Mtaalam wa maabara ya Mpango wa Taifa wa Damu Salama kanda ya kusini Kassim Mmera akionesha mazao ya damu yaliyohifadhiwa kwenye friji zilizopo maabara hiyo
Mtaalamu wa Mishipa ya Damu wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Kanda ya Kusini, iliyopo Mtwara, Inocensia Chale akielezea jinsi wanavyotayarisha vifaa kwa ajili ya uchangiaji damu salama
Mkuu wa Maabara NBTS Kanda ya Kusini, Hamis Mohamed akifafanua jinsi wanavyotumia mfumo kulebo mazao ya damu
Wataalam wa maabara ya Mpango wa Taifa wa Damu Salama kanda ya kusini-Mtwara wakiwa kwenye picha ya pamoja ndani ya jengo la mpango huo.
*******************************
Na. WAMJW – Mtwara
Mpango wa Taifa wa damu Salama (NBTS), Kanda ya kusini, umefikia asilimia zaidi ya 94 ya ukusanyaji wa damu salama sawa na chupa 374 katika wiki ya kuadhimisha siku ya wachangia damu duniani.
Hayo yamesemwa leo na Meneja wa mpango wa Taifa wa Damu Salama Kanda ya Kusini iliyopo mtwara Dkt. Pendael Sifuel wakati akizungumza kuhusu wiki ya maadhimisho hayo ambayo duniani hufanyika Juni 14 kila mwaka.
“Kanda yetu tulikuwa na lengo la kukusanya chupa 400 kwa wiki mbili za uhamasishaji na tayari tumekusanya chupa 374 sawa na asilimia 94, hii ni kutokana na lengo la kukusanya chupa 45 hadi 50 kwa siku, hadi siku tano zilizobaki tutaweza kufikia malengo na hata kuvuka”. Amesema.
Dkt. Sifuel amesema kwamba kanda yake imeweka mkakati wa kukusanya damu kutoka vijijini kutokana na eneo la mikoa husika ni dogo na halina vyuo vingi hivyo wamepeleka elimu zaidi ya uchangiaji damu kwa wananchi waliopo vijijini.
“Tumewekeza sana vijijini kwani wanaopata huduma hiyo ni wananchi wenyewe na kama mnavyojua kanda yetu ina mikoa mitatu tu,hivyo kila anayefika kituo cha kutolea huduma za afya na kuongezewa damu anavyorudi nyumbani anaenda kuwa balozi hivyo atatoe elimu kwani mgonjwa hupewa damu bila kuleta ndugu kuchangia”.
Kwa upande wa utoaji wa majibu meneja huyo amesema kuwa maabara yake tangu mwaka jana wizara ya afya kuwapatiwa mashine za kisasa za uchunguzi wa sampuli za damu umewawezesha kutoa majibu ya damu kutoka siku tatu hadi siku moja.
“Kuna wakati tunapata dharura wa uhitaji wa damu salama kwa haraka kutoka kwenye halmashauri hivyo mashine hizi zinatuwezesha kutoa majibu ndani ya saa tatu tangu kupata taarifa ya dharura na kurudisha majibu haraka kama damu tuliyopokea ni salama au la”.
Dkt. Sifuel alisema mashine hizo za kisasa zina uwezo wa kupima sampuli zaidi ya 100 ndani ya saa moja na ina uwezo wa kupima magonjwa kama UKIMWI, Homa ya Ini B na C pamoja na Kaswende.Mpango wa Taifa wa Damu salama kanda ya kusini inahudumia mikoa mitatu ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.