Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde,akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa juu ya mwenendo wa mafanikio makubwa ya kupambana na kudhibiti utumiaji wa dawa za kulevye nchini,Kushoto kwake ni Kamishna wa kinga na tiba Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya Dk.Peter Mfisi.
Kamishna wa kinga na tiba Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya Dk.Peter Mfisi,akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dodoma wakati akitoa maelezo juu ya mwenendo wa mafanikio makubwa ya kupambana na kudhibiti utumiaji wa dawa za kulevye nchini
……………………………………………………………………………….
Na. Alex Sonna, Dodoma
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa Serikali kwa kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imepata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya hapa nchini kwa mwaka 2019.
Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dodoma wakati akziungumza na waandishi wa habari juu ya mwenendo wa mafanikio makubwa ya kupambana na kudhibiti utumiaji wa dawa za kulevye nchini.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya Duniani ya mwaka 2019 (Word Drug Report 2019), takribani watu milioni 271 ambao ni asilimia 5.5 ya watu wenye umri wa miaka 15 hadi 64 walitumia dawa za kulevya mwaka 2017.
Aidha Mhe.Mavunde amesema kuwa kwa kushirikiana na wadau wa nje na ndani ya nchi operesheni mbalimbali ndani ya nchi ikiwemo mipakani na katika ukanda wa Pwani na Bahari ya Hindi na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza uingizwaji wa dawa za kulevya nchini.
Mhe. Mavunde ameeleza kuwa kwa mwaka 2019, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilikamata jumla ya kilogramu 55.35 za heroin, kilo 10.34 za cocaine, tani 21.16 za bangi na tani 9.07 za mirungi ikiwahusisha watuhumiwa wapatao 10,384 ambao kesi zao ziko katika hatua mbalimbali mahakamani.
“Dawa za kulevya zinazokamatwa huteketezwa kwa mujibu wa sheria kwa kushirikisha Mamlaka mbalimbali za Serikali baada ya hukumu kutolewa, Mwaka 2019 tuliteketeza kilo 122.55 za heroin na kilo 71.507 za cocaine katika viwanda vya saruji Dar es Salaam na Mbeya” amebainisha Mhe. Mavunde.
Mhe. Mavunde ameongeza kuwa katika kukabiliana na madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevyaSerikali imeendelea kuimarisha huduma za tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya ambao hadi mwezi Desemba mwaka 2019 serikali imeanzisha vituo sita vya kutolea matibabu kwa waratibu wa dawa za kulevya kwa kutumia Methadone.
Vituo hivyo vilivyopo katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, na Dodoma vilikuwa vimesajiri waraibu wapatao 7,600.
Aidha Mhe. Mavunde amesema kuwa waathirika wa dawa za kulevya katika nyumba za upataji nafuu (Sober houses) ambapo waraibu wapatao 3,600 waliweza kuhudumiwa, hivyo kufanya idadi ya waraibu waliohudumiwa mwaka 2019 kufikia zaidi ya 11,100.
Pia Mhe. Mavunde ameainisha kuwa matumizi ya dawa za kulevya kwa wajawazito husababisha athari kwa watoto wao na wanapojifungua na huathiri familia zao kwa kiwango kikubwa zaidi kwa kushindwa kuwapa malezi bora watoto wao.
“Hali hii inatengeneza vizazi vya waraibu wa dawa za kulevya hivyo wanawake walioathirika na dawa za kulevya kujitokeza ili wapatiwe matibabu katika vituo vilivyoanzishwa na Serikali” amesema Mhe. Mavunde.
Mhe. Mavunde ametoa wito kwa jamii kuendelea kujitokeza pale ambapo kuna utoaji wa Elimu juu ya dawa za kulevya inapotolewa katika maeneo yao kwa kupitia njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari, matukio ya kitaifa, semina, makongamano na mitandao ya kijamii. Utoaji wa elimu ni mkakati muhimu wa kupunguza matumizi haramu ya dawa za kulevya kwa makundi tofauti ya rika.
Kwa upande wa Kamishna wa kinga na tiba Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya Dk.Peter Mfisi,amesema kuwa wanawake wanaotumia vilevi wanavitumia kwa haraka zaidi kuliko wanaume na kuweza hupata uraibu wa madhara mengine kuliko wanaume.
Hata hivyo Dk.Mfisi amesema kuwa ipo sheria ambayo inampa mamlaka Kamishna anaweza kuruhusu kilimo cha bangi au koki kwa ajili ya matumzi ya kisayansi kama tafiti au matumizi ya kutengenezea dawa.
”Zipo njia ambazo lazima zifuatwe ili mtu aweze kupatiwa kibali kutoka wizara ya kilimo na wizara ya mambo ya ndani ya nchi na ijiridhishe kuwa mtu au mwananchi akilima zao la bangi atatumia kwa ajili ya kutengenezea dawa na si kitu chochote”amesisitiza Dk.Mfisi