Bodi mpya ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VET Board) imedhamiria kuongeza nguvu katika kuboresha na kupanua wigo wa utoaji Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini.
Akizungumza wakati wa semina ya kutambulisha shughuli za VETA kwa wajumbe wapya wa bodi ya VETA tarehe 26 Mei, 2020, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bw. Peter Maduki, ambaye pia aliongoza Bodi iliyopita (2016 – 2019), amesema kuwa Bodi hiyo itahakikisha kuwa mafunzo ya ufundi stadi yanawafikia na kuwanufaisha wananchi wengi zaidi ili kuchangia katika kujenga uchumi wa nchi.
Alisema ana imani kuwa Bodi hiyo itatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa, hasa kwa kuwa Bodi hiyo imeundwa kwa kuzingatia ushirikishwaji wa wadau wote muhimu wa mafunzo ya ufundi stadi kama vile waajiri, waajiriwa, watoa mafunzo na watunga sera.
“Waajiri watatupa mrejesho wa jinsi wahitimu wa VETA wanavyofanya kazi na kutoa mwelekeo wa aina ya mafundi stadi wanaowahitaji kwa siku zijazo na hivyo kutusaidia kuandaa mafundi stadi watakaokidhi mahitaji ya waajiri hao”. Alisema
Amewasihi wajumbe hao wa Bodi kufanya kazi kwa bidii, umakini, weledi na kutumia talanta zao katika kuleta matokeo chanya zaidi kwenye elimu na mafunzo ya ufundi stadi.
Naye Mwenyekiti wa RAAWU Taifa, Dkt. Michael Mawondo, ambaye pia ni mjumbe wa bodi hiyo amesema kuwa Elimu ya Ufundi Stadi ni eneo muhimu sana katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kwani ndipo mahali inapozalishwa nguvukazi yenye ujuzi unaozingatia mahitaji halisi ya soko kwa kada hiyo. Alisisitiza kuwa mikakati zaidi inahitajika ili kuboresha utoaji wa mafunzo hayo.
Rais wa Chama cha Wenye Viwanda, Biashara na Kilimo Tanzania, TCCIA Bw. Paul Koyi, ambaye pia ni mjumbe wa Bodi hiyo, amesisitiza umuhimu wa VETA kuwekeza zaidi kwenye matumizi ya TEHAMA kwenye utoaji wa mafunzo ili kuwezesha wahitimu wa ufundi stadi kuendana na mazingira halisi ya mabadiliko ya teknolojia yanayoenda kwa kasi sana.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, amesema kuwa VETA inaendelea na jitihada mbalimbali za kupanua wigo wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili kuyafikia makundi mbalimbali katika jamii na kuongeza ajira kwa vijana, kuongeza tija katika viwanda na kuboresha uzalishaji mali na huduma katika jamii.
Dkt. Bujulu ameahidi kutoa ushirikiano kwa wajumbe wa Bodi hiyo na kusisitiza kuwa menejimenti ya VETA itafanyia kazi kwa umakini maelekezo yatakayotolewa na Bodi hiyo.
Bodi hiyo itahudumu kwa muda wa miaka mitatu (2020 – 2023) na wajumbe wake ni Bw. Peter Maduki (Mwenyekiti), Bw.Ally A. Msaki (Mkurugenzi wa Ajira, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Dkt. Ethel Kasembe (Naibu Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia), Dkt. Michael Mawondo (Mwenyekiti wa RAAWU Taifa), Padre Dkt. Francis Xavier Ng’atigwa (Mjumbe wa Baraza la Maaskofu Tanzania) na Bi. Clotilda Timothy Ndezi (Mkurugenzi wa Programu za Maendeleo na Uhamasishaji, Jumuiya Ya Kikristo Tanzania, CCT).
Wengine ni Bw. Nuhu Mruma (Katibu mkuu, BAKWATA), Bi. Anna Kimaro (Mtaalamu wa Sera za Mazingira ya Biashara, Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania, CTI), Bw. Paul Faraj Koyi (Rais wa Chama cha wenye Viwanda, Biashara na Kilimo Tanzania, TCCIA), Bi. Leah Ulaya (Rais wa Chama cha Walimu Tanzania, CWT) na Dkt. Pancras Bujulu (Mkurugenzi Mkuu wa VETA, ambaye ni Katibu wa Bodi).