*****************************
Na.Alex Sonna,Dodoma
Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma Girres Muroto amethibitisha kushambuliwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema na kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni Freeman Mbowe usiku wa kuamkia leo nyumbani kwake jijini Dodoma.
Kamanda Muroto ameyasema leo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma amesema kuwa taarifa za tukio wamezipata majira ya saa moja asubuhi wakati tukio limetokea usiku wa saa sita.
“Asubuhi ya leo nimepokea taarifa kutoka kwa dereva wa Mbowe Wilhard Urasa kwamba wakati Mbowe alikuwa anatoka eneo la Medeli kuelekea nyumbani kwake Area D ,baada ya kushushwa kwenye gari wakati anapandisha kwenye ngazi kuelekea nyumbani kwake,alikutana na watu watatu ambao hakuwafahamu kwa sura wala kwa majina , walimkanyaga kwa mateke sehemu mbalimbali za mwili wake.”
Muroto amesema kuwa baada ya tukio hilo Mhe.Mbowe alichukuliwa na kupelekwa hospitali ya Ntyuka jijini Dodoma ambako anaendelea na matibabu.
Kamanda Muroto amesema,jeshi la polisi linafanya uchunguzi wa kina na kwamba hakuna kitu kitakachoachwa katika tukio hilo
Aidha ameonya kwamba tukio hilo lisitumike kisiasa kwa watu ama chama kujitafutia umaarufu.
” Bado tunafanya uchunguzi kujua undani wa tukio maana eneo lile lina walinzi na majirani,hivyo watahojiwa ili kujua ukweli.”amesema Muroto.
Ametumia nafasi hiyo kuwaonya wanasiasa wanaopanga kufanya mikusanyiko isiyo halali huku akisema kwa watakaofanya hivyo sheria itachukua mkondo wake.
“Tunaona kwenye mitandao ya kijamii kwamba kuna baadhi ya watu wamepanga kukusanyika kwenye chama cha chadema, jeshi la polisi lipo macho na yeyote atakayekusanyika kichochezi atashughulikiwa.” Amesisitiza na kuongeza.
“Natoa onto kwa watu wanaotaka kutumia tukio hili kama mtaji wa kisiasa,mitandao ya kijamii isitumike vibaya kueneza uongo ,kwani wapo wwnaojiandaa kutumia tukio hili kufanya machafuko,nawaonya waache Mara moja na wasiingilie kupotosha uchunguzi a jeshi la polisi unaendelea ili ufalifanye kazi yake.”
Kwa upande wake Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Ester Bulaya amesema,uongozi wa Chadema unapanga kumhamishia jijini Dar es salaam kwa matibabu zaidi na kwa ajili ya usalama zaidi.