Diwani wa kata ya Mwangata Nguvu Chengula akizungumza na wanahabari.(picha na Denis Mlowe)
………………………………………………………………………………..
NA DENIS MLOWE, IRINGA
DIWANI wa Kata ya Mwangata iliyoko Manispaa ya Iringa,Nguvu Chengula ameapa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Rais John Pombe Magufuri anashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa 2020 unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
Akizungumza na wanahabari kwenye ukumbi wa Boma, Chengula alisema kuwa atatumia jitihada zote pamoja na Mali anazomiliki kuhakikisha CCM inashinda chini ya Rais Magufuli kwa kutoa magari ya kampeni na vipaza sauti katika kuhakikisha anarudi madarakani.
Alisema kuwa kazi ambazo zimekwisha fanywa na Rais hadi sasa zimemfanya atangaze Rais Magufuli ndio mtu pekee ambaye anafata nyendo zake katika suala zima la uongozi.
Chengula ambaye ni mmiliki wa shule za Sun Academy zilizoko Manispaa ya Iringa alisema kuwa tangu rais Magufuli aingie madarakani amefinikisha mambo mengi ikiwemo vijiji 3559 kupata umeme Jambo ambalo lilikuwa ni ndoto na vijiji 4314 vinaendelea kupata nishati hiyo katika awamu ya pili.
Alisema Rais Magufuli kwa kipindi Cha miaka 5 amefanikiwa kufanikisha ujenzi wa vituo vya afya na zahanati zaidi ya 1000 hospitali 25 kitu ambacho kilishilindikana katika awamu nyingine.
Aliongeza kuwa katika suala la maji zaidi ya miradi 1571 imekamilika na vituo vya maji 126610 vimejengwa na kuweza kuhudumia watu milioni 31.65 kwa ajili ya watu wa vijijini.
Aliendelea kumsifu Rais Magufuli kwa kuwezesha wananchi wanaendelea kunufaika na mikopi isiyo na riba toka halmashauri zote nchini Jambo lililopewa msukumo mkubwa na na kuhakikisha kwamba tozo za mazao zimeondolewa hivyo kuwapa nafasi wakulima kuinua vipato vyao.
Akizungumzia miundo mbinu alisema kuwa serikali ya Magufuli imefanikiwa kuboresha Barabara ambapo zimejengwa kwa asilimia 98 kuunganisha mikoa yote nchini.
Aliongeza kuwa katika suala la elimu serikali imefanikisha kutolewa kwa bilioni 24.4 kila mwezi kwa shule za sekondari na msingi na kuongeza shule za msingi kutoka 16,899 mwaka 2015 Hadi 17,804 mwaka 2020 na sekondari toka 4708 Hadi 5330 mwaka 2020.
Aidha akizungumza kuhusu kata anayoongoza aliwashukuru wananchi kwa kumchagua na kusema kuwa amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuhakikisha anatimiza ahadi alizoahidi walipomchagua 2108.
Alisema kuwa amehakikisha Barabara za kata hiyo zinapitika ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii kufanyika na kujenga Barabara ya lami toka Zizi la Ng’ombe Hadi Ngelewala yenye km 1.4 kwa thamani ya sh. Milioni 600,000,000.
Aidha alifanikiwa kufanikisha uchimbaji wa mtaro wa maji mtaa wa Mwangata C kwa gharama ya sh.milioni 3.5 aidha kujenga chumba Cha darasa kwenye shule ya sekondari Mawelewele.