Home Mchanganyiko HUKUMU 18 ZATOLEWA KUHUSU MASHAURI YA KIJINSI

HUKUMU 18 ZATOLEWA KUHUSU MASHAURI YA KIJINSI

0

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama  ya Wilaya ya Chato, Mhe. Odira  Amworo akizungumzia kuhusu uboreshajji wa miundombinu ulivyorahisha utoaji wa haki kwa wakazi wa wilaya hiyo.

Mlinzi wa Mahakama hiyo, Tabitha Andrew akielezea jinsi anavyoifanya kazi ya TEHAMA mahakamani hapo.

Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Chato.

…………………………………………………………………………………

Na Magreth Kinabo na Innocent Kansha- Mahakama, Chato

Mahakama ya Wilaya ya Chato imefanikiwa kutoa   zaidi ya 18 zinazotokana na makosa ya ukatili  na unyanyasaji wa kijinsia baada ya jamii kuwa na uelewa juu ya suala hilo na kuweka mikakati ya kutatua changamoto hiyo.

Akizungumza na Maofisa Habari wa Mahakama ya Tanzania, Juni 9, mwaka huu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Odira  Amworo amesema  mashauri yanayoongoza kusikilizwa mahakamani hapo ni vitendo vya ukatili wa kijinsia huku akitolea mfano ubakaji na wanafunzi kupata ujauzito.

Alisema Mahakama hiyo, imekuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto hiyo, ambapo imeshatoa maamuzi mbalimbali.

‘‘Ongezeko la mashauri haya mahakamani hapa limetokana na mwamko wa jamii kuwa na uelewa wa masuala ya ukatili  na unyanyasaji wa kijinsia   baada ya kutolewa kwa elimu juu ya masuala haya, ambayo tuliitoa wakati wa maadhimisho ya Wiki ya  Sheria iliyotolewa mashuleni, ambapo tuliwaelimisha watoto wa kike wanapofanyiwa vitendo hivi watoe taarifa kwa wazazi na  kituo cha polisi,’’ alisema Mhe. Amworo.

Aliongeza kwamba mahakama hiyo imetoa hukumu tatu za kifungo cha maisha jela na hukumu zaidi ya 15 za kifungo cha miaka 30 jela zilizotokana na makosa ya ubakaji ili kutoa fundisho kwa watu wengine. Hivyo aliwataka watoto wa kike wasikubali kurubuniwa kushiriki katika vitendo vya ngono, bali wakijite katika masomo.Alisema takwimu hizo ni za tangu  baada  ya uzinduzi uliofanyika  mwaka jana hadi Juni mwaka huu.

Hakimu huyo alifafanua kuwa vitendo hivyo vinatokana na kuvunjika kwa baadhi ya ndoa, hivyo Mama anapobaki na mtoto wa kike chini ya umri wa miaka 10 baba wa kambo humwingilia kimwili.

Aliyataja mashauri mengine yanayosikilizwa na Mahakama hiyo kuwa ni makosa ya uvuvi haramu,kuvamia hifadhi za taifa kinyume cha sheria na kukutwa na dawa za kulevya.

Akizungumzia kuhusu ujenzi wa Mahakama hiyo ya kisasa, alisema umesaidia  kutatua tatizo la  utunzaji wa nyaraka kiholela , kuwa kuwa sasa linafanywa kwa ufanisi na hakuna tena malalamiko ya upotevu wa nyaraka, ukilinganisha na lile jengo la zamani la Mahakama ya Mwanzo  Chato Mjini ambalo mara kwa mara kulikuwa na upotevu wa nyaraka mbalimbali.

‘‘Hivi sasa tuna jengo maalumu la utunzaji nyaraka mbalimbali, ambapo zinatunzwa  vizuri kwa utaratibu uliopangwa,’’ alisititiza.

Hakimu huyo alisema walikuwa na mlundikano wa mashauri 50, kwa sababu ya kutokuwa  kuwa na mahakimu wa kutosha, lakini  sasa yamebaki mashauri matano baada ya kuongezewa Mahakimu kutoka  watatu hadi tisa. Hivyo mashaurihayo yanaweza kumalizika ndani ya  mwezi au wiki tatu. Iipokuwa yale makosa mauaji, kubaka, na kosa kumpatia ujauzito mwanafunzi ambayo upelelezi wake huchukua muda mrefu.

Kwa upande wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wamefanikiwa kuuhisha mashauri katika Mfumo wa Kuratibu na Kusajili Mashauri kwa njia ya Kielektroniki  (JSDS 11) tangu mwaka 2013 hadi sasa mashari 1, 348 ya madai na jinai. Kati ya mashauri hayo 169 ni hai.

Pia  mashauri yaliyofunguliwa kuanzia  mwezi Januari  hadi sasa ni 234, yaliyotolewa maamuzi ni mashauri 259. Mashauri yaliyofunguliwa kwa njia ya mtandao ni sita, lakini mawili yalikataliwa.

Tunamtumia mlinzi na mhudumu wa ofisi kuhuhisha takwimu kwa njia TEHAMA baada ya kuwapatia mafunzo na kufungua mashauri kwa njia ya mtandao.

Alitoa wito kwa jamii kutotumia nguvu ya umma kutafuta haki zao na kujichukulia sheria mkononi badala yake waitumie miundombinu ya kisasa ya Mahakama hiyo ili kuwezesha migogoro yao kutatuliwa wakati, weledi na haki.

Naye Mlinzi wa Mahakama hiyo, Tabitha Andrew alisema anaifanya kazi hiyo baada ya kupatiwa mafunzo ya siku moja kutoka kwa wataalamu wa  TEHAMA kutoka Makao Makuu.

‘‘Nimefanikiwa kuifanya kazi hii kwa kuwa ninapata ushirikino wa kutosha kutka kwa watumishi wenzangu.  Nina matarajio ya kujifunza zaidi katika eneo hili ili niweze kufikia kiwango cha juu na kuisaidia taifa la Tanzania,’’ alisema  Andrew ambaye ni mwajiriwa mpya kuanzia Novemba Mosi mwaka huu.

Kwa upande wake Afisa Tawala  wa Mahakama ya Wilaya ya Chato, Bw.  Faulent Kiowi  alielezea kwamba  baada ya kuanza kufanya kazi kwenye jengo jipya wamefanikiwa kujenga imani kwa wananchi na ifikapo muda wa  saa 7.00 mchana wanakuwa wameshahudumiwa ilinwaweze kuendelea shughuli nyingine. Pia tatizo la kuhairisha mashauri marakwa mara halipo kwa sababu ana chumba chake cha kufanyiakazi na vitendea kazi.

Afisa Tawala wa Wilaya ya Chato Bw. Masumbuko Sobilwe,  alisema awali wakazi wa wilaya hiyo walikuwa wakipata huduma za kimahakama kwenye Wilaya ya Biharamulo, ambapo umbali wake ni  zaidi ya kilomita  70.

‘‘Hivi sasa wananchi wanafurahia  kupatiwa huduma za Mahakama karibu na haki inatolewa kwa wakati. Pia kiwango cha malalamiko kimepungua, kwa kuwa zamani walikuwa wanalalamikia kutozwa tozo za kuwapeleka ndugu za mahakamani, lakini suala hili sasa halipo,’’ alisema Sobilwe. Huku akishukuru Serikali kwa kuwapatia huduma hiyo karibu.

Mahakama hiyo kwa mwaka hupokea wastani wa mashauri 400 kwa siku na ina hudumia wa watu 1600 kwa mwaka.