Prof Ndalichako ameyasema hayo leo wilayani Kondoa Mkoani Dodoma wakati alipofanya ziara ya kutembelea Chuo Cha Ualimu Bustani kwa ajili ya kukagua maendeleo yake na kuzungumza na wanafunzi wake.
Akizungumza baada ya kukagua miradi ya maendeleo chuoni hapo, Waziri Ndalichako amesema Serikali imetoa kipaumbele kwenye sekta ya elimu kwa kurabati, kujenga miundombinu ya taasisi zakei pamoja na kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia ili kuboresha dhana nzima ya ufundishaji na ujifunzaji.
Waziri Ndalichako amesema zaidi ya Sh Milioni 800 zimetumika kukarabati Chuo cha Ualimu Bustani kilichopo Halmashauri ya Mji Kondoa mkoani Dodoma.
Amesema ukarabati na ujenzi unaoendelea kwenye vyuo vya ualimu awamu ya kwanza imehusisha vyuo tisa, awamu ya pili vyuo nane na awamu ya tatu vyuo tisa na chuo cha Bustani kikiwemo na kufanya idadi ya vyuo vya ualimu vilivyokarabatiwa kufikia 25 kati ya Vyuo 35 vya Elimu nchini.
“Jana tumemsikia Rais Dk Joh Magufuli wakati akisoma utekelezaji wa serikali ya awamu ya tano kwa upande wa elimu makubwa yamefanyika nyie mmekuwa mashuhuda ikiwemo elimu bure ambapo kila mwezi zaidi ya shilingi bilioni 24 hutolewa.
Lakini pia uboreshaji wa miundombinu ya madarasa na mabweni katika vyuo na shule kongwe hata hapa kwenu mmeona ukarabati unaoendelea ambapo zaidi ya shilingi milioni 874 zimeletwa,” Amesema Prof. Ndalichako.
Aidha amewakumbusha kuwa uzalendo ni pamoja na kuyasema mazuri yanayofanywa na serikali ikiwemo ujenzi wa madaraja, umeme wa REA, ujenzi wa vituo vya afya pamoja na ujenzi wa barabara za lami na kuwataka kuacha kurubuniwa na wanaoisema vibaya serikali.
Kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu Prof Ndalichako amewataka wanafunzi hao kutokubali kutumika na wanasiasa na badala yake wapime yale yote wanayoambiwa na kuangalia kipi kilichofanyika katika kumchagua Kiongozi wanaemtaka.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Sezaria Makota ameishukuru serikali kwa namna ambavyo inapelekea miradi katika halmashauri ya Kondoa na hasa Chuo cha Ualimu Bustani na ujenzi wa ofisi za uthibiti Ubora wa Shule. Ameeleza miaka miwili iliyopita wizara ilipelekewa mradi wa maji ambao umekua msaada mkubwa kwenye chuo hiko.
Nae Mkuu wa Chuo cha ualimu Bustani Joina Chanafi amemueleza Waziri Ndalichako kuwa chuo hicho kina jumla ya watumishi wakufunzi 31 na kwamba hali ya itoaji elimu katika chuo hicho inaendelea vizuri bila changamoto yoyote.
Chanafi ameishukuru Serikali kwa kukarabati miundombinu ya chuo hicho ili kurejesha hadhi yake lakini pia kukiletea chuo kwa wakati fedha za uendeshaji ugharamiaji wa maji chakula na umeme.