Home Mchanganyiko MHE. MAVUNDE AITAKA NSSF KUCHUKUA HATUA ZA KISHERIA  KWA WAAJIRI WASIOWASILISHA MICHANGO...

MHE. MAVUNDE AITAKA NSSF KUCHUKUA HATUA ZA KISHERIA  KWA WAAJIRI WASIOWASILISHA MICHANGO YA WAFANYAKAZI WAO

0

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde (wa kwanza kushoto) akiongoza kikao baina ya Menejimenti ya NSSF na uongozi wa Knight Support.

Kaimu Mkurugenzi wa Sheria wa NSSF, Bw. Suleiman Msangi (aliyesimama), akimuonyesha Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira
Mhe. Anthony Mavunde, taarifa ya kuchelewa kuleta michango kwa Kampuni ya Night Support.

Mhasibu wa Kampuni ya Ulinzi ya Knight Support (mwenye shati nyeupe aliyekaa) pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Bresing Kachambwa (aliyekaa kushoto) wakiwa chini ya Ulinzi wa Polisi, kabla ya kuchukuliwa na kupelekwa Kituo cha Polisi

Mkurugenzi wa Kampuni ya Ulinzi wa Knight Support (wa kwanza kulia), Bresing Kachambwa na Wahasibu wa kampuni hiyo wakiwa kwenye gari ya Polisi, Makao Makuu ya NSSF baada ya kukamatwa kutokana na kushindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wa kampuni hiyo inayofikia Tzs. bilioni 8.417.

………………………………………………………………………………………….

Na. Majid Abdulkarim, Dodoma

Serikali imeelekeza orodha ya wadaiwa sugu na waajiri wote wasiowasilisha michango ya wafanyakazi wao kuchukuliwa  hatua za kisheria na wahusika kufikishwa mahakamani mara moja.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde wakati wa kikao baina ya Menejimenti ya NSSF, Kampuni ya Knight Support na Wafanyakazi wa Knight Support juu ya mustakabali wa malimbikizo ya wasilisho la michango ya wafanyakazi pamoja na tozo ya adhabu inayofikia takribani Tsh 8.4Bn ikiwa ni michango ya kuanzia mwaka 2011-2018.

Akizungumza Mhe.Mavunde ametoa rai kwa waajiri wote nchini ambao hawawasilishi michango  ya wafanyakazi wao kujisalimisha mapema  NSSF kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mhe. Mavunde amesema kuwa NSSF ifanye mawasiliano  na Wizara ya Mambo ya Nje juu ya kurejeshwa nchini mmiliki wa Kampuni ya Knight Support Raia wa Uingereza Bi. Christine Sutton.

Aidha Mhe. Mavunde amesema kuwa Mwakilishi wa Kampuni hapa nchini Bw.Blessing Kachambwa raia wa Zimbabwe azuiwe kutoka Nchini mpaka hapo wahusika wakuu wa Kampuni watakaposhughulikia malipo ya malimbikizo ya michango ya wafanyakazi.

Mhe. Mavunde ameeleza kuwa NSSF imeshinda kesi mahakamani juu ya deni hilo tajwa hapo juu na imethibitika kwamba Kampuni ya Knight Support haina mali za kukamata kuuzwa na kufidia deni hilo.

“Kurugenzi ya Sheria NSSF iandae nyaraka za kisheria za maombi ya kuwakamata wahusika wakuu na kuwafanya wafunguliwe  madai (Civil Prisoners)”, ameelekeza Mhe. Mavunde.

Pia ameongeza kuwa Mhe. Mavunde ameelekeza kufanyika Uchunguzi wa kina ufanyike kubaini wafanyakazi wa NSSF ambao hawakutimiza wajibu wao kwa kutofuatilia michango tangu mwaka 2011-2018.