Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Mh. Mussa Zungu (Kulia) akiambatana na Meya wa Manispaa ya Ilala Omari Kumbilamoto (wa pili kushoto) askari wa Ulinzi na viongozi wa ngazi mbalimbali za kiserikali alipofanya ziara katika eneo la machinjio ya Vingunguti. Picha na Charles Kombe.
Waziriwa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Mh. Mussa Zungu akiwaonyesha wanahabari (Hawapo pichani) bomba la Gesi ya Songas liloangukiwa na mawe kutokana na athari za uchimbaji mchanga katika eneo hilo. Picha Charles Kombe
……………………………………………………………………………………………
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira )Mhe. Mussa Azzan Zungu amefanya Ziara katika eneo la Machinjio ya Vingunguti pamoja na eneo la mtaa wa Songas lililopo Kinyerezi Jijini Dar es Salaam, yenye lengo la ukaguzi wa Mazingira katika maeneo hayo.
Katika Mradi wa Machinjio ya Kinyerezi Mhe. Zungu akiambatana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Jumanne Shauri, Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC Prof. Esnat Chaggu na viongozi mbalimbali wa Serikali amesema kuwa ziara yake imelenga kujiridhisha juu ya uwepo wa mazingira salama ikiwemo miundombinu ya maji taka.
“Tumejiridhisha na miundombinu ambayo imewekwa na wataalamu na wajenzi wa National Housing kwenye mradi huu. Pale ambapo kutakua na mapungufu tutashirikiana nao kwa kuwa tuna wataalamu, watakuwa wanatoa ushauri kuhakikisha kuwa maji yanaingia katika chemba tatu, yatatoka ya kwanza hadi ya tatu na yatakuwa safi na yataelekezwa katika mto Msimbazi.” Amesema Mhe.Zungu
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Jumanne Shauri amemshukuru Mhe. Zungu kwa kutembelea machinjio hayo na kuahidi kuendelea kuhakikisha yale yote aliyoyaagiza yanatekelezwa.
“Huu ni mradi mkubwa wa machinjio ya kisasa Tanzania na pengine Afrika na utakuza uchumi kwa kiwango kikubwa kwa Manispaa ya Ilala.Tukushukuru sana Mheshimiwa kwa kutembelea hapa na tunaahidi kuendelea kusimamia mazingira mazuri ya mchinjio haya.” Amesema Shauri
Katika Zira ya pili mtaa wa Songas eneo la Kinyerezi palipopita bomba la Gesi ya Songas linaloharibiwa na uchimbaji wa mchanga, Mhe. Zungu ametoa maelekezo kwa uongozi wa mtaa huo kupitia kamati za ulinzi kuwabaini wahusika wa uharibifu huo.
“Uchafuzi wa eneo hili ni kuharibu uchumi wa nchi na vilevile ni hatari kwa wakazi. Tani za mawe karibu tani saba zimeangukia kwenye bomba la gesi. Watoto, kina mama na wazee wanaweza kuathirika likitokea janga la moto kwenye eneo hili. Leo nitampa taarifa mkurugenzi Mkuu wa TPDC alete wataalamu wake ili kunusuru eneo hili.” Amesema Mhe. Zungu
Nae mwenyekiti wa Bodi ya NEMC Prof. Esnat Chaggu ametoa onyo kwa wananchi wote wanaoendelea na uchimbaji mchanga katika eneo hilo kuacha tabia hio kabla hatua kali za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.
“Sheria ya Mazingira ipo na itachukua mkondo wake na itaangalia kwamba hao watu wataweza kuchukuliwa hatua za namna gani. Kwahiyo ni jambo ambalo tunaomba lisimame mara moja. Mchanga uchimbwe katika maeneo mengine ambayo yameshatolewa vibali sahihi lakini hasara hii ni kubwa na si vyema iendelee.” Amesema Prof. Chaggu
Hatahivyo hii ni ziara ya tatu katika wiki hii ambazo ameendelea kuzifanya Mhe. Zungu zikiwa na lengo la kutatua changamoto mbalimbali za kimazingira zinazosababishwa na binadamu pamoja na miondombinu ya maji taka katika maeneo mbalimbali hapa nchini.