****************************
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kuwaua majambazi wawili na kufanikiwa kukamata silaha bunduki moja iliyotengenezwa kienyeji inayotumia risasi za Shotgun.
Ni kwamba mnamo tarehe 09.06.2020 majira ya saa 19:15 Usiku huko eneo la Nzingwa, Mtaa wa Itumbi, Kata ya Matundasi, Tarafa ya Kiwanja katika Mji Mdogo wa Makongolosi, Wilaya ya Chunya, Majambazi wawili wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 35 – 40 waliuawa kwa kupigwa risasi wakiwa katika harakati za kwenda kufanya uhalifu nyumbani kwa MIHANGWA BUNDALA.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kupitia kikosi kazi chake cha kupambana na ujambazi lilipata taarifa kutoka kwa msiri na kufika mara moja eneo la Nzingwa katika Mji Mdogo wa Makongolosi kwa lengo la kuwakamata majambazi hao lakini baada ya kuwaona askari na kuamriwa kutii amri halali walikaidi na kuanza kupiga risasi kwa askari na ndipo askari wakajibu mapigo na kufanikiwa kuwajeruhi majambazi hao na walifariki wakipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Chunya kwa matibabu.
Aidha katika upekuzi, majambazi hao walikutwa na silaha na vitu mbalimbali ambavyo ni:-
- Bunduki moja iliyotengenezwa kienyeji inayotumia risasi za Shotgun.
- Risasi mbili za Shotgun
- Panga moja jipya lililonolewa kwa mashine.
- Kisu kimoja kilichonolewa kwa mashine.
- Pikipiki 308 CAD Kinglion rangi Nyekundu.
- Tochi mbili.
- Ramani ya tukio inayoonyesha namna ya kufika nyumbani kwa MIHANGWA BUNDALA aliyelengwa na majambazi hao.
- Kofia mbili Capelo na mifuko miwili @ Bob Marley na kipande cha sabuni.
Msako wa kuwatafuta watuhumiwa wengine wakiwemo watu wawili waliohusika kuwakodi majambazi hayo unaendelea.
KUINGIZA NCHINI BIDHAA ZILIZOPIGWA MARUFUKU.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia 1. ESTER MWASEBA [32] Mkazi wa Ilomba na 2. DOTO GEORGE [25] Mkazi wa Igawilo – Mbeya wakiwa na Pombe Kali zilizopigwa marufuku nchini aina ya ICE London Dry Gin chupa 140 kutoka nchi ya Malawi.
Watuhumiwa walikamatwa mnamo tarehe 06.06.2020 majira ya saa 14:00 Mchana huko katika kizuizi cha Kayuki kilichopo Kijiji na Kata ya Ilima, Tarafa ya Pakati, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya katika barabara ya Kyela – Tukuyu. Pombe hizi zimepigwa marufuku kwa sababu ya madhara ya kiafya kwa mtumiaji kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha kilevi [Alcohol 42%]. Taratibu za kiforodha zinafanyika.