*********************************
NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM ) Kibaha Mjini ,Pwani ,Maulid Bundala amewaasa baadhi ya wanachama wa CCM Kongowe na Kibaha kijumla kuachana na siasa za majungu na badala yake wajenge umoja ,upendo na mshikamano ili kukiimarisha chama.
Aidha amekemea kupitapita kwa baadhi ya watu wenye nia ya kugombea nafasi za udiwani na ubunge na kudai atakaebainika kupitapita kuanza kampeni kabla ya wakati atachukuliwa hatua .
Akipokea taarifa ya utekelezaji ya ilani kata ya Kongowe ,Maulid alisema wanachama wa CCM wapunguze majungu ,na kuacha kupaka matope viongozi wa kuchaguliwa ambao bado hawajamaliza kipindi chao cha uongozi.
Alisema ,uongozi sio nguo kila mtu atavaa ,bali anatakiwa mmoja hivyo wawe watulivu ,ili kila mwenye sifa aweze kujitokeza na kugombea kwa kufuata kanuni kwani kila mmoja ana haki ya kugombea .
Bundala ,alisisitiza kinachotakiwa kufuatwa ni kuwa na subira hadi muda utakapotangazwa hivyo ,watu waache kuwekeana chuki ,makundi na majungu ama kuchafuana kwa maslahi ya chama.
Aliwataka ,wanaCCM kufuata utaratibu uliopo ndani ya chama na kuwa kitu kimoja ,kukisemea chama kwa utekelezaji mkubwa uliofanyika miaka mitano ya awamu ya tano ili chama kishinde kwa kishindo ifikapo uchaguzi mkuu ujao .
Akiwasilisha taarifa yake ya utekelezaji diwani anayemaliza muda wake ,Iddi Kanyalu alishukuru wananchi, wanaCCM ,watendaji na viongozi mbalimbali kwa ushirikiano waliompa kipindi chake cha uongozi .
Alisema wakati anaingia madarakani miundombinu ya madarasa ilikuwa na changamoto na sasa anamaliza muda wake akiiacha sekta ya elimu ikiwa na madarasa ya kutosha ,madawati..
Akizungumzia sekta ya afya,Kanyalu alieleza kaondoa kero ya dawa na jengo Mwambisi lakini anaondoka kukiwa bado na changamoto ya ukosefu wa kituo cha afya.
“Nilipigania kupata kituo cha afya ,ila kutokana na mipango ya halmashauri na eneo tulilokuwa nalo kuwa dogo hatukufanikiwa ,naamini wakati ujao tutakuwa na kituo cha afya, pia nimesaidia ajira kwa vijana wa Kongowe kupitia viwanda vilivyopo ikiwemo TANCHOICE .”; aliongeza Kanyalu .
Kuhusu maji alibainisha,huduma hiyo imesambazwa maeneo ambayo yalikuwa yana shida ya maji Mwambisi,Miembesaba,Ungindoni,Bamba na Kongowe hivyo kwasasa shida ya maji ikiwa ni historia katika maeneo hayo.
Hata hivyo ,alifafanua anatarajia kugawa pikipiki moja kila tawi ili kupunguza changamoto ya usafiri .
Nae mwenyekiti wa CCM Kongowe ,Simon Mbelwa alikemea baadhi ya wanachama wa CCM katika kata hiyo kuweka makundi ,kufanya majungu na chuki na viongozi waliopo madarakani.
Mbelwa aliwataka kila mmoja ajitathmini ,kama anaweza kuongoza kata ya Kongowe muda ukifika achukue fomu, badala ya kukashifu wanaomaliza muda wao jambo ambalo ni kukatishana tamaa.