaus Bamanyisa akisoma taarifa ya Mradi wa Safari City mbele ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara ya kukagua miradi inayoendeshwa na NHC kwenye mkoa wa Arusha jana. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
…………………………………………………………………………….
Na Munir Shemweta, WANMM ARUSHA
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limebadilisha viwango vya bei za kuuzia viwanja vyake kwenye mradi wa Safari City mkoani Arusha kwa kutoa punguzo la asilimia 40% kwa viwanja vyote.
Hayo yamebainishwa jana na Meneja wa NHC mkoa wa Arusha Ladislaus Bamanyisa wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa Safari City kwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipotembelea mradi huo akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya NHC pamoja na uendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Arusha.
Bamanyisa alisema, uamuzi wa kubadilisha viwango vya bei za mauzo katika mradi huo kumesababishwa na kusuasua kwa mauzo ya viwanja katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2019 ambapo Shirika limeuza viwanja 6 tu kwa kile alichokieleza hali ngumu ya kiuchumi .
Kwa mujibu wa Meneja huyo wa NHC mkoa wa Arusha, viwango vipya vilivyopitishwa ni vile vya makazi ambapo sasa itakuwa Tsh 21,000 kwa kila mita ya mraba badala ya Tshs 35,000 na Tsh 27,000 badala ya Tshs 45,000/- kwa viwanja vya biashara.
Aliongeza kuwa, tangu kuzinduliwa mradi wa Safari City Juni 2016 shirika limeuza jumla ya viwanja 589 vyenye thamani ya shilingi 13,097,198,200/= na kukusanya shilingi 7,981,887,540/= sawa na asilimia 61% ya makusanyo kwa viwanja vilivyouzwa.
Hata hivyo, alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 NHC imeuza viwanja 122 vyenye thamani ya Tsh 2,058,113,600 na kukusanya Tshs 453,952,600/- na kubainisha kuwa viwanja vilivyobaki na kuendelea kuuzwa ni 1,252.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuongeza kasi katika kukamilisha mradi wa safari city kwa kuweka miundombinu ili kupata mafanikio kama ilivyo dhamaira ya Shirika.
Alisema, Shirika la Nyumba la Taifa linatakiwa kukahikisha eneo la mradi linakuwa na miundombiunu imara kama vile barabara, maji pamoja na umeme ili kuwavutia wateja wanaotaka kununua viwanja vya mradi.
‘’NHC inatakiwa kushughulikia miundombinu hapa, adha anayoipata mteja anayenunua kiwanja na kufika eneo lake ni ngumu na hasa mvua ikinyesha atafikaje? Inabidi ajifikirie mara mbili kununua eneo hilo‘’ alisema Dkt Mabula
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ukosefu wa miundombinu inachangia eneo la mradi wa Safari City kutopata wateja na kubainisha kuwa mawasiliano na watoa huduma yawe karibu ili mji uweze kupendeza.
Aidha, Dkt Mabula amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa NHC kuhakikisha pia inautangaza mradi wa Safari City kupitia vipindi vya televisheni na radio ili kuwawezesha wananchi kuutambua na kununua viwanja vya mradi huo na hivyo kuliingizia Shirika mapato.
Pia Naibu Waziri Mabula aliitaka NHC kufikiria utaratibu wa kuwakopesha watumishi wa umma viwanja vya mradi huo kwa njia ya kulipa kwa awamu tofauti na ilivyo sasa ambapo shirika limekuwa likiwafikiria zaidi wafanyabiashara.
Mradi wa Safari City wenye eneo la ukubwa wa ekari 587.03 lenye viwanja zaidi ya 2,141 ulianzishwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ili kusaidia uendelezaji na usimamizi madhubuti wa mpango kabambe wa jiji la Arusha kama ulivyoandaliwa, kusaidia kupunguza uhamiaji holela pamoja na kuwawezesha watu binafsi, kampuni na taasisi mbalimbali kupata maeneo yenye huduma muhimu za kijamii.