

……………………………………………………………………
NA MWAMVUA MWINYI, BAGAMOYO
TAASISI ya kifedha ya Stanbic imejivunia,kuwa wadau wakubwa katika medani ya soka, wakigusia michuano mikubwa ya kombe la Dunia na Ligi Kuu ya nchini Uingereza.
Hatua hiyo ambayo benki hiyo imekuwa ikiichukua katika medani ya michezo hususani soka, imeelezwa kuwa kivutio kikubwa kwa mamilioni ya wapenda soka kutokana na kujitangaza kupitia mashindano hayo.
Hayo yalielezwa na meneja wa benki ya Stanbic nchini ,Richard Chenga kwa niaba ya Mkurugenzi, akizungumza na Wanafunzi wa Kidato cha tano na sita wa shule ya Sekondari ya Kikaro, iliyopo kijiji cha Mioni,kata ya Miono Halmashauri ya Chalinze, Bagamoyo,Pwani.
Alisema, wana- Miono wana kila sababu ya kuitumia benki hiyo kutokana na kujitoa kwao katika kuoneshwa kwa michezo hiyo, inayopendwa ulimwenguni, huku wakazi hao wakiwemo katika watu wanaofuatilia michezo hiyo.
“Kwa kuthamini mchango mkubwa wa wana-Miono ambao ni sehemu ya wateja wetu, leo tumekuja kuleta sehemu ya faida yetu kwenu kwa kuleta vifaa tiba vikiwemo vitanda na vitu mbalimbali vikigharimu sh. Mil. 9.4 vitavyoboresha upatikanaji wa huduma kwenu,” alisema Chenga.
Akiambatana na mwenyeji wake Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete, Chenga baada ya kuwasalimia wanafunzi hao alisema kuwa benki hiyo imekabidhi vifaa hivyo ikiwa ni sehemu ya faida wanayoipata kupitia wateja wana-Miono hao.
Kwa upande wake Ridhiwani aliupongeza uongozi wa benki hiyo kwa kuungana na wanafamilia wa Mpira wa Miguu ulimwemguni, kwani matangazo ya benki hiyo yamekuwa chachu kwa mashabiki wanaofuatilia ligi hizo.