Home Mchanganyiko MAHAKAMA ZA MWANZO GEITA ZASIKILIZA MASHAURI NDANI YA MIEZI MINNE

MAHAKAMA ZA MWANZO GEITA ZASIKILIZA MASHAURI NDANI YA MIEZI MINNE

0

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bukombe, Mhe.  Ainawe Moshi , akizungumzia  maboresho ya mahakama hiyo.  

Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Bukombe  

********************************

Na Magreth Kinabo na Innocent  Kansha –  Bukombe

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bukombe, Mhe.  Ainawe Moshi amesema  kwamba  Mahakama  za Mwanzo  katika   Mkoa wa Geita zimejipanga kumaliza mashauri ndani ya kipindi cha miezi minne, licha ya utaratibu uliopangwa wa miezi sita.

 Akizungumza na waandishi wa habari kutoka Mahakama  ya Tanzania, jana (8.06.20) kwenye ofisi ya Mahakama hiyo, wilayani Bukombe,  Hakimu huyo alisema  mahakama hizo zimejipangia utaratibu huo  licha ya kuwepo kwa muda maalumu wa kusikiliza shauri, ili kuwawezesha wananchi   kupata fursa ya kutosha ya kuendelea  kushiriki  katika shughuli za  kiuchumi na kijamii.

‘‘Napenda kuwaambia wananchi   na wadau wetu kuwa  Mahakama  ya Tanzania imeboresha miundombinu, hivyo sisi tumejipanga kumaliza mashauri kwa wakati tofauti na zamani  ambapo watu  walikuwa wanafahamu shauri linaweza kukaa  miaka miwili hadi saba mahakamani . Lakini kwa sasa hivi Mahakama inaenda na wakati hakuna shauri la Mahakama ya Wilaya linalokaa zaidi ya miezi 12, pia kwa Mahakama za Mwanzo tumejipanga kumaliza shauri ndani ya miezi minne,’’ alisema Moshi.

Aliongeza kuwa wananchi  wasiogope kufikisha mashauri yao mahakamani, bali wafike kwenye eneo hilo na watapata haki zao bila upendeleo  kwa wakati.

Kwa upande wake Afisa Tawala  wa Mahakama ya Wilaya, Bukombe, Bw.Sauwael  Urio alisema  kutokana na maboresho yaliyofanyika hivi sasa wanatoa nakala za hukumu ndani ya siku 21. Hivyo  hali hiyo imetokana kuwepo kwa mazingira wezeshi ya vitendea kazi na watumishi wa kutosha.

Alisema mahakama hiyo inapokea wastani wa  mashauri 600 kwa mwaka na kuhudumia takribani  wananchi 200,000  wanaotoka kwenye wilaya hiyo na Wilaya ya Mbogwe. 

 Aliongeza uwajibikaji na hamasa ya utendaji kazi  imeongezeka kwa kuwa  hakuna tatizo la baadhi ya watumishi kukosa nafasi ya kufanya kazi  na vitendea kazi hivi sasa halipo.

Naye Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Ushirombo, Mhe.  Damas  Gakwaya alisema  wanafanikiwa kusikiliza mashauri ngazi za mahakama hiyo kwa kipindi cha miezi miezi minne kwa  sababu  wanayapokea tayari yakiwa na shahidi uliokamilika. Pia hutumia utaratibu  wa kuwa karibu na wananchi ili kuwasaidia kutoa elimu juu ya masuala mbalimbali ya kisheria . Mahakama  hiyo kwa mwaka wanapokea  wastani wa mashauri 800 . 

    

Kwa upande wake Mtendaji Kata ya  Igulwa eneo  ambalo, Mahakama ya Wilaya ya Bukombe ilipo alisema anaishukuru Serikali kwa kuwapatia huduma hiyo, ambayo ina nafasi kubwa , ikiwemo Mahakama ya Mwanzo ya Ushirombo, ambapo  kwa sasa kila mtumishi ana chumba chake cha kufanyia kazi hali inayosababisha mashauri kumaliza saa 4.00 asubuhi  na wananchi wanapata muda kuendelea  na shughuli nyingine.

Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Bukombe lilizinduliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma Desemba 19 mwaka jana.

Mahakama ya Tanzania kupitia Mapango Mkakati wake wa Miaka Mitano, ambao unasisitiza kwamba utoaji haki kwa wote na kwa wakati  iliweka utaratibu wa muda wa kusikiliza shauri mahakamani katika Mahakama za Wilaya  kuwa lisidi miezi 12 na Mahakama za Mwanzo lisikilizwe katika kipindi cha miezi sita.