…………………………………………………………………..
Ni furaha kubwa ndugu msomaji kukuletea fursa za uwekezaji zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Busega kwa lengo la kukuwezesha kuifahamu vyema wilaya ya Busega pamoja na kuzifahamu fursa hizo mbalimbali zilizopo katika wilaya hii, ambazo zinawezesha uwekezaji wa aina mbalimbali katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Halmashauri ya wilaya ya Busega imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi za asili ambazo hazijawekewa uwekezaji wa kutosha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa mitaji ya uwekezaji mkubwa na wa ngazi ya kati. Kwa hali hiyo kumesababisha uwekezaji katika Halmashauri yetu kuwa ni wa chini lakini pia kwa upande mwingine ufinyu wa uwekezaji umesababishwa na wawekezaji wengi kutokuwa na taarifa sahihi au kutokuwa na taarifa kabisa juu ya fursa zilizopo Halmashauri ya wilaya ya Busega. Uwekezaji ni moja ya njia madhubuti inayoweza kupunguza/kutokomeza umasikini na kufikia azma ya Tanzania kuwa kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025.
Halmashauri ya Wilaya ya Busega ni mojawapo ya halmashauri 6 zilizopo mkoa wa Simiyu ambapo mkoa huu una jumla ya wilaya 5. Halmashauri ya Wilaya ya Busega imeanzishwa mwaka 2013 ikiwa ina Tarafa 2, kata 15, vijiji 59 na vitongoji 362. Vyombo vya kiutendaji vinaendeshwa kupitia Halmashauri ya Wilaya ambayo ina jumla ya madiwani 21 ambapo madiwani 15 ni wa kuchaguliwa na madiwani 6 ni wa viti maalum.
Kijiografia wilaya ya Busega inapakana na wilaya ya Magu upande wa kusini, wilaya ya Bunda upande wa kaskazini, wilaya ya Bariadi upande wa mashariki na kwa upande wa magharibi imepakana na ziwa Viktoria. Wilaya ya Busega ina jumla ya ukubwa wa kilometa za mraba 2129, ambapo kilometa za mraba 1524 ni nchi kavu, na kilometa za mraba 605 ni maji, hivyo wilaya hii ni chachu ya fursa kubwa kwa wawekezaji kwa uwekezaji ikiwemo uwekezaji wa viwanda vikubwa na vidogo vya uzalishaji. Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, Busega ina jumla ya idadi ya watu 203,597.
Halmashauri ya Wilaya ya Busega imejaliwa kuwa na hali nzuri ya hewa kwa uwekezaji mbalimbali. Ustawi na rutuba nzuri ya udongo uliopo Busega hustawisha mazao ya aina mbalimbali ya biashara na chakula ikiwemo pamba, mpunga, choroko, dengu, mahindi, mtama, mihogo na viazi.
Mazingira rafiki pamoja na hali nzuri ya hewa inawezesha ustawi wa mifugo, hivyo kufanya ufugaji ni moja ya shughuli kubwa ya kiuchumi wilayani Busega. Mifugo aina mbalimbali inazalishwa na kufugwa ikiwemo ufugaji wa ng’ombe, mbuzi, kondoo na ufugaji wa kuku wa kienyeji.
Halmashauri ya Wilaya ya Busega imejaliwa kuwa na sehemu ya ziwa Viktoria yenye ukubwa wa kilometa za mraba 605 upande wa magharibi kutoka kata ya Kiloleli mpaka kata ya Lamadi iliyopo kaskazini mwa wilaya hii. Ziwa Viktoria ndilo ziwa linalounganisha mikoa mingi nchini Tanzania na kati ya Halmashauri 6 zinazounda mkoa wa Simiyu, Halmashauri ya Wilaya ya Busega ndiye pekee imepakana na Ziwa Viktoria; hivyo shughuli za uvuvi na usafiri wa majini ni miongoni mwa shughuli kubwa za kiuchumi wilayani Busega. Samaki aina ya Sato na Sangara na dagaa hupatikana kwa wingi wilayani Busega, pia shughuli ya Ufugaji wa Samaki kwa kutumia Vizimba (Fish Cage) huchangia uchumi wa maendeleo kwa wananchi wa Halmashuri ya wilaya ya Busega. Kwa upande mwingine ziwa linasaidia kwa kiasi kikubwa kilimo cha umwagiliaji hivyo kufanya shughuli za kilimo wilayani Busega kuwa ni za mwaka mzima ambapo kilimo hicho ni pendekezwa katika dunia ya sasa.
Halmashauri ya Wilaya ya Busega imejaliwa kuwa na pori la akiba la Kijereshi lenye ukubwa kilometa za mraba 65.72. Pori hili linapakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa Upande wa Kaskazini na Mashariki na jumla ya Vijiji sita Lukungu, Mwabayanda, Mwakiroba, Kijilishi, Nyamikoma na Senta kwa Upande wa Kusini na Magharibi. Wanyamapori kama vile Tembo, Nyati, Simba, Chui, Pundamilia, Nyumbu, Nyamera, Kuro, Ngiri, Nguruwe pori, Fisi, Bweha dhahabu, Bweha masikio, Swalapala, Swala tomi, Tohe, nyani,Tumbili, Sungura na wengine wengi wanapatikana kwenye pori la akiba Kijereshi.
Pori hili lipo karibu na Miji mikuu Mwanza (145km), Musoma (100km) na Bariadi (75Km), na Mji mdogo unaokaua kwa kasi wa Lamadi (3km) na hii inawezesha wageni wanaoitembelea mji huu, Kukidhi shauku yao ya kuona wanyamapori kwa muda mfupi wanaoweza kuutenga katikati ya ratiba zao na kuweza kupata mahitaji kama malazi na chakula kwa gharama nafuu.
Pori la akiba Kijereshi linaweza kufikika kwa usafiri wa anga kupitia Uwanja wa ndege wa Mwanza. Na pia Ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Kimataifa eneo la Igegu- Bariadi (The Proposed Serengeti International Airport) Kunafungua fursa ya kukuza utalii wa Kanda ya Ziwa kwa kupata wageni wa kimataifa moja kwa moja kutoka nchi zao na kuwawezesha watanzania kutoka mikoa mingine ya nchi, kutembelea Pori kwa muda/siku chache hivyo kupunguza gharama za matumizi. Pia Halmashauri ya Wilaya ya Busega imepakana na lango la kuingia Hifadhi ya Wanyama ya Taifa ya Serengeti iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwa upande wa kaskazini mwa wilaya; hivyo hupokea wageni wengi wa ndani na nje ya Tanzania kwaajili ya Utalii.
Juhudi ya kukabiliana na changamoto ya miundombinu ya mawasiliano na nishati ni kubwa ambapo kwa sasa ni kipaumbele katika Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Mawasiliano ya barabara katika wilaya ni mazuri na sehemu zote zinafikika kwa wepesi na kwa wakati hivyo kufanya muingiliano wa watu kuwa ni mkubwa. Muingiliano huo pia huchangiwa na uwepo wa barabara kuu ya Mwanza-Musoma. Kwa upande wa nishati, karibu vijiji vyote 59 vipo kwenye mpango wa umeme vijjini chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), huku huduma za mitandao ya mawasiliano ya simu zikiwa ni nzuri zinazotolewa na makampuni ya TTCL, Vodacom, Tigo, Airtel, Halotel na Zantel mengineyo.
Kwa ujumla fursa za uwekezaji wilayani Busega ni kubwa hivyo hakuna haja ya wawekezaji kusita kuja kuwekeza kwenye Halmashauri yetu. Hivyo tunawakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza wilayani Busega ili kwa pamoja kuweza kuinua uchumi na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii nchini. Wawekezaji wenye ndoto na maendeleo wanayo nafasi ya kuchagua sehemu sahihi ya kufikia ndoto za maendeleo hawana shaka kukaribia kufanya uwekezaji Halmashauri ya Wilaya ya Busega.
Unakaribishwa Halmashauri ya Wilaya ya Busega.