*********************************
NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA VIJIJINI
NAIBU Waziri Wa Maji ,Jumaa Aweso ameiagiza RUWASA na DAWASA Mkoani Pwani ,kuongeza uzalishaji wa maji na kusimamia mradi wa maji wa Kipangege Kibaha ,ili wananchi wanaondokane na tatizo la kupata maji kwa mgao ,kwani wananchi hao wamechoshwa na maji ya kudunduliza .
Aidha ameielekeza ,RUWASA Mkoani hapo ,kuhakikisha wanamuondoa msimamizi wa mradi wa maji wa Kipangege, Kibaha na kuurudisha mradi mikononi mwa Jumuiya ya watumiaji ili kuondoa kero ya upatikanaji wa maji ya uhakika na kuchota maji kwa sh .150-200 kwa ndoo badala ya sh.100 iliyopangwa.
Aweso alitoa maagizo hayo ,wakati alipofanya ziara ya siku moja ,Kibaha Vijijini kufuatilia maelekezo aliyoyatoa yafanyiwe kazi katika mradi wa maji Kipangege ambao aliutembelea mwishoni mwa mwaka jana .
Alieleza ,adhma ya Serikali ya awamu ya tano ,chini ya Rais dkt.John Magufuli ni kumtua mama ndoo kichwani hivyo juhudi ziendelee ili kutimiza adhma hiyo .
“:Nilipata ombi la kuja hapa kutoka kwa mbunge wenu Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa , mwezi Desemba 2019 nilifika na nilitoa maagizo RUWASA Mkoa ,wilaya na DAWASA kuufuatilia mradi na kuhakikisha maji yanatoka “
“Nashukuru maji yalianza kutoka toka January mwaka huu lakini tatizo bado ni mgao unaosababisha kero pamoja na usimamizi mbovu kwa mkandarasi aliyekabidhiwa na wananchi awasimamie ,ni bora mradi urudi kwa wananchi waendeshe wenyewe, kwakuwa ni kwa ajili yao ,wanufaike nao na sio kumnufaisha mtu mmoja ” alisisitiza Aweso .
Hata hivyo ,Aweso alimtaka ofisa ununuzi RUWASA kuharakisha mchakato wa manunuzi ya vifaa vinavyotakiwa kwenye kuongeza kituo kimoja cha kuchotea maji ,”;kuboresha mradi kwa kujenga mnara na ununuzi wa tanki la lita 10,000 ili kuongeza upatikanaji wa maji kwa haraka.
Nae mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa ,alisema Kipangege ulikuwa na shida ya maji kwa miaka mingi hivyo ujio wa Naibu Waziri huyo umewanufaisha wakazi hao .
Jumaa aliishukuru serikali ,RUWASA ,na DAWASA kwa juhudi yao katika upatikanaji wa maji kwenye baadhi ya maeneo jimboni hapo ikiwa ni moja ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi .
Mwenyekiti wa Kipangege Shomari Jumaa,alieleza wanapata maji kwa mgao ambapo marekebisho na uboreshaji ukifanyika wataendelea kunufaika na mradi huo .
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Pwani ,Beatrice Kasimbazi alipokea maagizo yote na kusema watahakikisha wanaupokonya usimamizi wa mradi kwa mkandarasi na kuukabidhi kwa wananchi.
Alielezea ,ili kuboresha mradi kwa kujenga mnara wa mita 6 na tanki la lita 10,000 na kuongeza kituo kimoja cha kuchotea maji mchakato wa ununuzi wa vifaa tayari unafanyika na upo mwisho kukamilika .
Kasimbazi alifafanua ,mradi wa Kipangege ni kati ya miradi 26 mkoani Pwani ,na Kibaha ni mradi mmoja uliokuwa na changamoto , uliotegemewa kukamilika 2014 ulisuasua na RUWASA ilipoanzishwa ulifanyiwa kazi na kuanza kutoa maji January 2020 .