Mwenyekiti chama cha waandishi wa Habari mkoa wa Simiyu, Bw. Frank Kasamwa (kulia) akipokea zawadi kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi wa champ hicho, Bibi. Victoria Katoyo iliyotolewa na wanachama kutambua utendaji kazi wake mzuri katika kipindi kilichopita kabla ya kufanyika uchaguzi jana Juni 12, 2020 mjini Bariadi
…………………………………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu Simiyu
CHAMA cha waandishi wa habari Mkoa wa Simiyu (SMPC) jana kimefanya uchaguzi mkuu wa viongozi wake, ambao watakiongoza kwa muda wa miaka mitano.
Uchaguzi huo ulishirikisha nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho, ikiwemo nafasi ya Mwenyekiti, Makamu mwenyekiti, Katibu mtendaji, Katibu mtendaji msaidizi, mhasibu, na wajumbe watano wa kamati tendaji.
Chama hicho chenye wanachama 15 ambao ni waandishi wa habari, kilifanya uchaguzi huo ambao ulikuwa huru na haki, ambapo ulimazika salama chini ya usimamizi wa mwenyekiti wa uchaguzi Victoria Katoyo.
Katika nafasi ya Mwenyekiti ambayo iliwaniwa na mtu mmoja Frank Kasamwa (alikuwa akitetea nafasi yake), wajumbe walichangua kwa mara ya pili mfululizo kwa kumpa kura zote 15 za ndiyo.
Nafasi ya Makamu Mwenyekiti iligombewa na mtu mmoja Paschal Michael (TBC), alichaguliwa kwa mara nyingine kwa kupata kura 14 za ndiyo huku kura moja ikimpigia hapana.
Msimamizi wa Uchaguzi huo Bibi Katoyo alimtangaza Happy Severine kuwa Katibu Mtendaji wa chama hicho baada ya kumshinda Samwel Mwanga aliyekuwa akitetea nafasi yake kwa kura 8 dhidi ya 7 alizopata Mwanga.
Nafasi ya Katibu Msaidizi Derick Milton alitangazwa kushinda nafasi hiyo baada ya kupata kura 9 dhidi ya Costantine Mathias aliyekuwa akitetea nafasi hiyo kwa kupata kura sita.
Anitha Balingilaki alichaguliwa kuwa Mhasibu/Mwekazina wa chama hicho kwa kupata kura 15 za ndiyo kutokana kugombea peke yake katika nafasi hiyo huku Shabani Lupimo na Aidan Mhando wakichaguliwa kuwa wajumbe wa kamati tendaji.
Mara baada ya uchaguzi Mwenyekiti wa uchaguzi Bibi Katoyo aliwataka viongozi wapya kuhakikisha wanajenga chama hicho kwa kuwaunganisha wanachama wote wanakuwa wamoja na kuieletea maendeleo SMPC.