Mwenyekiti wa Baraza la Veterinari, Profesa Rudovick Kazwala akiongea na Vyombo vya Habari muda mfupi baada ya kumaliza Mkutano wa 45 wa Baraza la Veterinari ulilofanyika jijini Dodoma Juni 4, 2020.
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Tanzania, Profesa Hezron Nonga akifafanua jambo mbele ya Vyombo vya Habari katika Mkutano wa 45 wa Baraza la Veterinari ulilofanyika jijini Dodoma Juni 4, 2020.
Mwenyekiti wa Baraza la Veterinari, Profesa Rudovick Kazwala (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza hilo muda mfupi baada ya kumaliza Mkutano wa 45 wa Baraza la Veterinari ulilofanyika jijini Dodoma Juni 4, 2020. Wa kwanza kulia waliokaa ni Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Tanzania, Profesa Hezron Nonga, wa pili ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Veterinari, Dkt. Bhakilana Mafwere. Wa kwanza kushoto waliokaa ni Kaimu RASI wa Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Afya ya Sayansi ya Jamii – Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Profesa Elliot Phiri, na wa pili ni Msajili wa Baraza la Veterinari, Dkt. Bedan Masuruli.
…………………………………………………………………………
Na Mbaraka Kambona,
Baraza la Veterinari nchini Tanzania limewataka watu wote ambao hawana sifa za Udaktari wa Mifugo kuacha mara moja kuhudumia na kutibu Mifugo huku likionya kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa watakao kwenda kinyume na Sheria.
Onyo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Veterinari, Profesa Rudovick Kazwala katika Mkutano wa 45 wa Baraza hilo ulilofanyika jijini Dodoma Juni 4, 2020.
Akiongea na Vyombo vya Habari mara baada ya Mkutano huo, Profesa Kazwala alisema kuwa kutokana na fani hiyo ya Udaktari wa Mifugo kuingiliwa na watu wasiokuwa na sifa, Baraza limeamua kuandaa vitambulisho na beji vitakavyowatambulisha Madaktari hao pindi wanapokwenda kutoa huduma kwa wafugaji.
“Wale wote wanaojiingiza katika fani hii bila kuwa na vyeti vya kitaaluma wajue kuwa kuna sheria namba 16 ya Veterinari ya mwaka 2003 ambayo inakataza mtu ambaye hajasomea taaluma ya Udaktari wa mifugo kufanya kazi ya kuhudumia na kutibu mifugo, atakayekutwa na kosa hilo sheria itachukua mkondo wake” alisema Profesa Kazwala
Alisisitiza kuwa kuanzia sasa wafugaji wanapaswa kujua kuwa wataalamu wa mifugo watakuwa na vitambulisho vitakavyokuwa vinatolewa na Baraza hilo na kuwataka kuwakataa watu watakaokuwa wanakwenda kutaka kutibu mifugo yao bila kitambulisho.
“Huko nyuma hatukuwa na vitambulisho, kukosekana kwa vitambulisho kulipelekea watu wasio na sifa kujiingiza katika kazi ya tiba ya mifugo na kuchafua sifa za fani yetu”, Profesa alifafanua
Kufuatia changamoto hiyo, Profesa Kazwala alisema mkutano huo umekubaliana na kupitisha maamuzi kuwa wataalamu wa mifugo wawe na vitambulisho ambavyo vitasaidia kuzuia na kuwaondoa watu wasio na sifa ya udaktari wa mifugo.
Aliongeza kuwa watahakikisha wakaguzi wa mifugo wanapita kila mara kwa wafugaji kukagua mifugo yao na kufuatilia kama kuna watu kama hao ambao wanaendelea kuvunja sheria.
Profesa Kazwala ametoa wito kwa wafugaji na wananchi kwa ujumla kushirikiana na Baraza hilo kuwakataa watu hao wasio na vitambulisho huku akiwasisitiza hata hao madaktari watakaokuwa na vitambulisho wanapokwenda kutibu mifugo yao kuweka kumbukumbu zao vizuri ikiwemo namba ya usajili ya mtaalamu huyo ili kama likitokea tatizo lolote litakalo sababishwa na mtaalamu huyo iwe rahisi kumtambua.
Aidha, Profesa Kazwala amewaeleza wananchi kuwa huduma za mifugo zinaendelea kuboreshwa nchini na kuanzia sasa vituo vyote vinavyotoa matibabu ya wanyama lazima viwe na vifaa vya kuchunguza mifugo kwa maana ya Darubini ili kutoa vipimo sahihi vya Sampuli zitakazokuwa zinachukuliwa kutoka kwa mifugo.